Mambo ya kuzingatia kabla ya kuanzisha biashara

July 10, 2026 12:46 pm · Kelvin Makwinya
Share
Tweet
Copy Link
  • Ni pamoja na kufanya utafiti, kuwa na nidhamu kuweka mipaka na kukubali kujifunza.

Dar es Salaam. Wakati ukosefu wa ajira ukiendelea kuwa changamoto kubwa kwa vijana wengi nchini, biashara imeendelea kuonekana kama njia mbadala ya kujipatia kipato na kujenga uhuru wa kifedha. 

Kila siku, mamia ya vijana huingia kwenye biashara ndogo na za kati wakiamini ndizo zitakazowasaidia kujikwamua kiuchumi na kutoka kwenye ugumu wa maisha.

Nyuma ya hamasa hiyo, kuna upande mwingine wa simulizi. Idadi kubwa ya biashara mpya hushindwa kuendelea kwa muda mrefu, nyingine zikifungwa ndani ya miezi michache tangu kuanzishwa. 

Wataalamu wa uchumi na biashara wanasema changamoto hiyo haisababishwi na ukosefu wa mtaji pekee, bali pia na tabia ya kuanzisha biashara bila maandalizi ya kutosha, kufanya utafiti wa soko na kuandaa mpango wa wazi wa namna ya kuiendesha biashara.

Mtaalamu wa fedha na uchumi kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Abel Kinyondo, anasema kwa vijana wengi, huanzisha biashara hutokana na kuona mtu mwingine amefanikiwa au kusikia kuwa biashara fulani inalipa. 

Hata hivyo, mafanikio ya biashara hayaamuliwi na ukubwa wa faida inayosikika mitaani, bali uwezo wa mjasiriamali kuelewa soko analolenga, mahitaji ya wateja wake na namna bora ya kuendesha biashara hiyo kwa nidhamu na ufanisi. 

Fanya tafiti 

Akizungumza na Nukta Habari Profesa Kinyondo anansema kosa kubwa linalofanywa na vijana wengi wanaotaka kuingia kwenye biashara ni kukurupuka na kuiga wanachofanya wengine bila kuchunguza kama mazingira yao, mtaji, soko na uwezo wa kusimamia biashara hiyo vinaendana na uhalisia.

Akizungumza na Nukta Habari, Profesa Kinyondo amesema si sahihi kwa mtu kuamua kuwekeza kwenye biashara kwa sababu tu amemuona mwingine akifanikiwa, bila kufanya tathmini ya kina ya biashara husika na nafasi yake ya kuweza kuimudu.

“Kabla ya kuingia huko inabidi ufanye utafiti mkubwa sana kuhakikisha hiki kitu kweli kinalipa,” amesema Profesa Kinyondo.

Kwa mujibu wa mtaalam huyo, utafiti unahusisha kufahamu kama bidhaa au huduma unayotaka kuuza inahitajika, nani ni wateja wako, ushindani ukoje, eneo unalolenga lina uwezo wa kuibeba biashara hiyo na mtaji uliopo unaweza kuhimili gharama za kuanzisha na kuendesha shughuli hiyo kwa kipindi fulani.

Kuwa na nidhamu, weka mipaka

Hata biashara inayoonekana kuwa na faida inaweza kushindwa mapema iwapo muanzilishi wake atakosa nidhamu ya matumizi, usimamizi mzuri wa fedha na misingi sahihi ya uendeshaji. 

Kwa mujibu wa Prof Kinyondo, biashara haiwezi kukua kwa kutegemea mazoea, bali kwa maamuzi ya kimkakati yanayotokana na taarifa sahihi na ufuatiliaji wa karibu wa mapato na matumizi.

Mbali na kuwa na nidhamu, mchumi huyo anasisitiza umuhimu wa kuweka mipaka ndani ya biashara. 

Anasema wafanyabiashara wengi, hasa wanaoanza, hujikuta wakichanganya biashara na mahusiano ya kifamilia au urafiki, jambo linaloweza kudhoofisha mapato na kuathiri mtaji bila mhusika kutambua mapema.

Ameeleza kuwa ni kawaida kwa baadhi ya wafanyabiashara kutoa bidhaa au huduma bure kwa ndugu, marafiki au watu wa karibu kwa sababu ya ukaribu wa kijamii, lakini tabia hiyo huondoa nidhamu ya biashara na kuifanya ishindwe kusimama kama taasisi inayopaswa kuingiza mapato.

“Ukimpa mmoja bure utaona aibu kumnyima mwingine,” amesema Profesa Kinyondo.

Kuwa tayari kujifunza

Profesa Kinyondo pia amezungumzia umuhimu wa familia katika kujenga kizazi chenye uelewa wa biashara akiwataka wazazi kuwashirikisha watoto wao katika biashara au miradi wanayoendesha ili kuwajengea uzoefu wa mapema na kuwafundisha namna shughuli za kiuchumi zinavyoendeshwa.

Ushirikishwaji huo unaweza kuwasaidia watoto kujifunza mambo ya msingi kama matumizi sahihi ya fedha, nidhamu ya kazi, namna ya kuhudumia wateja, kusimamia changamoto na kutambua thamani ya kujitegemea. 

Kwa mtazamo wake, uzoefu huo unaweza kuwa mtaji muhimu kwa watoto watakapokuja kuanzisha shughuli zao binafsi hapo baadaye.

Hata hivyo, amesisitiza kuwa kuwashirikisha watoto kwenye biashara za familia haimaanishi kuwa lazima waendelee na biashara hizo hizo wanapokua. Badala yake, ni njia ya kuwajengea msingi wa uelewa wa biashara na kuwapa nafasi ya kujifunza, huku wakibaki na uhuru wa kuchagua taaluma, ndoto au biashara wanazotaka kuzifuata maishani.

Aidha, Profesa Kinyondo amesema kukosa kukulia kwenye familia yenye biashara hakupaswi kumfanya mtu aamini kuwa hawezi kufanikiwa katika ujasiriamali. 

Kwa mujibu wake, maarifa ya biashara yanaweza kujengwa kupitia kujifunza, kujituma, kutafuta ushauri sahihi na kuwa tayari kujifunza.

Amesisitiza kuwa msingi wa mafanikio si mtu ametokea wapi, bali utayari wake wa kujifunza, kuelewa mazingira ya biashara anayotaka kuingia na kujenga uwezo wa kusimamia fursa zinazomzunguka.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Masoko & Zaidi
Loading…
No recent matches
No upcoming matches
/
No matches found for this filter
10 Jul, 2026 · TZS
No forex gainers today
No forex losers today
Forex rates unavailable
10 Jul, 2026 · TZS
No gainers today
No losers today
10 Jul, 2026
No active movers today

Inaendeshwa na Nukta AI

Follow us on TikTok

Nukta Habari

FOLLOW NOW
Subscribe to our channel

Nukta TV

SUBSCRIBE NOW
130 wakamatwa kwa tuhuma za kupanga na kuhamasisha uhalifu Tanzania

130 wakamatwa kwa tuhuma za kupanga na kuhamasisha uhalifu Tanzania

Nukta TV

Mfumuko wa bei Tanzania wapungua kwa 0.2%

Mfumuko wa bei Tanzania wapungua kwa 0.2%

Nukta TV

Rais Samia awaonya wanaharakati wenye matendo ya kigaidi

Rais Samia awaonya wanaharakati wenye matendo ya kigaidi

Nukta TV