Vipaumbele vitano bajeti ya Serikali mwaka 2026/27
- Ni pamoja na kuimarisha utawala bora, demokrasia, amani, na utulivu.
- Pia kujenga uchumi imara, jumuishi na shindani.
Dodoma. Serikali imesema Bajeti ya Mwaka wa Fedha 2026/27 itajikita katika maeneo matano ya vipaumbele ikiwemo kujenga uchumi imara, jumuishi na shindani ikiwa ni mwanzo wa safari ya utekelezaji wa Dira 2050 inayolenga kuwa na uchumi wa Dola za Marekani trilioni moja.
Katika hotuba yake ya hali ya uchumi wa Taifa, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji Prof Kitila Mkumbo ameliambia Bunge jijini Dodoma kuwa vipaumbele hivyo vitasaidia kuharakisha maendeleo ya kiuchumi na kijamii.
Vipaumbele hivyo vilivyopo kwenye Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2026/27 ni uimarishaji wa uwezo wa watu na maendeleo ya jamii na uimarishaji uhifadhi wa mazingira na ustahimilivu kwa mabadiliko ya tabianchi.
“Kusimamia utekelezaji wa vichocheo vya mageuzi ikiwemo nishati, miundombinu ya usafiri na usafirishaji, utafiti na maendeleo, na mageuzi ya kidigitali,’’ ameongeza Prof Mkumbo wakati akibainisha vipaumbele.
Utekelezaji wa vipaumbele hivyo ni sehemu ya kukamilisha utekelezaji wa Mpango wa nne wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano (2026/27 – 2030/31)
Kipaumbele kingine katika bajeti hiyo ya kwanza kwa Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan tangu aanze awamu ya pili na ya mwisho ni kuimarisha utawala bora, demokrasia, amani, na utulivu.
Katika hotuba yake kuhusu hali ya uchumi wa taifa na mpango wa maendeleo wa Taifa wa mwaka 2026/27 leo Juni 11, 2026 bungeni jijini Dodoma Prof Mkumbo amesema Serikali itashirikiana na sekta binafsi kuweka mkazo kwenye miradi ya kimkakati yenye manufaa na matokeo makubwa.
Miradi ya kimkakati
Miongoni mwa miradi hiyo inayopangwa kutekelezwa ni pamoja na maendeleo ya mji wa ikolojia ya bahari Bagamoyo na mfumo wa usafirishaji fungamanishi na mradi wa kitovu changamani cha makaa ya mawe Mchuchuma na Chuma Liganga.
Vilevile, programu ya kitaifa ya umwagiliaji na mageuzi ya viwanda vya uchakataji wa mazao ya kilimo, kitovu cha teknolojia na uchakataji wa madini adimu Dodoma, pamoja na mradi wa kiwanda cha kuchakata gesi asilia ya kimiminika (LNG) mkoani Lindi.
Miradi mingine ni pamoja na kitovu cha kisasa cha viwanda na uchumi wa buluu katika ukanda wa maziwa makuu na programu shirikishi ya uendelezaji wa miji nchini.
“Gharama za utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo wa mwaka 2026/27 zinakadiriwa kufikia Sh86.3 trilioni, sawa na asilimia 18.1 ya gharama za utekelezaji wa Mpango wa Nne wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano, unaotarajiwa kugharimu jumla ya Sh477.7 trilioni,” ameeleza Prof. Mkumbo.
Katika mgawanyo wa uwekezaji huo, sekta binafsi inatarajiwa kuchangia Sh60.1 trilioni, sawa na asilimia 69.6 ya gharama zote huku sekta ya umma ikichangia Sh26.2 trilioni, sawa na asilimia 30.4.
Kati ya fedha hizo mashirika ya umma yatachangia Sh5.5 trilioni na Serikali itachangia Sh20.8 trilioni kupitia Bajeti ya Serikali itakayowasilishwa baadaye leo na Waziri wa Fedha.