Kuzimwa kwa intaneti kunavyoathiri maisha ya Watanzania
- Husababisha kusimama kwa shughuli za kiuchumi, kuvuruga mawasiliano, hasara ya kifedha na huathiri elimu na huduma za afya.
- Matukio ya kuzimwa kwa intaneti hutokea zaidi wakati wa Uchaguzi Mkuu.
- Wadau washauri sera na sheria za mtandao ziangaliwe upya kutatua changamoto hiyo.
Dar es Salaam. Kati ya Oktoba 29 na Novemba 3, 2025, Tanzania ilishuhudia hitilafu kubwa ya kutopatikana kwa huduma za kidijitali. Baadhi ya huduma za kijamii zinazohitaji mtandao zilisimama. Watumiaji wa benki za mtandaoni hawakuweza kufikia akaunti zao na kufanya miamala. Hata watumiaji wa majukwaa ya kidijitali walikosa haki ya kupata taarifa, kutoa maoni na kuwasiliana.
Sababu ilikuwa moja tu. Intaneti ilizimwa. Kuzimwa kwa intaneti kulihusishwa na vurugu zilizotokea katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana uliompa ushindi Rais Samia Suluhu Hassan.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Thabit Kombo alisema Serikali ilichukuwa hatua hiyo ya kuzima intaneti ili kudhibiti hali ya kiusalama na kusambaa kwa habari potofu kutokana na ghasia zilizoshuhudiwa kipindi hicho.
Hilo siyo tukio la kwanza. Katika Uchaguzi Mkuu wa 2020 uliomuweka madarakani Hayati Rais John Magufuli, intaneti ilizimwa kwa siku saba, sambamba na kuzuiwa kwa mitandao ya kijamii ikiwemo X (zamani Twitter), Facebook, YouTube na WhatsApp.
Kuzimwa kwa intaneti husababisha kusimama kwa shughuli za kiuchumi, kuvuruga mawasiliano, hasara ya kifedha na huathiri elimu na huduma za afya.
Pia kupunguza upatikanaji wa taarifa kwa jamii, jambo ambalo wadau wa teknolojia wanasema liangalie upya kisheria ili kuzuia hali kama hiyo isitoe siku zijazo.
Mtaalam wa teknolojia na ulinzi mtandaoni, Anwar Said anasema matukio ya kuzimwa kwa intaneti au kupunguza kasi yake yakifanyika yanapunguza imani ya wananchi kutumia miundombinu ya kidijitali ya umma (DPI) jambo linaloathiri uimara wake katika ukuaji wa uchumi.
“Athari ya kwanza ni imani ya ile mifumo (DPI) itaondoka kwa watumiaji. Hasara nyingine ni collective punishment (adhabu ya pamoja) yaani unapozima mtandao kwa wafanyabiashara wadogo hasa mawinga wanaotegemea intaneti kufanya shughuli zao ndio wanaumia zaidi kwenye hii adhabu ya pamoja.
“Inawezekana kosa lipo, kuna watu wanasambaza habari potofu lakini unapozima (intaneti) moja kwa moja yule aliyefanya kosa umempata na hawa ambao hawahusiki wanakua wamepata madhara makubwa,” anasema Said.

Intaneti hufungua fursa mbalimbali za kibiashara na mawasiliano na kuchangia katika ukuaji wa uchumi wa mtu mmoja mmoja na Taifa. Picha | Nukta Africa.
Kwa mujibu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), hadi kufikia Desemba 2025, Tanzania ilikuwa na watumiaji wa intaneti milioni 58.1 ikiwa ni takriban mara mbili ya watumiaji waliokuwepo miaka mitano iliyopita.
Matumizi ya intaneti yamechochewa zaidi na ongezeko la watumiaji wa simu za mkono ikiwemo simu janja. Hadi Desemba 2025, TCRA inaeleza kulikuwa na watumiaji simu milioni 106.9 nchini.
Isack Nyaimaga, mtumiaji wa majukwaa ya kidijitali ikiwemo huduma za malipo anasema intaneti kwake ni eneo la kazi, ikizimwa inamkosesha fursa za kupata kipato na wakati mwingine imekuwa ikimsababishia msongo wa mawazo.
“Kuzimwa kwa mtandao ni hali ambayo ilikuwa ngumu kwangu binafsi kwa sababu muda mwingi nategemea mtandao, kazi zangu zote bila mtandao haziendi,” anasema Nyaimaga. “Siku ambayo mtandao unazimwa (Oktoba 29, 2025) nilikuwa nataka kufanya miamala. Imagine (Fikiria) nilikuwa natuma muamala Nigeria ukashia njiani. Ilikuwa ni experience ambayo ilinipa msongo wa mawazo.”
Nyaimaga, mkazi wa jijini Dar es Salaam anapendekeza wadau wakiwemo wabunifu wa teknolojia kubuni njia mbadala zitakazosaidia huduma za kidijitali kufanya kazi hata kama kuna changamoto za intaneti ili kupunguza madhara kwa watu.
Kuzima intaneti ni kukiuka haki za binadamu
Licha ya Serikali kudai kuwa uzimaji wa intaneti husaidia kudhibiti vurugu na kusambaa kwa habari za uzushi na upotoshaji wakati wa uchaguzi, Tume ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu (ACHPR) inaeleza kuwa Tanzania ilipaswa kuepuka kuzima huduma za intaneti.
Taarifa ya ACHPR iliyotolewa Novemba 1, 2025 inaeleza kuwa kitendo hicho kinakiuka uhuru wa kujieleza na upatikanaji wa taarifa kama ilivyoainishwa katika Ibara ya 9 na 19 za Mkataba wa Afrika wa Haki za Binadamu na Watu na Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Kiraia na Kisiasa.
Watoa huduma mtandaoni nao waguswa
Mwanzilishi mwenza wa programu tumishi ya Sheria Kiganjani, Musa Kisena anasema intaneti ilipozimwa mwaka jana, shughuli zao zilisimama na watu wanaowahudumia hawakupata huduma za kisheria kutatua changamoto zao za maisha.
“Sisi shughuli zetu kwa asilimia 90 zinategemea intaneti. Tukikosa intaneti kwa siku tano tutakosa chakula,” anasema Kisena. “Intaneti ikiyumba na biashara yetu inayumba maana yake inatuathiri kiuchumi na sehemu zote hizo.
Sheria Kiganjani ilibuniwa na vijana wa Tanzania kwa lengo kuu moja; kuzifanya huduma za kisheria kupatikana kwa kila mtu na sehemu yoyote kwa njia ya simu za mkononi.

