Hitilafu ya roketi yakwamisha Nasa kwenda mwezini
- Jaribio hilo limeahirishwa kutokana na injini namba tatu kutozalisha moto wa kutosha.
- Likifanikiwa litakuwa jaribio la pili baada ya miaka 50 kupita.
- Ni maandalizi ya kuwapeleka binadamu ifikapo mwaka 2025.
Dar es Salaam. Hitilafu katika moja ya injini nne za roketi ya Shirika la Anga za Juu la nchini Marekani (Nasa) imekwamisha jaribio la kwenda mwezini lililotakiwa kufanyika leo Agosti 30.
Jaribio hilo ni utekelezaji wa misheni ya Artemis 1 inayokusudia kufanya majaribio kadhaa ya kwenda na kuuzunguka mwezi kisha kwenda katika sayari ya Mirihi (Mars) ikiwa ni maandalizi ya kuwapeleka watu ifikapo mwaka 2025.
Misheni hiyo ilitakiwa kufanyika kutokea kituo cha Nasa cha Kennedy kilichopo katika jimbo la Florida nchini Marekani na taarifa iliyochapishwa na Nasa imesema jaribio hilo limeahirishwa kutokana na injini namba tatu kutozalisha moto wa kutosha.
“Baada ya ukaguzi wa Mfumo wa Uzinduzi wa Anga (SLS), wahandisi waligundua tatizo katika mojawapo ya injini nne za RS-25 la kutofikia viwango vya joto vinavyofaa na kutokana na hilo tumesitisha uzinduzi leo, timu itatangaza tarehe mpya,” imeeleza Nasa.
Inatarajiwa hii leo jopo la wahandisi litakutana kujadiliana suala hilo ingawa inahisiwa jaribio la pili litafanyika mapema Septemba 2 mwaka huu.
Umesoma hii?:
Jaribio hili linafanyika ikiwa imepita miaka hamsini tangu Marekani walipofanya misheni ya Apollo mwaka 1972 ambapo ilishuhudiwa binadamu akifika mwezini kwa mara ya kwanza.
Roketi yenye nguvu zaidi kuwahi kutengenezwa na Nasa itakisukuma chombo cha anga za juu cha Orion hadi mwezini kwa kasi ya kilomita 39,400 kwa saa kuukabili umbali wa kilomita 386,000 mpaka kuufikia mwezi.
Ikiwa kila kitu kitakwenda sawia chombo hicho kitakamilika kuuzunguka mwezi mwaka 2024 ambapo wanaanga wa Marekani wanatarajia kupeleka binadamu katika uso wa mwezi mwishoni mwa mwaka 2025 huku jambo hilo likirushwa mubashara Youtube.
Katika miaka ya hivi karibuni mataifa makubwa duniani kama Marekani, China na Urusi yamekuwa yakioeshana umwamba katika medani ya teknolojia ya anga za juu kwa kurusha vyombo ikiwemo satelaiti na roketi zinazoenda katika sayari ya Mirihi.
Latest
