Sababu zinazoweza kuathiri uwezo wa mwanamke kupata ujauzito

February 24, 2026 5:50 pm · Fatuma Hussein
Share
Tweet
Copy Link
  • Ni pamoja na kuziba kwa mirija ya uzazi,  na mzunguko usio sahihi wa hedhi na matatizo ya homoni.

Dar es Salaam. Utasa, au hali ya kushindwa kubeba ujauzito ni miongoni mwa changamoto zinazowakumba mamilioni ya wanawake duniani kote suala linalowakosesha furaha ya kuitwa mama.

Shirika la Afya Duniani (WHO) linakadiria kuwa mtu mmoja kati ya watu wazima sita wenye uwezo wa kuzaa duniani hukumbwa na changamoto ya utasa katika kipindi fulani cha maisha yao.

Daktari Bingwa wa Uzazi na Magonjwa ya Wanawake katika Hospitali ya Taifa Muhimbili, Dk Benny Kimaro, ameiambia Nukta Habari kuwa miongoni mwa sababu kubwa ya utasa ni kuwa na mzunguko usioeleweka pamoja na uwiano usio sahihi wa homoni.

Kwa mujibu wa daktari huyo, mzunguko wa hedhi wa mwanamke unapaswa kuruhusu yai kuzalishwa kila mwezi lipevuke vizuri ili liweze kukutana  na mbegu ya kiume kwa ajili ya kutungisha mimba.

Uwezo wa kushika mimba unategemea ushirikiano wa mifumo kadhaa ya mwili wa mwanamke pamoja na ubora wa mbegu za mwanaume.

“Ili ujauzito upatikane, ni lazima yai lipevuke vizuri, mirija iwe wazi, kizazi kiwe katika hali nzuri na homoni ziwe katika uwiano sahihi,” anasema Dk Kimaro.

iwapo mzunguko wa hedhi ya mwanamke hauelewiki husababisha mayai ya mwanamke kutokukomaa kwa wakati  au yasitoke kabisa suala ambalo liinachangiwa zaidi na  mvurugiko wa homoni au ugonjwa wa PCOS (Polycystic Ovary Syndrome).

Fibroids (leiomyomas) hupatikana kwa asilimia 20-70 ya wanawake wakiwa na umri wa kuzaa. Picha/ Canva. 

Hitilafu katika mji wa mimba 

Mji wa mimba ni sehemu maalum ambayo mimba hujishikiza baada ya kutungwa na kuruhusu ukuaji wa mtoto kwa miezi tisa.

Hitilafu yoyote katika eneo hili ikiwemo fibroids (uvimbe usio wa saratani kwenye kizazi), unaojulikana pia kama myoma, pamoja na endometriosis, (tishu za kizazi hukua nje ya mfuko wa uzazi) huweza kusababisha mwanamke kushindwa kubeba mimba au kuharibika mara kwa mara.

Kuziba kwa mirija ya mfuko wa uzazi

Changamoto nyingine ni kuziba kwa mirija ya uzazi ambako kunasabishwa na maambukizi kama PID au magonjwa ya zinaa na kuzia urutubishaji na usafirishai wa yai kwenda katika mji wa mimba.

“Inapotokea changamoto katika swala zima la mirija ina maana basi makutano ya mbegu na yai hayawezi kufanyika. Changamoto hauwezi kupata ujauzito,” amesema Dk Kimaro.

Hata hivyo, Dk Kimaro ameongeza kuwa mwanamke mwenye mrija mmoja bado anaweza kupata ujauzito, ingawa inaweza kuchukua muda mrefu zaidi. 

Endapo mirija yote imeathirika, teknolojia ya uzazi wa kusaidiwa kama upandikizaji (IVF) inaweza kuwa mbadala. 

Uwezo wa kushika mimba unategemea ushirikiano wa mifumo ya homoni, mayai yenye afya, na mji wa mimba wa mwanamke, pamoja na mbegu bora za mwanaume. Picha/ Canva.

Mbegu bora za mwanaume zatajwa

Licha ya jamii mara nyingi kuelekeza lawama kwa mwanamke, Dk Benny Kimaro anaeleza kuwa takribani asilimia 30 hadi 35 ya changamoto za uzazi zinamhusu mwanaume. 

Anabainisha kuwa ubora wa mbegu za kiume hupimwa kwa kuangalia idadi, uwezo wa kusogea, pamoja na umbo lake . 

Mbegu inapaswa kuwa na kichwa chenye uwezo wa kupenya kwenye yai na mkia unaoiwezesha kusafiri kwa kasi kuelekea kulikopo yai, kasoro katika vigezo hivi hupunguza uwezekano wa urutubishaji.

Kitaalamu, mwanaume anatakiwa kuwa na angalau mbegu milioni 15 kwa kila mililita moja ya shahawa ili kuongeza uwezekano wa ujauzito.

Idadi au ubora duni wa mbegu hupunguza uwezekano wa yai kurutubishwa na kati ya mbegu hizo,ni mbegu moja tu (au mbili kwa mapacha) ndiyo hufanikiwa kurutubisha yai.

 Wataalamu wanashauri wanandoa wote wawili kufika kliniki pamoja kwa ajili ya vipimo na ushauri badala ya kumlaumu mmoja.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Follow Us on TikTok

Subscribe to Our YouTube Channel

Subscribe

Loading videos...

Loading videos...

Loading videos...

Enable Notifications OK No thanks