Pesa zinazopotea intaneti ikizimwa
Kampuni ya NetBlocks ya Uingereza inayofuatilia utendaji wa intaneti duniani, inakadiriwa kuzimwa kwa intaneti Tanzania kati ya Oktoba 29 na Novemba 3, 2025 kulikodumu kwa saa 126, kumesababisha hasara ya Dola za Marekani 72.3 milioni sawa na Sh176.8 milioni kwa viwango vya kubadilisha fedha vya Desemba 2025.
Kwa mujibu wa ripoti ya hivi karibuni ya Gharama ya Kuzima Intaneti iliyotolewa na kampuni ya Top10VPN ya Uingereza, hasara za kimataifa zilizotokana na kuzimwa kwa makusudi kwa intaneti ziliongezeka hadi Dola za Marekani bilioni 19.7 (Sh50.2 trilioni), sawa na ongezeko la asilimia 156 ikilinganishwa na mwaka 2024.
Serikali katika nchi 28 ikiwemo Tanzania mwaka jana, zilisababisha kukatika kwa intaneti kwa zaidi ya saa 120,000 mwaka 2025, huku matukio mengi yakiripotiwa nchini Urusi.
Kulikuwa na ongezeko la asilimia 47 la saa za kuzimwa kabisa kwa intaneti na ongezeko la asilimia 66 la saa za kuzimwa kwa mitandao ya kijamii ikilinganishwa na mwaka 2024.
NetBlocks na Top10VPN zinaeleza kuwa kuzimwa kwa intaneti kulisababisha hasara katika uzalishaji, biashara na huduma za mtandaoni ikiwemo za malipo, jambo ambalo linaathiri ujenzi wa DPI duniani.
Jinsi ya kushughulikia changamoto ya kuzimwa kwa intaneti
Ripoti iliyoaangazia haki za kidijitali na uzimaji wa intaneti wakati wa Uchaguzi Mkuu iliyotolewa na Shirika la Tech and Media Convergency (TMC), Novemba 2025, inapendekeza kukomesha hatua za kupunguza kasi ya intaneti na zuio la sehemu fulani ya mawasiliano na kurejesha kikamilifu huduma za intaneti nchi nzima.
“Hii inajumuisha upatikanaji usio na mipaka wa mitandao yote ya kijamii na majukwaa ya kutuma ujumbe,” imeeleza ripoti hiyo.
TMC katika ripoti hiyo inapendekeza kupitia upya na kufuta sheria kandamizi, zikiwemo baadhi ya vifungu vya Sheria ya Makosa ya Mtandao 2015 na Kanuni za TCRA zinazotoa mamlaka makubwa kwa Serikali kuamuru udhibiti wa mawasiliano, ufuatiliaji, na kuzimwa kwa huduma za intaneti.

Kuzima intaneti bila sababu za msingi ni ukiukaji wa haki za binadamu ikiwemo kumkosesha mtu uhuru wa kujieleza na kupata taarifa kupitia majukwaa ya mtandaoni. Picha | Deccan Herald.
Kuzimwa kwa intaneti hakupaswi kuwa suluhu ya kwanza katika kushughulikia migogoro ya kisiasa. Na pale kunapokuwa na ulazima wa kufanya hivyo, mchakato wa kuzima na kurejesha huduma unapaswa kuwa wa kisheria na wazi.
Kwa sasa, Tanzania haina sheria za moja kwa moja za kudhibiti intaneti. TMC inapendekeza kuwa suala hili linapaswa kushughulikiwa kwa haraka. Sheria hizo zitakapopitishwa, zinapaswa kuwa za haki, sahihi na zisizo na utata.
Chama cha Intaneti duniani (Internet Society) katika mapendekezo ya kisera kuhusu kuzimwa kwa intaneti kinaeleza kuwa Serikali zinapaswa kupitisha sera ya kutosimamisha au kuzima huduma za mtandao kama sehemu ya dhamira yao ya kuendeleza mtandao ulio wazi na usio na vizuizi.
“Badala ya kukimbilia kuzima mtandao, zinapaswa kushughulikia changamoto katika chanzo chake,” inaeleza sehemu ya mapendekezo ya chama hicho.
Internet Society inaeleza zaidi kuwa Ili kulinda uchumi na kudumisha uaminifu pamoja na utegemevu wa miundombinu, serikali zinapaswa kuchambua athari hasi za kuzima mtandao katika uzalishaji, imani ya wafanyabiashara, na uwekezaji wa kifedha wa muda mfupi na mrefu.
Latest