Fahamu madhara ya kutumia dawa hovyo wakati wa ujauzito

June 8, 2026 5:18 pm · Fatuma Hussein
Share
Tweet
Copy Link
  • Matumizi ya dawa kihorera yanaweza kusababisha ulemavu wa kudumu au kuharibika kwa mimba.

Dar es Salaam. Ujauzito ni safari ya kipekee ya mwanamke inayobeba matumaini makubwa ya kuleta maisha mapya duniani.

Katika kipindi hiki, afya ya mama na mtoto anayekua tumboni huunganishwa kwa karibu kiasi kwamba kila jambo analofanya mama linaweza kuwa na athari kwa mtoto wake.

Miongoni mwa mambo yanayohitaji umakini mkubwa ni matumizi ya dawa. Ingawa dawa husaidia kutibu na kudhibiti magonjwa mbalimbali, matumizi holela ya dawa wakati wa ujauzito yanaweza kuhatarisha maisha ya mama na mtoto. 

Kwa mujibu wa tovuti ya Kituo cha Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa (CDC), wanawake tisa kati 10 hutumia aina fulani ya dawa wakati wa ujauzito huku wanawake saba kati ya 10 wakitumia angalau dawa moja ya hospitali iliyoandikwa na daktari. 

Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Wanawake na Uzazi, Dk Benny Kimaro kutoka Dar es Salaam, anasema mama mjamzito anaweza kupatwa magonjwa kutokanana kinga zake kushuka hivyo kulazimika kutumia dawa.

“Mama mjamzito kitaalam huwa kinga zake za mwili zinashuka kwa hiyo utaweza kuona kwamba ni rahisi naye kupatwa na magonjwa, kwa muda wote ule anaweza akaumwa na ugonjwa mwingine kwa sababu kuwa mjamzito haina sababu kwamba mama hawezi kuumwa tena,” anasema Dk Kimaro.

Hali hii humfanya mama kuwa katika hatari ya kupata baadhi ya magonjwa kama ilivyo kwa watu wengine.

Hata hivyo, kushuka huko kwa kinga mwili hakupaswi kuwa sababu ya matumizi hohela dawa hususani katika kipindi cha miezi mitatu ya mwanzo wa ujauzito kwasababu  ndani ya kipindi hicho ndipo viungo vya mwili wa mtoto vinaanza kutengenezwa.

Dawa aina yoyote inaweza kutumiwa na mama mjamzito . Picha|Fatuma Hussein

Katika kipindi hiki, matumizi holela ya dawa yanaweza kusababisha madhara makubwa kwa mtoto aliyeko tumboni ikiwemo kuathiri ukuaji wa ubongo, mikono, miguu, masikio au viungo vingine muhimu.

Madhara haya yanaweza kusababisha mtoto kuzaliwa na ulemavu wa viungo au matatizo mengine ya maendeleo ya mwili au kusababisha mimba kutoka au kupotea.

Dawa huathiri vipi ujauzito?

Athari za dawa kwa mama na mtoto hutegemea mambo mbalimbali, ikiwa ni pamoja na umri wa ujauzito wakati dawa inapotumika, aina, nguvu na dozi ya dawa, uwezo wa dawa kuvuka kondo la nyuma (placenta), hali ya afya ya mama na mwitikio wa mwili wa mama kwa dawa husika.

Kulingana na tovuti ya Mayoclinic miongoni mwa athari za matumizi hayo ya dawa ni pamoja baadhi ya dawa kukosa matokeo kwa mama wala mtoto wakati wa ujauzito, kusababisha ulemavu wa kuzaliwa, matatizo ya ukuaji au hata kifo cha mtoto akiwa tumboni.

Vilevile, baadhi ya dawa huathiri afya ya mama kwa namna inayopunguza mtiririko wa damu kwenda kwa mtoto, jambo linaloweza kudhoofisha ukuaji wake, kuathiri kazi ya kondo la nyuma kusambaza oksijeni na virutubisho kwa mtoto hali inayoweza kusababisha mtoto kuzaliwa akiwa na uzito mdogo au ukuaji hafifu.

Pia, baadhi ya dawa huongeza mikazo ya misuli ya uterasi na hivyo kuongeza hatari ya kujifungua kabla ya wakati au kuathiri afya ya mtoto.

Dk Kimaro anasisitiza kuwa ni muhimu kwa mama mjamzito kushauriana na daktari, mfamasia au mtoa huduma wa afya kabla ya kuanza, kuacha au kubadilisha matumizi ya dawa yoyote wakati wa ujauzito.

Kuepuka matumizi holela ya dawa ni njia muhimu ya kupunguza hatari ya ulemavu wa kuzaliwa, matatizo ya ukuaji wa mtoto, kupoteza ujauzito na madhara mengine yanayoweza kudumu maisha yote.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Inaendeshwa na Nukta AI

Follow us on TikTok

Nukta Habari

FOLLOW NOW
Subscribe to our channel

Nukta TV

SUBSCRIBE NOW
Kwanini uchafuzi wa mazingira ni tishio kwa afya ya binadamu na uchumi

Kwanini uchafuzi wa mazingira ni tishio kwa afya ya binadamu na uchumi

Nukta TV

Tunachokifahamu kuhusu ziara ya Rais Samia Urusi, kidiplomasia na uchumi

Tunachokifahamu kuhusu ziara ya Rais Samia Urusi, kidiplomasia na uchumi

Nukta TV

Kutoka Ubunge hadi mshauri wa Rais, Panda shuka ya Ummy Mwalimu katika siasa

Kutoka Ubunge hadi mshauri wa Rais, Panda shuka ya Ummy Mwalimu katika siasa

Nukta TV