Africa Agri Expo 2026 yafungua dirisha, masoko ya kimataifa kwa wakulima Tanzania
- Ni kwa mara ya kwanza maonyesho hayo yanafanyika Tanzania yakiwakutanisha wakulima, wafugaji, wafanyabiashara, kujifunza kuhusu teknolojia mpya, bidhaa, huduma, masoko na fursa za biashara katika sekta hiyo.
Dar es Salaam. Kwa mkulima wa Tanzania, kuzalisha mazao mengi ni jambo moja, lakini kupata soko la uhakika la kuyauza mazao hayo ili kujipatia kipato ikiwemo kwenye masoko ya kimataifa, ni safari nyingine yenye changamoto zake.
Hili ni moja ya masuala yaliyoibuliwa katika maonyesho ya 10 ya Africa Agri Expo 2026, yaliyofanyika kwa mara ya kwanza nchini Tanzania.
Africa Agri Expo 2026 ni jukwaa linalowakutanisha pamoja wakulima, wafugaji, wafanyabiashara, wataalamu, wawekezaji na watoa huduma katika sekta za kilimo, chakula, mifugo na ufugaji wa kuku.
Maonyesho hayo ambayo kwa mwaka huu yamefanyika kuanzia Septemba 2 hadi 3 katika viwanja vya Sabasaba jijini Dar es Salaam yaliandaliwa na kampuni ya uandaaji maonyesho ya Tab group kutoka nchini India.
Katika maonyesho hayo, wakulima, wafugaji, wafanyabiashara, wataalamu na watoa huduma katika sekta za kilimo, chakula, mifugo na kuku, walipata fursa ya kujifunza kuhusu teknolojia mpya, bidhaa, huduma, masoko na fursa za biashara katika sekta hiyo.
Kwanini Tanzania ?
Mkurugenzi wa TAB Group, Tahir Abdul, amesema Tanzania ina nafasi kubwa ya kunufaika na biashara ya kilimo kutokana na uwezo wake wa uzalishaji na nafasi yake katika biashara ya kikanda.
Akizungumza na Nukta Habari, Tahir amesema moja ya umuhimu wa Africa Agri Expo ni kuwakutanisha wazalishaji na wadau kutoka masoko mbalimbali, ili bidhaa zinazozalishwa Tanzania ziweze kupata fursa ya kuonekana na kufikia wanunuzi na wawekezaji.

“Tunaona fursa nyingi zitokanazo na kilimo kwenye soko la Tanzania. Tanzania ni moja kati ya kitovu kikuu cha biashara katika ukanda wa Afrika Mashariki,” amesema Tahir.
Tahir amebainisha kuwa maonyesho hayo yanatoa nafasi kwa wafanyabiashara na wazalishaji kukutana na kujifunza kuhusu teknolojia na kutafuta fursa za masoko ya kimataifa.
Sekta ya kilimo inakua
Kwa mujibu wa Wizara ya Kilimo, uzalishaji wa mazao ya chakula Tanzania ulifikia tani milioni 23.78 msimu wa 2024/2025, kutoka tani milioni 22.8 msimu uliotangulia, huku sekta ya kilimo ikichangia asilimia 24.6 ya Pato la Taifa mwaka 2025.
Wakati huo huo, mauzo ya nje ya mazao yaliongezeka kwa asilimia 51.9, kutoka Dola za Marekani bilioni 2.33 mwaka 2022/2023 hadi Dola za Marekani bilioni 3.54 mwaka 2023/2024, jambo linaloifungulia fursa Tanzania kuuza bidhaa kimataifa.
Hata hivyo, ili wakulima wanufaike zaidi, kuna umuhimu wa kuwaunganisha na masoko pamoja na elimu ya kuzalisha bidhaa zenye viwwango ili ziweze kuvuka mipaka ya kimataifa kwa mujibu wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS).
Vijana: Kilimo si cha wazee
Kwa muda mrefu, kilimo kimekuwa kikihusishwa zaidi na watu wa vijijini au kizazi cha wazee. Vijana waliohudhuria maonyesho hayo wameonesha mtazamo tofauti kwamba kilimo kinaweza kuwa biashara kwa kizazi kipya na si lazima mtu awe na mtaji mkubwa kuanza.
Esabela Jacob (23) anayejishughulisha na kilimo cha mwani kwa miaka miwili ameiambia Nukta Habari kuwa aliona fursa katika kilimo kwa sababu mahitaji ya chakula yanaendelea kuwepo ndani na nje ya Tanzania.

“Tuna utajiri mwingi sana wa ardhi, mimi nikaona nijikite huko kwa sababu niliona fursa ya chakula kinahitajika kwa wingi na sio ndani ya Tanzania tu bali hata sehemu tofauti tofauti za nje,” amesema.
Kwa upande wake, Eliakim Ruthu, mjasiriamali anayejishughulisha na kilimo cha mbogamboga na ufugaji wa kuku kwa miaka saba anasema mtaji mkubwa si lazima uwe kigezo cha kwanza cha kuingia kwenye kilimo unaweza kuanza mtaji kidogo ulionao
‘Tumieni chapa ya Made in Tanzania’
Wakati fursa za masoko ya kimataifa zikijadiliwa, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade), Ephraim Mafuru, amesisitiza umuhimu wa Tanzania kujenga chapa imara ya bidhaa zake.
Akizungumza na Nukta Habari katika maonyesho hayo, Mafuru amewahamasisha wafanyabiashara na wazalishaji kutumia chapa ya “Made in Tanzania”, huku akisisitiza kuwa bidhaa inayolenga soko la kimataifa inapaswa pia kuzingatia ubora, ufungashaji na uongezaji thamani.
“Wafanyabiashara wa Tanzania tutumie vifungashio vilivyotengenezwa Tanzania, vilivyo na ubora wa kufika sokoni, sio bidhaa za Tanzania inatengenezwa na vifungashio vingine, alafu inapitia nchi nyingine alafu inaenda kutangazwa kama export ya hiyo nchi,” amesema Mafuru.
Nukta Africa ndani ya maonyesho
Nukta Africa ni moja kati ya wadau walioshiriki katika maonyesho hayo ikiwa kama mshirika wa habari.

Kwa zaidi ya miaka nane, Nukta Africa imekuwa ikichangia katika sekta ya habari, teknolojia na biashara kwa kutumia habari, data, teknolojia na ubunifu kuwaunganisha wananchi na taarifa, maarifa na fursa zenye umuhimu kwa maisha na shughuli zao za kiuchumi.
Kupitia maonyesho hayo Nukta Africa ilipata nafasi ya kuonyesha bidhaa na huduma katika banda lao ambapo moja katika huduma bidhaa nyingi walizoonyesha ilikuwepo Nukta AI ambayo iliwavutia watazamaji wengi.