Mambo ya kuzingatia wakati, kabla na baada ya ‘Interview’

March 20, 2026 9:00 am · Kelvin Makwinya
Share
Tweet
Copy Link
  • Wataalamu wanasema ni vizuri kujiandaa kabla, wakati na baada ya interview.
  • Wasema unacho’post’ kwenye mitandao yako ya kijamii yaweza kuwa kikwazo kupata ajira.

Dar es Salaam. Katika soko la ajira linalozidi kuwa na ushindani mkubwa, mahojiano ya kazi maarufu kama ‘Interview’ (Usaili) yameendelea kuwa kigezo kikuu cha waajiri kutambua uwezo, nidhamu na mtazamo wa waombaji kazi. 

Usaili ni mahojiano rasmi kati ya mwajiri na muombaji kazi yanayofanyika ili kumpima na kumfahamu vizuri mgombea kabla ya kumpa ajira. 

Katika mahojiano hayo, mwajiri huuliza maswali kuhusu elimu, uzoefu, ujuzi, tabia na mtazamo wa kazi wa muombaji, huku muombaji naye akipewa nafasi ya kujieleza na kuuliza maswali.

Kwa kawaida, usaili wa ajira hufanyika kwa njia kuu mbili, usaili wa kuandika, unaolenga kupima maarifa na uelewa wa mgombea, na mahojiano ya mdomo, yanayolenga kutathmini uwezo wa mawasiliano, kujiamini na namna anavyojieleza mbele ya waajiri.

‘Vijana wanakosa ajira kwa kushindwa interview’

Kwa mujibu wa wataalamu wa Shirika la kazi la Umoja wa Mataifa (ILO), interview ni hatua muhimu inayosaidia waajiri kutathmini kama mtahiniwa  anaendana na mahitaji ya kazi pamoja na utamaduni wa taasisi husika.

Hata hivyo, kwa vijana wengi hasa wale wanaoingia katka ajira kwa mara ya kwanza au wasio na uzoefu mkubwa, ‘interview’ imekuwa kikwazo kinachokatisha tamaa kutokana na kushindwa kufanya maandalizi sahihi yatayowapa nafasi ya kupata ajira wanapokwenda kwenye usaili.

ILO inaeleza kuwa vijana wengi hukosa ajira si kwa sababu hawana uwezo, bali kwa kukosa ujuzi wa kujiwasilisha na kujiamini wakati wa mahojiano. 

Kwa kawaida, usaili wa ajira hufanyika kwa njia kuu mbili, usaili wa kuandika, unaolenga kupima maarifa na uelewa wa mgombea, na mahojiano ya mdomo, yanayolenga kutathmini uwezo wa mawasiliano, kujiamini na namna anavyojieleza mbele ya waajiri. Picha | Zanzibar News.

Ikiwa wewe ni mmoja wa vijana hao, Nukta Habari tumekuandalia makala itakayokusaidia kufanya maandalizi yatakayoweza kubadili matokeo na kushawishi mwajiri kukupa nafasi ya ajira utakapoenda kwenye usaili.

Maandalizi hayo ya  interview yamegawanyika katika hatua kuu tatu ambazo ni kabla ya interview, wakati wa interview na baada ya interview kama anavyoeleza Afisa Vipawa na mtaalamu wa masuala ya uajiri kutoka Niajiri Plattform, Mary Kopwe.

“Watu wengi wanaangalia tu siku ya interview, lakini ukweli ni kwamba mafanikio ya usaili yanaanzia kwenye maandalizi. Ukijiandaa vizuri, unajipa nafasi kubwa ya kufaulu,” anasema Kopwe.

Kabla ya ‘interview’

Mtaalamu huyo anasema kuwa kabla ya kufika kwenye usaili, ni muhimu kwa muombaji kufanya maandalizi ya kina ikiwa ni pamoja na kufanya utafiti kuhusu kampuni au taasisi husika, kuelewa majukumu ya nafasi aliyoomba, pamoja na kujiandaa kujibu maswali ya msingi kama vile kujitambulisha, kueleza uzoefu wake na kubainisha malengo yake ya kazi.

“Jua kampuni inafanya nini, historia yake, wana ‘product’ gani au wanatoa huduma gani…ni vizuri kuijua kampuni, inakufanya kuwa na kujiamini zaidi hata utakapoulizwa maswali,” anasema Kopwe.

