NMB kugawanya hisa 1 kuwa 10 kuchochea uwekezaji sokoni
- Hii ina maanisha kuwa hisa moja ya NMB ya sasa itakuwa ni sawa na hisa 10 huku bei ya hisa moja ikipungua kwa uwiano huo huo.
Dar es Salaam. Wanahisa wa benki ya NMB wamepitisha azimio la kugawanya hisa za benki hiyo kwa uwiano wa 1 kwa 10 hatua inayotarajiwa kuongeza idadi na kupunguza bei ya hisa za benki hiyo sokoni.
Uamuzi huo wa NMB umelenga kuweka uwiano wa bei ya hisa kati ya kampuni nyingine na NMB ambayo kwa sasa ina hisa ghali zaidi.
Mgawanyo wa hisa (stock split) ni kitendo cha kampuni kugawanya hisa zake zilizopo kuwa hisa nyingi zaidi kwa uwiano fulani bila kubadilisha thamani ya jumla ya uwekezaji wa mwanahisa.
“Kwa kuigawanya hisa ya NMB tunaiweka karibu na hisa ya nyingine…hata kama kwa mfano sasa mtu na Sh7,000 ataweza kununua hisa tano, hiyo ni moja ya faida ya wazi,” Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa NMB, David Nchimbi ameeleza katika Mkutano Mkuu wa Wanahisa wa NMB.
Hii inamaanisha kuwa, ikiwa NMB itafanikiwa kupata ridhaa ya kugawanya hisa zake kwa uwiano wa 1:10 kutoka kwa mamlaka zinazosimamia taasisi za fedha, kila hisa moja ya NMB itazidishwa mara kumi.

Kwa mfano, mwanahisa ambaye anahisa 10 za NMB, kwa uwiano huo atakuwa na hisa 100.
Hata hivyo, ongezeko hilo la hisa linakwenda sambamba na kupungua kwa bei ya hisa kwa uwiano sawa na huo kutegemea na bei ya hisa iliyopo wakati ambao mabadiliko yanafanyika.
Maana yake ni kwamba kama mabadiliko hapo yangefanyika leo ambapo hisa moja ya NMB inauzwa Sh14,930 basi mwekezaji angekuwa na hisa 10 zenye thamani ya Sh1,493 kwa kila hisa.
Kwa mujibu wa Afisa Mtendaji Mkuu wa NMB, Ruth Zaipuna hatua hiyo itaongeza idadi ya hisa za NMB zilizopo sokoni na kufanya watu wengi waweze kuwekeza bila wanahisa wakongwe kupoteza thamani ya uwekezaji wao.
“Ile siku tutakayofanya mgawanyo tutaangalia bei iliyopo sokoni, kama bei itakayokuwa sokoni siku hiyo ni Sh15,000 kama ambayo ilivyo leo, ina maana siku hiyo bei ya hisa moja ya NMB, badala ya kuwa Sh15,000 itakuwa Sh1,500,” ameelekeza Zaipuna.
Maoni mseto kwa wahahisa
Hata hivyo, wakati wanahisa wakipitisha azimio hilo kwa kishindo baadhi ya wanahisa wamekuwa na maoni mseto kuhusiana na mgawanyo huo.
Wakati wawekezaji wengi wakipiga shangwe kwa kuona fursa ya kuongeza uwekezaji kwa kununua hisa nyingi zaidi kuliko hivi sasa kutokana na bei ya hisa kuwashinda, mambo ni tofauti kwa Victoria Mandari.
Mandari ambaye ameanza kuwekeza NMB tangu benki hiyo mashuhuri ya kibiashara kuorodheshwa kwenye Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE) amekuwa na maoni tofauti akieleza hofu yake ya kupoteza thamani ya hisa zake ambazo amewekeza kwa muda mrefu.

Mandari ameieleza Nukta Habari kuwa ingawa hatua hiyo itaongeza idadi ya ya wanahisa kwa kufanya bei yake kuwa nafuu, bado anahofu kwamba huenda hisa za wawekezaji wa zamani kama yeye zisiwe na thamani ile ile.
“Na ninaona kama watu watakuwa na mawazo kama mimi, wataweza kukimbia sasa hivi kuuza hisa zao zikiwa na thamani kubwa kabla haijapungua,” amesema Mandari.
Hata hivyo, kwa mujibu wa Nchimbi, mgawanyo huo hauathiri kwa namna yeyote thamani ya hisa kwa sababu kupungua kwa bei ya hisa kunaendana na kuongezeka kwa idadi ya hisa hivyo kufanya thamani kuwa sawa.
Kwa sasa benki ya NMB ndiyo kampuni yenye hisa ghali zaidi kwenye soko la DSE ikiwa ni mara 5 zaidi ya mshindani wake wa karibu Benki ya biashara ya CRDB.
Huenda kufanya mgawanyo huo wa hisa kukachochea ongezeko la ushiriki wa wawekezaji sokoni na kuongeza mzunguko wa biashara ya hisa za NMB katika soko ambayo kwa wengi imeonekana kuwa ghali.