Maboresho mifumo ya kibenki yanavyoweza kuathiri uchumi Tanzania

August 6, 2026 5:10 pm · Kelvin Makwinya
Share
Tweet
Copy Link
  • Pamoja na maboresho, taasisi za kifedha zinapaswa kuwa na mifumo mbadala ya kuhakikisha huduma haziingiliwi wakati wa matengenezo. 

Dar es Salaam. Umewahi kufikiria kitakachotokea endapo mifumo ya huduma za kifedha, ikiwemo benki, itapata hitilafu na kukufanya ushindwe kabisa kutoa au kupokea fedha?

Huenda ukasema utasubiri mifumo irejee katika hali ya kawaida au utatumia akiba yako. Lakini je, hitilafu hiyo ikidumu kwa siku, wiki au hata mwezi mmoja, maisha yako na shughuli zako za kiuchumi zitaathirikaje?

Katika uchumi wa sasa unaotegemea miamala ya kidijitali kwa kiasi kikubwa kusimama kwa huduma za kifedha kunaweza kuvuruga shughuli za kila siku za wananchi, wafanyabiashara na taasisi mbalimbali.

Wakala wa benki, Jeniffer Godwin anayefanya biashara Kinondoni jijini Dar es Salaam, ameiambia Nukta Habari kuwa kukosekana kwa huduma za kibenki wakati fulani kumepelekea ofisi yake kupoteza wateja wengi na kupunguza idadi ya miamala aliyokuwa akifanya.

Godwin, ambaye kipato chake hutegemea idadi ya wateja na thamani ya miamala anayohudumia, amesema changamoto hiyo husababisha kukosekana kwa mapato kutokana na kupungua kwa shughuli za biashara katika uwakala wake.

“Kwa sababu wanalipa kwa kamisheni, nimekosa tayari kamisheni siku mbili tatu,” ameeleza Godwin

Ahmed Khan, mmoja wa wateja wa huduma za benki, kupitia mtandao wa kijamii wa Instagram ameeleza athari za kukosekana kwa huduma za kibenki kulivyovuruga shughuli zake za kibiashara.

Khan ametolea mfano marekebisho ya mifumo yaliyofanyika katika moja ya benki nchini Tanzania kuanzia Julai 31, 2026, kulivyomzuia kufanya malipo kwa wasambazaji na kushughulikia miamala ya wateja.

“Kila siku inayopita bila huduma inatugharimu katika shughuli zetu za kibiashara,” ameandika Khan katika mtandao wa Instagram.

‘Inapunguza kasi ya ukuaji uchumi’

Mchambuzi wa uchumi na fedha kutoka Dar es Salaam, Paul Chengula, anasema maboresho ya mifumo ni sehemu ya maendeleo ya kawaida katika sekta ya huduma za kifedha, hasa katika kipindi ambacho taasisi za fedha zinaimarisha mifumo yao kukabiliana na ongezeko la hatari za kimtandao na kuboresha ubora wa huduma kwa wateja.

Hata hivyo, anasisitiza kuwa pamoja na maboresho hayo, ni muhimu kwa taasisi za kifedha kuwa na mifumo mbadala ya utoaji huduma ili kuhakikisha huduma zinaendelea kutolewa hata pale mfumo mkuu unapokuwa katika matengenezo au unapokumbwa na changamoto za kiufundi.

Chengula anasema kusimama kwa huduma za kifedha zinazotumiwa na mamilioni ya Watanzania hakuachi athari kwenye sekta ya benki pekee bali katika uchumi wote.

Kwa mujibu wa Chengula, kuchelewa kwa biashara, malipo na shughuli nyingine za kiuchumi, kupunguza kasi ya ukuaji wa uchumi hususan katika kipindi ambacho Tanzania inalenga kujenga uchumi wa dola za Marekani trilioni moja unaotegemea teknolojia ifikapo mwaka 2050.

“Kwa sababu Serikali itakosa mapato, benki zitakosa mapato, hao mawakala na hata watumiaji, fikiria kuna malipo ya kiuzalishaji unatakiwa kuyafanya alafu haiweekani,” amesema Chengula.

