Watengeneza maudhui Kenya wavuna mamilioni TikTok, Tanzania ikisuasua
- Ni kupitia kipengele cha ‘Tiktok for Business’ ambacho hakipo kwa Tanzania.
- Kwa sasa kipengele hiko kinapatikana kwenye mataifa 70 duniani huku Mataifa ya Afrika yakiwa ni matano tu ambayo ni Misri, Kenya, Morocco, Nigeria na Afrika Kusini.
Dar es Salaam. Zaidi ya watengeneza maudhui 200 nchini Kenya wamepata mapato ya zaidi ya Sh45 milioni za Kenya (zaidi ya Sh900 milioni za Tanzania) ndani ya mwaka mmoja kupitia kipengele kipya cha ‘Tiktok for Business’ kilichopo ndani ya mtandao wa TikTok.
Takwimu za mtandao wa Tiktok zilizotolewa hivi karibuni zinaonyesha kuwa Dola za Marekani 350,000, zilipatikana kupitia ushirikiano wa matangazo na makampuni mbalimbali uliofadhiliwa kupitia jukwaa hilo tangu ilipoanzishwa mwaka 2025.
Jochen Bischoff, Mkuu wa Biashara za Kimataifa wa TikTok kwa Afrika, ameliambia Shirika la Habari la Kenya, ‘The Star’ kuwa matokeo hayo yanaonesha jinsi watengenezaji wa maudhui wanavyoweza kutumia majukwaa ya kidijitali kufungua fursa za kiuchumi.
‘Tiktok for Business’ ni nini?
TikTok for Business ni jukwaa la kibiashara la TikTok lililoundwa mahsusi kusaidia biashara, makampuni, na watengenezaji wa maudhui kufanikisha masoko yao kwa njia ya kidijitali.
Jukwaa hili linatoa zana za uchambuzi na ripoti ikiwemo utendaji wa matangazo na kukuza matangazo yakiwemo ‘In-Feed Ads’, ‘TopView’, ‘Brand Takeovers’, pamoja na ‘Hashtag Challenges’ zinazowezesha watumiaji kuingiliana na makampuni kupitia ubunifu.

‘Tiktok for Bussiness’ inawapa mapato watengeneza maudhui kupitia kampeni za matangazo kutoka kwa makampuni huku ikipanua biashara kufikia soko la kimataifa na kuongeza mauzo au uelewa wa bidhaa.
Kwa mujibu wa vyombo vya habari vya Kenya kama The Star, Pulse Kenya, na TechTrendsKE, programu hii ya biashara ya TikTok inachangia ukuaji wa uchumi wa kidijitali na inavutia uwekezaji mkubwa kutoka kampuni za ndani na za kimataifa kuwekeza nchini humo.
Tanzania bado kitendawili
Wakati Kenya ikianza kunufaika na mtandao huo, hali ni tofauti kwa watengenezaji wa maudhui nchini Tanzania ambao bado hawajafikiwa na kipengele hicho.
Hii inamaanisha watengenezaji wa maudhui kupitia Tiktok nchini Tanzania hutegemea vipengele kama kutumiwa zawadi wakiwa mbashara (live gifts) na mashabiki, mikataba binafsi na makampuni ya ndani, matangazo ya bidhaa na ushawishi wa mitandao (influencer marketing) pekee kujipatia kipato kupitia mtandao huo.

Kwa sasa kipengele cha TikTok for Business inapatikana kwenye mataifa 70 duniani huku Mataifa ya Afrika yakiwa ni matano tu ambayo ni Misri, Kenya, Morocco, Nigeria na Afrika Kusini.
Hata hivyo, Serikali ya Tanzania Inaendelea kuimarisha mazingira kwa watengenezaji wa maudhui, na hivi karibuni Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo ilizindua mfuko wa Sh2 bilioni kwa lengo la kuwawezesha watengeneza maudhui kama hatua ya kuimarisha uchumi wa ubunifu na matumizi ya teknolojia ya kidijitali nchini.
Latest