Hisa au hati fungani? Mtihani mkubwa kwa mwekezaji

August 4, 2026 12:43 pm · Kelvin Makwinya
Share
Tweet
Copy Link
  • Hisa humfanya mnunuaji kuwa sehemu ya umiliki wa kampuni, hati fungani humfanya mwekezaji kuwa mkopeshaji kwa Serikali au taasisi.

Dar es Salaam. Kadiri changamoto za kiuchumi na kutokuwa na uhakika wa kipato kwa siku za baadae zinavyoendelea kujitokeza, watu wengi hasa vijana wameanza kuangalia kwa makini maeneo ya fursa za uwekezaji yatakayoweza kuwapatia usalama wa kifedha katika siku zijazo.

Miongoni mwa maeneo ambayo kwa sasa yamegeukiwa kwa kasi ni uwekezaji katika masoko ya mitaji, hususan kupitia hisa na hati fungani.

Kwa sasa, vijana wengi wanaona uwekezaji huu ndiyo njia salama na ya uhakika zaidi kuzalisha kipato kulinganisha na njia nyingine kama kuanzisha biashara ambayo wakati mwingine hukosa uhakika wa faida na kuhitaji nguvu nyingi.

Mwelekeo huu unachochewa zaidi na elimu ya fedha na upatikanaji wa taarifa hususan kupitia mitandao ya kijamii huku wengi wakivutiwa na hadithi za faida za haraka kutoka kwenye mitandao hiyo.

Hata hivyo, licha ya vijana kuinukia kuwekeza katika masoko ya mitaji wengi wao bado wanawekeza bila kuwa na elimu ya fedha jambo linaloweka uwekezaji wao kwenye hatari.

Utofauti upo wapi?

Kwa mujibu wa Imani Muhingo, Meneja Mwandamizi, Huduma za Uwakilishi wa Hisa, Benki ya CRDB kununua hisa ni sawa na kuwekeza au kununua sehemu ya kampuni iliyoorodheshwa katika soko la hisa. 

Muhingo anaeleza kuwa mwekezaji anayenunua hisa hupata faida kwa njia kuu mbili ambazo ya kwanza ni kupitia gawio la faida ambalo hugawanywa kwa wamiliki na ya pili ni kupitia kuongezeka kwa thamani ya hisa sokoni zinazomwezesha mwekezaji kuuza hisa zake kwa faida.

“Kama utanunua hisa moja kwa Sh500 sasa, kutokana na kampuni kukua bei ya hisa ikapanda na kufikia Sh5,000 kwa hisa moja, thamani ya hisa zako itakuwa imeongezeka mara 10 zaidi” anaeleza Muhingo.

Kwa sasa, kuna makampuni 28 yaliyoorodheshwa katika Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE), ambapo 22 ni ya ndani ya Tanzania na sita ni ya nje yaliyosajiliwa pia kufanya biashara katika soko hilo. 

Miongoni mwa kampuni zinazofanya vizuri zaidi kwa kuzingatia faida, gawio, thamani ya soko na mwenendo wa hisa ni NMB Bank Plc, CRDB Bank Plc, Tanzania Breweries Limited (TBL), Tanzania Cigarette Corporation (TCC), Vodacom Tanzania Plc, Dar es Salaam Stock Exchange Plc (DSE) na Twiga Cement Plc. 

Wakati hisa humfanya mnunuaji kuwa sehemu ya umiliki wa kampuni, hali ipo tofauti kwa upande wa hati fungani ambayo inamfanya mwekezaji kuwa mkopeshaji.

Kwa sasa, kuna makampuni 28 yaliyoorodheshwa katika Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE), ambapo 22 ni ya ndani ya Tanzania na sita ni ya nje yaliyosajiliwa pia kufanya biashara katika soko hilo. Picha | Gustaph Goodluck | Nukta Habari.

Afisa Masoko kutoka UTT AMIS, Paschazia Charles aliiambia Nukta Habari kuwa hati fungani (bonds) ni bidhaa ya kifedha iliyoorodheshwa sokoni inayowezesha wawekezaji kununua deni la mkopeshaji kwa muda maalum.

