Serikali, NMB kushirikiana kutoa mikopo nafuu kuinua wajasiriamali wadogo
- Mikopo hiyo inawalenga wafanyabiashara wenye mauzo ghafi yasiyozidi kiasi cha Sh4,000,000 kwa mwaka, wakiwemo mama na baba lishe, machinga, waendesha bodaboda, waendesha guta.
- Makundi mengine yanayotambuliwa na kusajiliwa na mamlaka husika katika maeneo mbalimbali nchini
Dar es Salaam. Serikali imeingia makubaliano na Benki ya NMB kwa lengo la kutoa mikopo yenye masharti nafuu kwa wafanyabiashara ndogondogo nchini, hatua inayolenga kuongeza mitaji ya biashara na kukuza uchumi jumuishi.
Kwa mujibu wa taarifa kwa umma iliyotolewa leo Januari 30, 2026, Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dk Dorothy Gwajima, amesema makubaliano hayo yameiwezesha Benki ya NMB kusimamia utoaji wa mikopo ya Serikali yenye riba ya asilimia saba kwa mwaka kwa wafanyabiashara ndogondogo watakaokidhi vigezo vilivyowekwa.
“Serikali imeingia makubaliano na Benki ya NMB kusimamia mikopo ya Serikali yenye masharti nafuu na riba ya asilimia saba kwa mwaka kwa lengo la kuwawezesha wafanyabiashara ndogondogo nchini,” imesema sehemu ya taarifa hiyo iliyotolewa na Waziri Dk Gwajima.
Dk Gwajima ameeleza kuwa mikopo hiyo inawalenga wafanyabiashara wenye mauzo ghafi yasiyozidi kiasi cha Sh4,000,000 kwa mwaka, wakiwemo mama na baba lishe, machinga, waendesha bodaboda, waendesha guta, pamoja na makundi mengine yanayotambuliwa na kusajiliwa na mamlaka husika katika maeneo mbalimbali nchini.
Kwa vijana na wajasiriamali wa Tanzania, hatua ya Serikali kuingia makubaliano haya ni fursa muhimu kwao kuweza kupata mitaji kwa masharti nafuu, kuanzisha au kupanua biashara zao, kuongeza uzalishaji na ajira, na hivyo kujiimarisha kiuchumi na kuboresha maisha yao kwa ujumla.
Jinsi ya kupata mkopo
Kwa mujibu wa taarifa hiyo kwa vyombo vya habari , ili kunufaika na mikopo hiyo, mwombaji anatakiwa kuwa Mtanzania mwenye umri usiopungua miaka 18, awe na kitambulisho cha Taifa au namba ya NIDA, na awe ametambuliwa na kusajiliwa katika mfumo wa utambuzi na usajili wa wafanyabiashara ndogondogo (WBN–MIS).
Dk Gwajima ameeleza kuwa utaratibu wa kuomba mikopo hiyo ni rahisi, mwombaji anatakiwa kufika katika tawi la Benki ya NMB, kujaza fomu ya maombi na kuwasilisha nyaraka zinazohitajika.
Ameongeza kuwa mikopo hiyo ina masharti nafuu ikilinganishwa na mikopo ya kawaida ya kibiashara. Mbali na riba ya asilimia saba kwa mwaka, pia kuna muda wa marejesho kuanzia miezi mitatu hadi 24 kulingana na aina ya biashara. Aidha, mkopo huo utakuwa na bima dhidi ya kifo na ulemavu wa kudumu kwa mkopaji.
Latest