Marekani, Tanzania zasaini makubaliano afya ya $3.1 bilioni

July 2, 2026 4:19 pm · Nuzulack Dausen
Share
Tweet
Copy Link
  • Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan imekataa kipengele cha kubadilisha sampuli za magonjwa ikieleza kuwa itajenga uwezo huo ndani ya nchi. 
  • Tanzania inatarajia kupokea msaada wa zaidi ya Sh3.4 trilioni ndani ya miaka mitano.

Dar es Salaam. Tanzania imeingia makubaliano ya kuboresha sekta ya afya na Marekani yenye thamani ya Dola za Marekani bilioni 3.1 sawa na zaidi ya Sh8 trilioni huku Serikali ikikataa pendekezo la kubadilisha sampuli za wagonjwa baina ya nchi hizo mbili. 

Mkataba wa Makubaliano (MoU) uliosainiwa siku ya Jumatano unalenga kuokoa maisha, kuendeleza malengo ya pamoja ya afya duniani, na kuimarisha uwezo wa Tanzania wa kujitegemea katika kukabiliana na magonjwa ya kuambukiza na tishio jipya la kiafya.

Katika makubaliano hayo ya miaka mitano, Serikali ya Tanzania imesema itawekeza zaidi ya Dola za Marekani bilioni 1.8 zaidi ya Sh4.7 trilioni katika kuboresha mifumo ya huduma za afya katika kipindi hicho. 

“Serikali ya Marekani, ikishirikiana na Bunge la Congress, inakusudia kutoa zaidi ya Dola za Marekani bilioni 1.3  (Sh3.4 trilioni) katika kipindi chote cha miaka mitano ya MOU hiyo ili kuendeleza malengo ya pamoja ya afya duniani,” imesema taarifa ya Ubalozi wa Marekani nchini Tanzania. 

Makubaliano hayo yatakuwa chini ya Mkakati wa Afya wa Ulimwengu wa ‘Marekani Kwanza’ (America First Global Health Strategy) wa Serikali ya Rais wa Marekani Donald Trump ambao umekuwa ukikosolewa vikali kwa kuwa na masharti magumu yakiwemo ya kutaka mataifa shirika kutoa taarifa nyeti za masuala ya afya. 

Waziri wa Afya wa Tanzania, Mohamed Mchengerwa alisema, wakati wa hafla ya utiaji saini huo, kuwa Serikali haikusaini makubaliano ya kushirikiana sampuli (specimen sharing agreement), na kueleza kuwa suala hilo litashughulikiwa ndani ya nchi kwa viwango vya kimataifa.

Tanzania yagomea ushirikiano wa sampuli

“Katika mchakato wa mazungumzo haya, tulijadili mambo mengi na washirika wetu na katika suala moja, Tanzania ilifanya uamuzi wa wazi, hatukuingia kwenye makubaliano ya kushirikiana sampuli…tulifanya uamuzi huo si kwa sababu ya kutokuaminiana, bali kwa sababu ya kujiamini kwamba Tanzania itajenga uwezo wake wa ndani wa maabara,” amesema Mchengerwa wakati wa hafla hiyo Julai mosi jijini Dar es Salaam. 

“Sampuli za Tanzania zikiwemo zile za milipuko, magonjwa ya mlipuko na yale yenye uwezo wa kuwa janga kubwa (pandemics) zitapimwa, kuhifadhiwa na kusimamiwa hapa hapa katika ardhi ya Tanzania kwa viwango vya juu zaidi vya kimataifa vya usalama wa kibiolojia na ulinzi wa kibiolojia (biosafe and biosecurity).”

Mchengerwa anasema katika majadiliano yaliyosaidia kufikia makubaliano hayo, wataalamu waliweka mbele uzalendo, usalama na maslahi ya Taifa mbele ili kuhakikisha kuwa utekelezaji wake unaleta maendeleo na si vinginevyo. 

Tumezingatia usalama, maslahi ya Taifa

“Haya tuliyokubaliana ndiyo mtazamo wa nchi yetu, huu ndiyo mtazamo wa kizalendo kwa ajili ya taifa letu,” amesema Mchengerwa. 

Tanzania imeungana na nchi nyingine za Afrika zikiwemo Madagascar, Kenya, Sierra Leone, Botswana, na Ethiopia kusaini makubaliano ya nchi mbili ya afya duniani na Marekani. Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani imesema katika taarifa yake kuwa hadi Julai mosi, 2026, nchi 34 zilikuwa zimeshasaini makubaliano yenye thamani ya zaidi ya Dola za Marekani bilioni 24 au sawa na zaidi ya Sh62.4 trilioni.

Uwekezaji huo ni mwendelezo wa jitihada za kukabiliana na maradhi ya Ukimwi, malaria, kifua kikuu na magonjwa mengine ya kuambukiza. 

“Uwekezaji huu wa pamoja unaonyesha dhamira ya nchi zote mbili katika kuzuia kuenea kwa magonjwa ya kuambukiza, na kuimarisha uwezo wa Tanzania wa kugharamia, kusimamia, na kujiendesha yenyewe katika kutoa huduma muhimu za afya,” imesema taarifa hiyo ya Ubalozi wa Marekani nchini. 

 erikali ya Rais Samia Suluhu Hassan inakabiliwa na shinikizo la kifedha katika kugharamia miradi mikubwa ya miundombinu na huduma za kijamii ikiwemo afya, kutokana na kupungua kwa misaada ya kigeni huku Marekani na nchi za Ulaya zikibadilisha sera zao.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Masoko & Zaidi
Loading…
No recent matches
No upcoming matches
/
No matches found for this filter
No forex gainers today
No forex losers today
Forex rates unavailable
2 Jul, 2026 · TZS
No gainers today
No losers today
2 Jul, 2026
No active movers today

Inaendeshwa na Nukta AI

Follow us on TikTok

Nukta Habari

FOLLOW NOW
Subscribe to our channel

Nukta TV

SUBSCRIBE NOW
Msikie Jaji Mkuu Masaju : Mambo wasiopaswa kufanya madalali wa Mahakama.

Msikie Jaji Mkuu Masaju : Mambo wasiopaswa kufanya madalali wa Mahakama.

Nukta TV

Dk Mwigulu: Kama siyo Rais Magufuli mradi wa Bwawa la Mwalimu Nyerere usingefanyika

Dk Mwigulu: Kama siyo Rais Magufuli mradi wa Bwawa la Mwalimu Nyerere usingefanyika

Nukta TV

Umuhimu wa elimu ya mikopo

Umuhimu wa elimu ya mikopo

Nukta TV