Kwa maneno mengine, kununua hati fungani ni kama kumpa mtu mkopo kwa riba ambapo baada ya muda wa makubaliano kufika, mtu yule atakurudishia fedha zako pamoja na kiasi cha riba ambacho mkopeshaji hukipata kama faida.

Kwa mfano ukiwekeza kiasi cha Sh100,000 kwenye hati fungani yenye riba ya asilimia 12 kwa mwaka kwa muda wa miaka 5, utapokea malipo ya riba ya Sh12,000 kila mwaka bila kupoteza mtaji ambao utarudishiwa mwisho wa kipindi cha makubaliano. 

Soko la mitaji lazidi kukua

Amko la vijana katika kuwekea kwenye masoko ya mitaji, unakwenda sambamba na ukuaji wa masoko hayo nchini.

Ripoti ya Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana ya mwaka 2023 – 2024 katika mwaka ulioishia Juni 30, 2024, inaonyesha jumla ya thamani ya miamala ya hisa na hati fungani iliongezeka kwa asilimia 13.8 na kufikia Sh3.88 trilioni, kutoka Sh3.41 trilioni mwaka 2023. 

Thamani ya jumla ya uwekezaji katika masoko ya mitaji, kwa mujibu wa ripoti hiyo, ilifikia Sh43.15 trilioni, ongezeko la asilimia 20.8 ikilinganishwa na Sh35.71 trilioni mwaka uliotangulia, hali inayoakisi mazingira mazuri ya kiuchumi na kuongezeka kwa uelewa wa umma.

Ripoti hiyo inaonyesha kuwa shughuli za biashara katika soko la hisa ziliongezeka kwa kasi kubwa, ambapo thamani ya hisa zilizouzwa ilipanda kwa zaidi ya asilimia 153 hadi kufikia Sh272.67 bilioni mwaka 2024, kutoka Sh107.58 bilioni mwaka 2023. 

Sambamba na hilo, idadi ya hisa zilizofanyiwa biashara iliongezeka hadi hisa milioni 252 kutoka milioni 113 mwaka uliopita, huku viashiria vikuu vya soko, ikiwemo Tanzania Share Index na DSE Share Index, vikirekodi ongezeko la kati ya asilimia 9 na 12.

Hati fungani nazo katika soko la awali, Serikali ilitoa hati fungani zenye thamani ya Sh3.73 trilioni, huku mahitaji ya wawekezaji yakizidi kiasi kilichotolewa, ishara ya imani kubwa ya soko. 

Aidha, biashara ya hati fungani za Serikali iliongezeka kwa zaidi ya asilimia 10 hadi kufikia Sh3.55 trilioni, wakati biashara ya hati fungani za kampuni binafsi ilipanda kwa zaidi ya asilimia 300. 

Upi ni uwekezaji bora?

Licha ya kuwepo kwa tofauti kati ya mifumo hii ya uwekezaji na baadhi ya watu kuelewa tofauti hizo, bado kumekuwa na mijadala miongoni mwa vijana kuhusu ni ipi uwekezaji bora, hali inayowafanya wengine kusita kufanya uamuzi sahihi wa kuwekeza.

Hata hivyo, ukweli ni kwamba fursa zote za uwekezaji ni nzuri bali ufanisi wa uwekezaji hutegemea malengo ya kifedha ya mwekezaji, muda wa uwekezaji, kiwango cha hatari anachoweza kuvumilia pamoja na ukubwa wa mtaji alionao mwekezaji.

Johari Mlowezi, mkazi wa Singida ni moja kati ya vijana waliogeukia uwekezaji kwenye masoko ya mitaji baada ya kujaribu biashara tofauti bila mafanikio.

Mlowezi ameiambia Nukta Habari kuwa malengo yake uwekezaji ya muda mrefu ndiyo yamemfanya apendelee kuwekeza zaidi kwenye hisa dhidi ya hati fungani jambo analokiri kumfanya awe na nidhamu ya fedha.

