Musk kujenga makazi ya binadamu mwezini

February 9, 2026 4:07 pm · Kelvin Makwinya
Share
Tweet
Copy Link
  • Ni baada ya kubadilisha mwelekeo kutoka mpango wake wa muda mrefu kujenga mji huo sayari ya Mars.
  • Musk anaamini maisha nje ya dunia ni bima ya kumfanya binadamu kuendelea kuwepo hata kama ingekumbwa na majanga makubwa. 

Dar es Salaam. Mwanzilishi wa kampuni binafsi ya anga ya SpaceX na tajiri namba moja duniani, Elon Musk, ametangaza mpango mpya wa kujenga makazi ya kudumu ya binadamu mwezini tofauti na maono ya awali ya kujenga makazi hayo katika sayari ya Mars.

Musk ametangaza uamuzi huo leo Februari 9, 2026 kupitia ukurasa wake wa mtandao wa kijamii anaoumiliki X (zamani Twitter) akifafanunua kuwa uharaka wa kufanikisha ujenzi huo ni miongoni mwa sababu za kufanya maamuzi hayo.

“Tunaweza kufanikisha hilo (ujenzi wa makazi hayo) chini ya miaka 10, wakati katika sayari ya Mars ingechukua zaidi ya miaka 20.” amesema Musk kupitia mtandao wa X.

Musk mwenye umiliki wa asilimia 46 ya hisa zote za kampuni ya SpaceX itakayohusika na ujenzi huo amebainisha sababu nyingine iliyomsukuma kuhamishia ujenzi huo mwezini ni muda wa ufikaji.

Kwa mujibu wake, safari ya kwenda mwezini kutoka duniani huchukua siku mbili suala litakaloiwezesha kampuni yake kusafiri mara tatu kwa mwezi tofauti na safari ya kuelekea Mars inayochukua takriban miezi 6 ambayo ni mara 90 zaidi ya safari ya mwezini.

Hata hivyo, Musk amebainisha kuwa licha licha ya kubadili uelekeo mpango wa kujenga mji katika sayari ya Mars bado haujafutwa na kubainisha kuwa mpango huo utaendelea katika miaka mitano mpaka saba ijayo.

Binadamu kuwa viumbe wa sayari nyingi

Mpango wa Musk wa kuwezesha maisha ya binadamu ulianza mapema mwaka 2001 kabla ya kuanzisha kampuni ya SpaceX mwaka 2002 huku lengo kuu ilikiwa ni sayari ya Mars.

Kwa mujibu wa Musk, dhana hii ilisukumwa zaidi na hatari za muda mrefu zinazokabili Dunia, ikiwemo mabadiliko ya tabianchi, vita, magonjwa na majanga mengine ya asili jambo lililomfanya kuona makazi nje ya Dunia kama bima ya kuhakikisha kwamba hata kama Dunia itapata majanga makubwa binadamu ataendelea kuwepo.

Musk anaamini maisha nje ya dunia ni bima ya kumfanya binadamu kuendelea kuwepo hata kama ingekumbwa na majanga makubwa. Picha | Business Insider.

Mwaka 2020 Musk aliwahi kuahidi kuwa mpaka kufikia mwaka 2026 binadamu ataweza kutua katika sayari ya Mars hata hivyo, changamoto za kiteknolojia, kifedha na ushirikiano wa kimataifa zimepelekea SpaceX kurekebisha ramani yake ya muda mfupi.

Ikiwa Musk atafanikisha mpango wake basi wa kujenga makazi ya kudumu nje ya Dunia, binadamu ataingia katika hatua mpya ya kihistoria ya kuwa viumbe ama spishi zinazopatikana katika sayari nyingi ulimwenguni. (multi-planetary species). 

Musk anatangaza hatua ya kubadilisha mpango wa maisha ya binadamu nje ya dunia ikiwa ni siku chache tu tangu atangaze kuunganisha kampuni yake ya SpaceX na kampuni yake ya akili bandia (AI) na mitandao ya kijamii ya xAI na kufanya kampuni yenye thamani kubwa zaidi duniani ikiwa na thamani ya takriban Dola za Marekani trilioni 1.25.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Follow Us on TikTok

Subscribe to Our YouTube Channel

Subscribe

Loading videos...

Loading videos...

Loading videos...

Enable Notifications OK No thanks