Deogratius Ndejembi apendekezwa kumrithi Nchimbi
- Ni baada ya takribani saa 26 tangu Rais Samia aridhie kujiuzulu kwa Dk Nchimbi ambaye pia amefutwa uanachama wa CCM kuanzia leo Agosti 26, 2026.
Dar es Salaam. Chama cha Mapinduzi (CCM) kimempendekeza Deogratius Ndejembi kuwa Makamu wa Rais kuchukua nafasi ya Dk Emmanuel Nchimbi aliyejiuzulu wadhifa huo na kufutwa uanachama wa chama hicho tawala nchini.Â
Katibu Mkuu wa CCM, Dk Asha Rose-Migiro amewaambia wanahabari usiku wa leo Jumatano, Agosti 26, 2026 jijini Dar es Salaam kuwa Halmashauri Kuu ya CCM imependekeza jina Ndejembi na kwamba kwa sasa zinafuata taratibu za kikatiba ili likapitishwe na Bunge.Â
Ndejembi, ambaye kwa sasa ni Waziri wa Nishati, iwapo atapitishwa na Bunge siku chache zijazo atakuwa Makamu wa Rais wa tatu ndani ya miaka mitano ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan. Ndejembi mwenye miaka 43, ataingia kwenye historia ya kuwa moja ya viongozi walioshika nafasi hiyo ya juu nchini baada ya Rais akiwa na umri mdogo.Â
Taarifa hiyo ya CCM inakuja ikiwa ni takribani saa 26 tangu Rais Samia Suluhu Hassan apitishe ombi la Dk Nchimbi aliyetangaza kujiuzulu Agosti 25 mwaka huu. Dk Nchimbi alieleza katika taarifa yake kwa umma kuwa atang’atuka ifikapo Septemba 4, 2026.
Kwa mujibu wa Katiba ya Tanzania mara kiti cha makamu wa rais kinapokuwa wazi kwa sababu yeyote iliyoainishwa ikiwamo kujiuzulu ndani ya kipindi kisichozidi siku 14 Rais atapendekeza jina makamu wa rais ambaye atatakiwa kupitishwa kwa kura ya wabunge walio wengi.Â
Huu ni mwisho wa enzi Dk Nchimbi kisiasa?
Licha ya Rais Samia kuridhia kujiuzulu kwa Dk Nchimbi, CCM kimetangaza kumfuta uanachama kiongozi huyo namba mbili kutokana na utovu wa nidhamu na maadili.Â
Dk Migiro amesema Kamati Kuu na Halmashauri Kuu kwa pamoja vimeridhika pasipo kuacha shaka kuwa Dk Nchimbi alivunja Katiba na kanuni za chama hicho ambacho kimekuwa madarakani tangu Tanzania ipate uhuru takriban miaka 65 iliyopita.Â
Hatua ya CCM kumfukuza uanachama Dk Nchimbi itakuwa ni pigo kwa kiongozi huyo ambaye alikuwa akitajwatajwa na baadhi ya wachambuzi kuwa huenda akafaa kuwania urais mwaka 2030.Â
Awali Nukta Habari ilizungumza na Wakili Peter Majanjara kutoka Chika Attorneys ambaye alibainisha kuwa licha ya Rais Samia kuridhia ombi la Nchimbi kujiudhuru, bado Dk Nchimbi anasalia kuwa makamu wa Rais hadi pale atakapo ng’atuka rasmi Septemba 4.
Hii ina maana kuwa siku 14 zinazotoa nafasi ya kufanyika kwa mchakato wa kumpata Makamu wa Rais Mpya zitaanza kuhesabiwa kuanzia Septemba 4 siku ambayo Nchimbi ataachia madaraka rasmi.
Hata hivyo, Majanjara anaeleza kuwa katiba haijaweka wazi kwamba ni nini kitatokea iwapo siku hizo 14 zitapita.