Unaweza kuwekeza kiduchu kiduchu

“Nikiwaza kuwa mchakato wa kuipata fedha yangu unachukua muda mrefu natafuta njia mbadala na uwekezaji wangu unakuwa salama… na hii ndo maana ya uwekezaji,” anasema Mlowezi.

Mlowezi ambaye kipato chake ni Sh300,000 kwa mwezi anasema hutumia hata kiasi cha Sh2,000 anayoipata kama akiba kuwekeza kwenye hisa jambo lililomsaidia kutimiza malengo yake ambayo asingeweza kutimiza kutokana na kutokuwa na uwezo wa kupata fedha nyingi kwa pamoja.

Wakati Mlowezi akiona hisa ni chaguo bora kwake kuwekeza, hali ipo tofauti kwa Maphosa Banduka ambaye huwekeza zaidi kwenye hati fungani.

Hati fungani uhakika

Maphosa, ambaye ana zaidi ya miaka minne tangu aanze kuwekeza, anasema huchagua hati fungani kutokana na malengo ya muda mfupi aliyonayo kwa kuwa hana haja ya kusubiri kwa muda mrefu ili kupata faida ya uwekezaji wake. 

“Pesa ya hati fungani ni pesa unayoweza kuipangia hesabu kwa sababu ni ya uhakika unajua kabisa ikifika wakati fulani itaingia…hisa zinaweza zikapanda na ukahitaji kuuza ili upate faida lakini ni lazima kuwepo na mnunuzi kwa wakati huo hivyo zinaweza pia kukaa muda mrefu sokoni, anasema.

Maphosa, ambaye huwekeza zaidi kwenye kampuni ya UTT Amis, anasema usalama wa uhakika wa mtaji wake kwenye hati fungani ni jambo linalompa ujasiri tofauti na hisa ambayo mara nyingine humweka mwekezaji katika presha kutokana na kupanda na kushuka kwa thamani ya mtaji wake.

“Uwekezaji kwenye hisa una faida kubwa lakini nahitaji uwekezaji ambao hata kama unanipatia faida ndogo lakini ni wa uhakika,” ameongeza  Maphosa.

Jipange unapotaka kuwekeza

Kwa mujibu wa wataalamu wa fedha na wazoefu wa uwekekezaji, hakuna jibu la moja kwa moja kuhusu uwekezaji upi ni bora kati ya hisa na hati fungani.

Muhingo anasema kwamba hisa huja na fursa ya faida kubwa zaidi, lakini pia hubeba hatari ya kupanda na kushuka kwa thamani ya mtaji wakati hati fungani ikitoa uhakika wa mapato ya riba na usalama wa mtaji, ingawa faida yake huwa ya wastani.

“Hasara pekee unayoweza kuipata kwenye hati fungani ni endapo kutakuwa na mfumuko wa bei ambao utashusha thamani ya pesa yako, lakini kiasi kitabaki kuwa kile kile,” anasema Muhingo.

Kwa mujibu wa Muhingo, swali halipaswi kuwa ni upi ni uwekezaji bora, bali ni uwekezaji upi unaendana na ndoto, uwezo na mipango wa kifedha wa mwekezaji husika.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Masoko & Zaidi
Loading…
No recent matches
No upcoming matches
/
No matches found for this filter
No forex gainers today
No forex losers today
Forex rates unavailable
4 Aug, 2026 · TZS
No gainers today
No losers today
4 Aug, 2026
No active movers today

Inaendeshwa na Nukta AI

Follow us on TikTok

Nukta Habari

FOLLOW NOW
Subscribe to our channel

Nukta TV

SUBSCRIBE NOW
NISHATI

NISHATI

Nukta TV

Utani wa Rais Samia kwa wachimba madini wa Katoro

Utani wa Rais Samia kwa wachimba madini wa Katoro

Nukta TV

Rais Samia: Misaada imepungua, tukaze buti

Rais Samia: Misaada imepungua, tukaze buti

Nukta TV