Deni la Serikali lapaa kwa asilimia 8.7, lafikia Sh114.34 trilioni
- Kati ya kiasi hicho, deni la ndani lilikuwa Sh38.44 trilioni na deni la nje lilikuwa Sh75.89 trilioni
Dar es Salaam. Deni la Serikali ya Tanzania limeongezeka kwa asilimia 8.97 hadi kufikia Sh114.34 trilioni ndani ya mwaka mmoja ikichangiwa na utekelezaji wa miradi mikubwa ya maendeleo.
Waziri wa Fedha, Balozi Khamis Omar aliyekuwa akiwasilisha bajeti kuu ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2026/27 bungeni jijini Dodoma leo Juni 11, 2026 amesema kati ya fedha hizo zilizokopwa deni la ndani lilikuwa Sh38.45 trilioni sawa na asilimia 33.6 huku deni la nje likifikia Sh75.89 trilioni sawa na asilimia 66.4.
Kwa mujibu wa kiongozi huyo, fedha hizo zilizoongezeka kutoka Sh104.93 trilioni iliyotumika kipindi kama hicho mwaka 2025 zilielekezwa katika miradi ya kimkakati.
“Deni hilo limetokana na mikopo iliyoelekezwa katika maeneo ya kimkakati yanayochochea ukuaji wa uchumi, ikiwemo ujenzi wa miundombinu ya usafirishaji, nishati na mawasiliano,” ameeleza Balozi Omar.
Pamoja na mikopo hiyo kuendelea kusaidia utekelezaji wa baadhi ya miradi ya mikakati ikiwemo ujenzi wa reli ya kisasa (SGR) na bwawa la Julius Nyerere baadhi ya vyama vya siasa vya upinzani na wadau wa maendeleo wamekuwa wakipinga mwenendo wa ukopaji huo.

Miongoni mwao ni Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) iliyopinga utaratibu na kasi ya kuchukua mikopo, hususan ile inayopelekea kukua kwa kasi kwa deni la Taifa.
Rais Samia Suluhu Hassan aliwahi kutolea ufafanuzi kuhusu kupaa kwa deni hilo, akibainisha kuwa limetokana na sababu mbalimbali ikiwemo kushuka kwa Shilingi ya Tanzania.
“Ni vyema wananchi wakaelewa kuwa baadhi ya mikopo tuliyopokea sasa ilisainiwa miaka ya nyuma. Pia, mabadiliko ya thamani ya fedha yamechangia kuonekana kuwa deni limeongezeka kwa takribani trilioni 3.9,” alisema Rais Samia,” alisema Rais Samia Juni 27, 2025.
Deni bado ni himilivu
Licha ya deni hilo kupaa, Balozi Omar tathmini iliyofanywa Novemba 2025 imeonesha kuwa deni hilo ni himilivu katika kipindi cha muda wa kati na mrefu.
“Deni la nje kwa Pato la Taifa ni asilimia 24.4 dhidi ya ukomo wa asilimia 40 na deni la nje kwa mauzo ya nje ni asilimia 123.1 dhidi ya ukomo wa asilimia 180. Hii inaonesha kuwa nchi yetu ina uwezo mzuri wa kusimamia na kuhimili deni lake bila kuathiri uthabiti wa misingi ya uchumi,”amesema Balozi Omar
Hata hivyo, huenda deni hilo likaongezeka zaidi baada ya Serikali kutarajia kukopa jumla ya Sh15.54 trilioni katika mwaka wa fedha 2026/27.
Kati ya kiasi hicho, mikopo ya ndani ni Sh6.56 trilioni, mikopo ya nje yenye masharti nafuu Sh6.55 trilioni na mikopo ya nje yenye masharti ya kibiashara Sh2.43 trilioni