Mlipuko wa Ebola 2026: Visa vyafikia 2,073, vifo 796 ndani ya miezi miwili DRC.
- Mlipuko huo unakuwa wa tatu kwa ukubwa na wenye kasi kuliko mlipuko wowote katika historia ya Ebola.
- Mkoa wa Ituri unendelea kuwa kitovu cha maambukizi, mapigano yakiathiri juhudi za kuudhibiti.
Dar es Salaam. Shirika la Afya Duniani (WHO) limesema mlipuko wa Ebola katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) umefikia visa 2,073 na kusababisha vifo 796 ndani ya miezi miwili tangu Serikali itangaze rasmi mlipuko huo.
Mkurugenzi Mtendaji wa WHO, Dk Tedros Adhanom Ghebreyesus aliyekuwa akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari jana Julai 16, 2026, amesema kasi ya maambukizi imeufanya mlipuko huo kuwa wa tatu kwa ukubwa kuwahi kurekodiwa, ukienea kwa kasi zaidi kuliko mlipuko mwingine.
“Takribani theluthi mbili ya vifo vinatokea katika jamii, ambapo wagonjwa hawafiki katika vituo vya afya kupata matibabu,” amesema Dk Ghebreyesus

Ni zaidi ya miaka 18 sasa nchi ya DRC inapambana na ugonjwa wa Ebola bila mafanikio huku ukiendelea kugharimu maisha ya maelfu ya watu.
Kwa mara kwanza ugonjwa huo uliingia nchini humo mwaka 1976 na kuathiri wagonjwa 318, huku wengine 280 wakipoteza maisha suala liloacha simanzi nchini humo hususan katika eneo la Yambuku.
Tangu wakati huo Ebola imekuwa ikiingia na kutoka DRC kama vile mtu aliyesahau kitu cha thamani kwenye mipaka ya nchi hiyo inayosifika kwa uchimbaji wa madini.
Hata hivyo, Wakongo hawatausahau mwaka 2018 hadi 2020 baada ya kupambana na ugonjwa huo kwa machozi na damu kulikopelekea kurekodiwa kwa kesi mpya 3,470 na vifo 2,287.
Huenda mwaka huu hiyo ikajirudia baada ya jitihada mbalimbali za kuudhibiti ugonjwa huo zinazofanywa na WHO kuendelea kugonga mwamba kwa miezi mitatu tangu kuripotiwa kwake Mei 15, 2026.

Kwa mujibu wa WHO, mlipuko wa Ebola wa mwaka 2018 hadi 2019 nchini DRC ulichukua zaidi ya miezi 10 kufikia visa 2,000 vilivyothibitishwa, tofauti na mlipuko wa sasa ambao umefikia kiwango hicho ndani ya miezi miwili pekee.
WHO imesema zaidi ya asilimia 80 ya visa vipya vinagunduliwa nje ya orodha za watu waliokuwa wamekutana na wagonjwa, hali inayoonyesha kuwa bado kuna minyororo ya maambukizi ambayo haijafuatiliwa.
Mapambano yakoje?
Mkoa wa Ituri Kaskazini Mashariki mwa DRC umeendelea kuwa kiini kikuu cha maambukizi ya virusi hivyo, huku WHO kushirikiana na Kituo cha Kudhibiti na Kudhuia Magonjwa Afrika (Africa CDC) na wadau wengine, ikiendelea kuimarisha hatua za kudhibiti ugonjwa huo.
Takwimu zinaonyesha uwezo wa matibabu umeongezeka hadi vitanda zaidi ya 800, idadi ya maabara ikiongezeka kutoka maabara moja hadi 16, huku kiwango cha ufuatiliaji wa waliokutana na wagonjwa kikifika asilimia 80.
Zaidi ya wahudumu wa afya 21,000 wanaendelea kupatiwa mafunzo, huku shughuli za mazishi salama na yenye heshima zikiboreshwa kwa kiwango kikubwa.

Katika juhudi za kutafuta tiba na kinga, WHO imesema majaribio ya kitabibu na utoaji wa chanjo na dawa unaendelea chini ya uongozi wa Chuo Kikuu cha Oxford na Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Tiba ya DRC
WHO imeeleza kuwa, licha ya kutokuwepo kwa chanjo au tiba zilizoidhinishwa rasmi, watu 377 wamepona, jambo linaloonyesha kuwa utambuzi wa mapema na huduma salama vinaweza kuokoa maisha.
Licha ya juhudi zinazoendelea WHO imesema juhudi za kudhibiti Ebola nchini DRC zinaendelea kukabiliwa na changamoto za kiusalama, kiufundi na upungufu wa zaidi ya Dola za Marekani milioni 400 za kufadhili mwitikio wa dharura.
“Hii si misaada, ni uwekezaji katika usalama wa afya wa mataifa, tunataka kuimarisha uwezo wa kukabiliana na mlipuko katika mikoa mipya iliyoathirika kabla maambukizi hayajasambaa zaidi.” amesema Dk Tedros.