Mama mzazi wa Hayati Magufuli afariki dunia, Rais Samia amlilia
- Amefariki dunia leo Mei 25, 2026 nyumbani kwake Chato, mkoani Geita baada ya kuugua muda mrefu.
]Arusha. Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amesema amepokea kwa masikitiko makubwa taarifa ya kifo cha Mama mzazi wa aliyekuwa Rais wa awamu ya tano, Dk John Pombe Magufuli aliyefariki dunia leo Mei 25, 2026 nyumbani kwake Chato, mkoani Geita.
Jesca Magufuli, mtoto wa Hayati Magufuli amethibitisha kutokea kwa kifo hicho katika mahojiano yake na AyoTV yaliyofanyika kwa njia ya simu akifafanua kuwa bibi yake amefariki baada ya kuugua muda mrefu.
“Bibi yetu (Suzana Mussa) amefariki saa moja nyumbani kwake Chato baada ya kuugua kwa muda mrefu, taratibu za msiba familia itawajulisha, Bwana ametoa na Bwana ametwaa” amesema Jesca.
Kupitia taarifa ya Bakari Machumu, Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu iliyotolewa usiku leo Maei 25,2026 imeeleza kuwa Rais Samia ametoa pole kwa familia ya Hayati Dk Magufuli, ndugu, jamaa, marafiki na wote walioguswa na msiba huu.
“Kwa niaba ya Serikali, na kwa niaba yangu binafsi, naungana na familia katika kipindi hiki kigumu cha majonzi, tukiwaombea nguvu, faraja na uvumilivu…Halikadhalika, Rais Dkt. Samia anaiombea roho ya marehemu pumziko la milele. Amina,” imeeleza taarifa ya Rais Samia.