Fursa kwa wakulima, uhitaji mazao ya chakula ukiongezeka Kenya, Uganda

Huenda Tanzania ikawa na nafasi kubwa ya kuongeza mauzo ya mazao ya chakula katika nchi za Kenya na Uganda baada ya mauzo katika soko hilo kushuka kwa asilimia 70.
Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade) inabainisha kuwa katika mataifa hayo bado kuna uhitaji mkubwa wa chakula husasan mahindi, mchele, dengu na maharage ya soya.
Takwimu za TanTrade zinaonyesha mauzo ya mazao hayo katika soko la Uganda yalipungua kwa asilimia 71 ndani ya miaka mitano kutoka Dola za Marekani milioni 154 kwa mwaka 2021 hadi Dola za Marekani milioni 45 mwaka 2025.
Kwa upande wa soko la Kenya, mauzo yalishuka kwa asilimia 92 katika kipindi sawa na hicho yakipungua kutoka Dola za Marekani milioni 121 mwaka 2021 hadi Dola za Marekani milioni 10.
Licha ya mabadiliko ya kiwango cha mauzo katika miaka ya hivi karibuni, ripoti inaonyesha kuanzia mwaka 2026 hadi 2030, soko la Uganda linakadiriwa kuongeza mauzo ya Dola za Marekani milioni 135, huku soko la Kenya kuongeza Dola za Marekani milioni 82.
Hii inamaanisha fursa kwa wakulima wa Tanzania hususan wanaolima mazao ya mahindi, mchele, dengu na maharage ya soya, kuongeza uzalishaji na thamani ya mazao zaidi ili kupanua wigo wa kujipatia kipato kutoka katika soko hilo.