Mapendekezo 284 ya tume ya kodi kuwafuta machozi wafanyabiashara Tanzania
- Mapendekezo hayo ni yale yaliyowasilishwa na Tume ya Rais ya kutathmini maboresho ya Mfumo wa Kodi Tanzania.
Tume yapendekeza kuondoa uwezekano wa mlipa kodi na afisa wa TRA kuonana ana kwa ana.
Arusha/Dar es Salaam. Tume ya Rais ya kutathmini maboresho ya Mfumo wa Kodi Tanzania imetoa mapendekezo 284 katika maeneo saba muhimu yanayotarajiwa kutoa ahueni kwa wafanyabiashara nchini Tanzania.
Tume hiyo iliyowasilisha ripoti yake mbele ya Rais Samia Suluhu Hassan leo Machi 18, 2026 ikiwa ni takribani miezi 20 tangu iundwe Julai, 2024 kufuatia migogoro ya kikodi iliyokuwa ikiibuka mara kwa mara kutoka kwa wafanyabiashara nchini kuanzia mwishoni mwa mwaka 2023.
Mwenyekiti wa Tume hiyo Balozi Ombeni Sefue aliyekuwa akiwasilisha ripoti hiyo amesema mapendekezo hayo yataimarisha mifumo ya kodi nchini yakikidhi mahitaji ya Watanzania.
“Tunaamini kuwa mapendekezo yatakayotolewa leo yatakidhi matarajio yako Mheshimiwa Rais na matarajio ya Watanzania wakiwemo wafanyabiashara, wawekezaji, washirika na wadau wa masuala ya kodi nchini,” amesema Balozi Sefue.
Kati ya mependekezo yaliyowasilishwa 146 yanahusu sera na sheria, mifumo ya Tehama (41), masuala ya kiutawala (30), urasimishaji na upanuzi wa wigo wa kodi (25), mazingira ya uwekezaji na biashara (15), utatuzi wa migogoro ya kodi (14), pamoja na masualla 13 yanayohusu muundo na mfumo wa usimamizi wa kodi.
Miongoni mwa mapendekezo hayo, yapo yanayowagusa moja kwa moja wafanyabiashara wadogo ambayo huenda yakawafuta machozi na kupunguza kero zilizokuwa zikilalamikiwa mara mara ikiwemo kupunguza uwezekano wa afisa kodi na mlipaji kodi kuonana ili kupunguiza urasimu na mianya ya rushwa.
“Tunapendekeza kuondoa utaratibu wa maafisa wa kodi kuonana uso kwa uso na walipa kodi na kupunguza matumizi ya fedha taslimu na makaratasi kwa kadri inavyowezekana masuala yote yafanyike kwa njia ya mitandao…
…Ikiwa upo umuhimu wa kuonana basi yatengwe maeneo mahususi yenye uwazi na ‘CCTV camera’ ili kuweka rekodi ya mazungumzo na kuondoa usiri kati ya walipa kodi na maafisa,” amesisitiza Sefue.

Mwenyekiti wa Tume ya Rais ya Kutathmini Maboresho ya Mfumo wa Kodi nchini Katibu Mkuu Kiongozi Mstaafu Balozi Ombeni Sefue akizungumza kabla ya kukabidhi Ripoti ya Tume hiyo kwa Rais Samia Suluhu. Picha|Ikulu Mawasiliano.
Katika eneo la sera na sheria, tume imependekeza kuundwa kwa mfumo maalum utakaowatambua, kuwalea na kuwakuza wafanyabiashara wadogo ili kukuza uchumi wa mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla.
“Kwa niaba ya wenzangu tunakuomba sana usije ukamaliza muda wako wa uongozi bila kuwaachia Watanzania mfumo timilifu, kamilifu, jumuishi yani ‘360 degree wa ecosystem’ kuwatambua, kuwalea na kuwakuza wajasiriamali wadogo wa Tanzania,” amesema Balozi Sefue.
Masuala mengine ya muhimu yaliyopendekezwa ni kuanzishwa kwa programu tumizi (app) pamoja na kuunganishwa kwa kadi mbalimbali za malipo kuwa mfumo mmoja ili kurahisisha upatikanaji wa huduma kirahisi nakuwawezesha walipa kodi kutekeleza majukumu yao bila kulazimika kufika ofisi za Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).
TRA kubadilishwa jina
Sambamba na hayo, tume pia imetoa pendekezo la kubadilisha jina la TRA kuwa Huduma za Mapato Tanzania (TRS) ili kuakisi mabadiliko ya kimtazamo na kuimarisha utoaji wa huduma kwa walipa kodi.
“Tumeona nchi nyingi ambazo wanaitwa hivyo, wala haitawapunguzia hadhi yao,” amesema Balozi Sefue.
Latest