Ili kukabiliana na changamoto hiyo, ameshauri Watanzania kutotegemea njia moja pekee ya kufanya miamala ya kifedha. 

Anasema kuwa na zaidi ya akaunti moja ya benki, au kuchanganya akaunti za benki na huduma za fedha kwa njia ya simu, kunaweza kusaidia kupunguza athari endapo huduma za taasisi moja zitakumbwa na changamoto za muda. 

Tanzania yakumbatia miamala kidijitali 

Changamoto za kusimama kwa huduma za kifedha zimeibuka katika kipindi ambacho Tanzania inaongeza kasi ya mageuzi ya kidigitali, ikiwa na lengo la kujenga uchumi wa Dola za Marekani trilioni moja ifikapo mwaka 2050 unaotegemea zaidi teknolojia, mifumo ya malipo na huduma za kidigitali. 

Juni 30, 2026, Serikali ilitoa ilitoa amri inayotaka malipo katika miamala iliyoainishwa kufanyika kwa njia za kielektroniki pekee, hatua inayobadilisha namna wananchi na wafanyabiashara watakavyofanya malipo katika huduma mbalimbali nchini.

Amri hiyo ya miamala ya kielektroniki ya mwaka 2026 (Electronic Transactions Order, 2026), imeweka utaratibu huo katika sekta mbalimbali, ikiwa ni sehemu ya kupunguza utegemezi wa fedha taslimu na kuongeza matumizi ya malipo kidigitali katika uchumi wa Tanzania.

Kwa mujibu wa amri iliyotolewa, kuanzia Julai mosi 2026 malipo katika huduma mbalimbali na biashara nchini yanatakiwa kufanyika kwa njia za kielektroniki pekee. 

Fedha taslim sasa basi

Kwa lugha rahisi inamaana kuwa sasa Mtanzania atahitaji kuwa na njia ya malipo ya kidigitali kama vile akaunti ya benki au huduma za fedha kupitia mitandao ya simu kufanya malipo kwenye shughuli zake za kila siku.

Huduma hizo ni pamoja na huduma za usafiri ikiwemo mwendokasi, vivuko, treni, usafiri wa anga, mabasi ya mikoani, teksi za mitandaoni, madaraja ya kulipia na maegesho ya magari.

Aidha, sekta za biashara kama vile maduka makubwa, vituo vya mafuta, kumbi za mikutano na sherehe, viwanja vya michezo, hoteli na migahawa vyote vimejumuishwa katika utaratibu huo.

Kadhalika katika sekta ya elimu, ada na michango ya shule za awali, msingi, sekondari, vyuo vya kati na vyuo vikuu vinatakiwa kupokelewa kwa njia za digitali.

Malipo katika shughuli za utalii, upangishaji au ununuzi wa nyumba, viwanja na mashamba, biashara ya vyombo vya moto pamoja na shughuli za kilimo nazo zitaendeshwa kupitia mifumo ya malipo ya kielektroniki.

Kwa upande wa mfanyabiashara anatakiwa kuwa na miundombinu kama vile mashine za malipo za POS, namba za malipo (Lipa Namba) au ‘Merchant Code’ ili kuwawezesha wateja kufanya malipo bila kutumia fedha taslimu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Masoko & Zaidi
Loading…
No recent matches
No upcoming matches
/
No matches found for this filter
No forex gainers today
No forex losers today
Forex rates unavailable
6 Aug, 2026 · TZS
No gainers today
No losers today
6 Aug, 2026
No active movers today

Inaendeshwa na Nukta AI

Follow us on TikTok

Nukta Habari

FOLLOW NOW
Subscribe to our channel

Nukta TV

SUBSCRIBE NOW
Sh10,000 sasa kununua lita 2.57 za petroli, lita 2.51 za dizeli mwezi Agosti

Sh10,000 sasa kununua lita 2.57 za petroli, lita 2.51 za dizeli mwezi Agosti

Nukta TV

NISHATI

NISHATI

Nukta TV

Utani wa Rais Samia kwa wachimba madini wa Katoro

Utani wa Rais Samia kwa wachimba madini wa Katoro

Nukta TV