Meli za mafuta ya ndani kupewa kipaumbele Tanzania

March 26, 2026 7:38 pm · Nuzulack Dausen
Share
Tweet
Copy Link
  • Hatua hiyo imeenga kuongeza usalama wa mafuta nchini.

Dar es Salaam. Serikali ya Tanzania imesema itatoa kipaumbelea kupakua mafuta kutoka kwenye meli zilizoleta mzigo kwa ajili ya matumizi ya ndani ya nchi ikiwa ni moja ya hatua ya kuhakikisha kuwa kuna mafuta ya petroli ya kutosha kumudu mahitaji ya soko. 

Tanzania ni miongoni mwa nchi duniani zilizoathirika na vita inayoendelea baina ya Israel na Marekani na Iran iliyosababishwa kufungwa kwa mlango wa Hormuz unaosaidia usafirishaji wa asilimia 20 ya mafuta yote yanayotumika duniani. Vita hiyo inayokaribia mwezi sasa imetengeneza uhaba wa mafuta na kupanda kwa bei ya nishati hiyo katika mataifa mengi yakiwemo ya Afrika na kutishia uchumi wa mataifa hayo.

Waziri wa Nishati, Deogratius Ndejembi amesema kuwa kwa sasa wataharakisha ushushaji wa meli za mafuta yanayoenda kutumika nchini ili kuleta usalama wa mafuta licha ya kuendelea kuwepo taharuki miongoni mwa watumiaji. 

Amesema kwa sababu Tanzania ni nchi yenye bandari, inawajibika kuwapatia huduma ya bandari ya upokeaji wa mafuta na mizigo mingine kwa nchi jirani. 

“Kwa hali ilivyo sasa ili kuhakikisha bado tunaendelea kuwa na usalama wa mafuta nchini nimewaelekeza PBPA (Wakala wa Uagizaji Mafuta kwa Pamoja) tunaanza kwanza kushusha mafuta yetu ya hapa ndani ya nchi,” amesema Ndejembi wakati wa mkutano na viongozi wa taasisi zinazohusika na udhibiti na uingizaji wa mafuta nchini. 

Miongoni mwa nchi zinazotegemea Bandari ya Dar es Salaam kuingiza mafuta ni Malawi, Zambia, Burundi, Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Mapema wiki hii Waziri wa Nishati na Madini wa Malawi, Dk Jean Mathanga alifunga safari kukagua miundombinu ya mafuta katika kituo cha Kurasini Oil Jet (KOJ-1) ikiwa ni sehemu ya nchi hiyo kuhakikisha ina mafuta ya kutosha. 

Mbali na kuharakisha upakuaji wa mafuta, waziri huyo amesema wameanza utaratibu wa ugawaji wa mafuta kwa awamu kwa wasambazaji (sequencing) katika ushushaji wa mafuta hayo ili kukamilisha oda sokoni. 

“Hii inamaanisha kwamba kama msambazaji, kwa mfano, alikuwa na oda ya lita 15,000 na mwingine anakumbana na upungufu kwenye depo lake, wapewe lita 5,000…kila mmoja, na mzigo wa yule msambazaji mwingine utakapofika, nao watagawana kwa namna hiyo hiyo hadi oda itimie…utaratibu huu wa ugawaji unaanza leo,” amesema. 

‘Msiwe na taharuki’

Katika kikao hicho, Ndejembi amewataka Watanzania kutokuwa na taharuki juu ya upatikanaji wa mafuta kwa kuwa nchi ina nishati hiyo ya kutosha na kwamba kuna baadhi ya watu wenye hofu ya uhaba wananunua kiwango kikubwa na kuathiri ugavi wa nishati hiyo muhimu kwa uchumi. 

“Unakuta kituo kile kama kilikuwa kimekadiria kuuza lita 20,000 kwa siku kinauza sasa lita 30,000 ambayo inaharibu au inavuruga utaratibu wao wa upatikanaji wa mafuta kutoka depo mpaka pale,” amesema. 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Follow Us on TikTok

Subscribe to Our YouTube Channel

Subscribe

Loading videos...

Loading videos...

Loading videos...

Enable Notifications OK No thanks