Necta yabadili ratiba ya mitihani, tahadhari ya El Niño
- Marekebisho hayo yanahusu mitihani na upimaji iliyokuwa imepangwa kufanyika katika kipindi cha Oktoba na Novemba 2026, huku hatua hiyo ikilenga kuhakikisha shughuli hizo zinafanyika katika mazingira salama.
Dar es Salaam. Baraza la Mitihani Tanzania (Necta) limefanya marekebisho ya ratiba ya Upimaji na Mitihani ya Taifa ya mwaka 2026 iliyokuwa ifanyike Oktoba na Novemba, kutokana na tahadhari ya uwezekano wa mvua kubwa za El Niño.
Mabadiliko hayo yamelenga kuhakikisha usalama wa wanafunzi, walimu, wasimamizi na maofisa wengine wanaohusika na uendeshaji wa mitihani, pamoja na kulinda mitihani, vifaa na nyaraka zinazohusiana na mitihani hiyo.
Akizungumza leo Ijumaa, Septemba 25, 2026, Naibu Waziri wa Elimu, Wanu Hafidh Ameir amesema uamuzi huo umefikiwa baada ya Wizara ya Elimu kupokea taarifa kutoka mikoa mbalimbali kuhusu maandalizi ya kukabiliana na athari zinazoweza kusababishwa na mvua hizo.
Amesema pamoja na maandalizi hayo, wizara imeona kuna umuhimu wa kufanya marekebisho ya ratiba ili kupunguza changamoto zinazoweza kujitokeza iwapo mvua kubwa zitanyesha katika kipindi ambacho mitihani hiyo ilikuwa ikifanyika.
“Lengo la marekebisho ya ratiba ni kuhakikisha usalama wa wanafunzi, walimu, wasimamizi na maofisa wengine wanaohusika na uendeshaji wa mitihani, pamoja na kulinda mitihani, vifaa na nyaraka za mitihani, iwapo mvua kubwa zitatokea mwezi Novemba 2026,” amesema.
Kwa mujibu wa Katibu Mtendaji wa Necta, Profesa Said Mohamed, upimaji wa kitaifa wa Darasa la Nne sasa utafanyika Oktoba 5 na 6, 2026, badala ya Oktoba 21 na 22, 2026.
Upimaji wa kitaifa wa Darasa la Pili ambao awali ulipangwa kufanyika Novemba 17 na 18, 2026, sasa utafanyika Oktoba 7 na 8, 2026.
Aidha, upimaji wa kitaifa wa Kidato cha Pili umehamishwa kutoka Novemba 2 hadi 13 na sasa utafanyika kuanzia Oktoba 12 hadi 23, 2026.
Kwa upande wa mtihani wa Taifa wa Kidato cha Nne, ambao awali ulipangwa kuanza Novemba 9 hadi 27, 2026, sasa utaanza Oktoba 19 na kukamilika Novemba 6, 2026.
Kwa mujibu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), msimu wa mvua za Vuli 2026 unatarajiwa kuathiriwa kwa kiwango kikubwa na hali ya El Niño, huku mvua zikitarajiwa kuanza mwishoni mwa Septemba hadi wiki ya kwanza ya Oktoba, na kuongezeka zaidi Novemba hali inayotazamiwa kuleta athari mbalimbali ikiwemo mafuriko.