Kopwe anaongeza kuwa kufanya mazoezi ya usaili, iwe peke yako au kwa msaada wa watu wengine, humsaidia muombaji kujiandaa vyema kwa aina ya maswali yanayoweza kuulizwa na namna bora ya kuyajibu. 

“Unaweza ukasimama hata mbele ya kioo, ukavuta picha kwamba upo mbele ya waajiri wako ukaanza kujijengea kujiamini na maswali ambayo yapo ‘basic’,” anabainisha Kopwe.

ILO inaeleza kuwa vijana wengi hukosa ajira si kwa sababu hawana uwezo, bali kwa kukosa ujuzi wa kujiwasilisha na kujiamini wakati wa mahojiano. Picha | Utumishi.

Aidha, amesema ili kumvutia mwajiri ni vema kuhakikisha mtahiniwa anaandaa nyaraka zote muhimu na zinazohitajika, akizingatia usafi, usahihi na ziendane na nafasi aliyoomba. Usafi huo unahusisha pia namna zilivyoandikwa, kuhakikisha zinafuata maelekezo yaliyotolewa na zinawasilisha taarifa kwa ufasaha na umakini.

Maandalizi hayo pia yanatakiwa kugusia eneo la mavazi, ambapo yanatakiwa yawe mavazi rasmi na yanayoendana na mazingira ya kazi unayoiomba akisisitiza kuwa mwonekano wa kwanza unaweza kuwa na ushawishi mkubwa katika maamuzi ya mwajiri.

Wakati wa interview

Kopwe anabainisha kuwa wakati wa mahojiano, ni vyema mwombaji wa ajira kuwa mtulivu, kujiamini na kujieleza kwa uwazi. Mawasiliano mazuri ya macho, lugha ya mwili na namna ya kujibu maswali kwa ufupi lakini kwa ufasaha

“Subiri ukaribishwe, kaa vizuri na unapojibu maswali usiropoke, chukua muda wako pangilia jibu lako alafu zungumza…ni vyema unapojibu maswali ukawataja majaji kwa majina yao, inaonyesha kweli ulikuwa makini ” amesisitiza Kopwe.

Amebainisha kuwa ni muhimu kwa muombaji kuuliza maswali wakati wa usaili kwani huonyesha umakini, shauku ya kazi husika na husaidia kupata uelewa mpana kuhusu majukumu, mazingira ya kazi na matarajio ya mwajiri.

“Usiondoke bila kuuliza swali,” amesisitiza Kopwe.

Ni vyema kufuatilia mrejesho kwa njia ya kitaalamu, ikiwa ni pamoja na kutuma barua pepe ya shukrani kwa mwajiri ndani ya saa 24 tangu kufanyika kwa usaili. Picha | Utumishi.

Baada ya ‘interview’

Akizungumzia hatua ya baada ya usaili, Mary Kopwe anasisitiza umuhimu wa muombaji kuendelea kuonesha weledi hata baada ya mahojiano kukamilika. 

Anasema ni vyema kufuatilia mrejesho kwa njia ya kitaalamu, ikiwa ni pamoja na kutuma barua pepe ya shukrani kwa mwajiri ndani ya saa 24 tangu kufanyika kwa usaili.

Kwa mujibu wa Kopwe, hatua hiyo huonyesha heshima, umakini na dhamira ya kweli ya muombaji kuipata nafasi hiyo. “Kutuma ujumbe wa shukrani ni jambo dogo lakini lenye uzito mkubwa, linaweza kukuweka tofauti na waombaji wengine,” anasema.

Ameongeza kuwa muhimu kwa muombaji kufuatilia mrejesho kwa kuuliza kwa heshima ikiwa amefanikiwa kupata nafasi hiyo au lah, pamoja na kufahamu ni lini matokeo rasmi ya usaili yatatangazwa.

“Subiri hata baada ya wiki mbili, ndio uanze kuuliza. Lakini sio kila wakati, utaonekana kero,” amesisitiza Kopwe.

Usikose kufuatilia mfululizo wa makala hizi za ajira ambapo tutaangazia jinsi mitandao ya kijamii inavyoweza kuwa fursa au kikwazo cha kukukosesha ajira.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Follow Us on TikTok

Subscribe to Our YouTube Channel

Subscribe

Loading videos...

Loading videos...

Loading videos...

Enable Notifications OK No thanks