BoT: Dhahabu itakayouzwa haitatumika kugharamia miundombinu Tanzania

January 30, 2026 5:23 pm · Fatuma Hussein
Share
Tweet
Copy Link
  • Imesema inatarajia kuuza ili kuweka uwiano wa akiba na kuwekeza katika fedha za kigeni.

Dar es Salaam. Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imesema imepanga kuuza sehemu ya akiba ya dhahabu kwa ajili ya kuongeza mali nyingine za benki hiyo na si kufadhili miradi ya maendeleo ya Serikali.

BoT imekuwa ikinunua akiba ya dhahabu kutoka katika soko la ndani kwa ajili ya kuongeza akiba ili kukabiliana na mitikisiko ya kiuchumi inayotokana na mabadiliko ya Dola ya Marekani.

Mkurugenzi wa Masoko ya Fedha wa BoT, Emmanuel Akaro amewaambia wanahabari jijini Dar es Salaam kuwa benki hiyo huweza kuuza sehemu ya dhahabu ili kununua mali nyingine, ikiwemo Dola za Marekani, tofauti na madai yaliyoripotiwa na baadhi ya vyombo vya habari.

“Ni kweli kuna mpango wa kuuza dhahabu, lakini tumefikia kiwango tulichokusudia kiwe kwenye mizania yetu (Dola za Marekani bilioni 2 kiwango elekezi). Tunapozidi kiwango hicho, kuna vihatarishi, hivyo tunalazimika kuuza. Uamuzi wa kuuza unategemea hali ya soko,” amesema Akaro.

Hata hivyo, hakubainisha siku na kiwango cha dhahabu walichopanga kuuza.

Akaro amesema leo Januari 30, 2026 kuwa hatua hiyo itasaidia kuzawasizisha uwiano wa akiba za rasilimali za BoT.

Katika maelezo yake, amesema BoT haiuzi dhahabu ya akiba ya Taifa kwa ajili ya kufadhili miradi ya miundombinu ya Serikali kama ilivyokuwa imeripotiwa na mashirika ya habari ya kimataifa ya Bloomberg na Business Insider. 

Uuzwaji huu wa dhahabu utategemea na mwenendo wa wa bei iliyopo sokoni. Picha/ Doing Business Tanzania.

Katika habari hiyo, vyombo hivyo vilikuwa vimeeleza kuwa Serikali ipo mbioni kuuza dhahabu kugharamia miradi ya maendeleo, jambo lililoibua mjadala mkubwa mtandaoni na baadhi ya wataalamu wa uchumi.

Vyombo hivyo vya habari vilimnukuu Waziri wa Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo, akieleza kuwa Tanzania inapanga kuuza sehemu ya akiba ya dhahabu kwa sababu ya kupungua kwa misaada ya maendeleo kutoka nchi za Magharibi.

Hadi sasa, Akaro ameeleza, Tanzania inamiliki dhahabu fedha, iliyosafishwa yenye thamani ya takribani Dola za Marekani bilioni 3.24, sawa na zaidi ya Sh7 trilioni huku zoezi hilo la ununuzi na uuzaji wa madini hayo likiwa endelevu.

Aidha, Akaro ameeleza kuwa ununuzi na uuzaji wa dhahabu unaofanywa na Benki Kuu ni shughuli za kawaida za usimamizi wa akiba, zinazolenga kudhibiti hatari na kurekebisha uwiano wa uwekezaji.

Kwa mujibu wa sheria BoT ya mwaka 2006, benki hiyo ina wajibu wa kununua, kuhifadhi na kusimamia dhahabu kama sehemu ya akiba ya fedha za kigeni. 

Hata hivyo, sheria hiyo hairuhusu matumizi ya moja kwa moja ya dhahabu kufadhili miradi ya maendeleo ya Serikali.

Kwa mujibu wa BoT, hadi mwisho wa Desemba 2025 akiba ya dhahabu ya Tanzania ilikuwa na thamani ya takribani dola za Marekani bilioni 1.3, ikiwa ni sehemu ya jumla ya akiba ya fedha za kigeni inayozidi dola bilioni 6.5. 

Katika uchumi wa Tanzania, dhahabu inaendelea kuwa nguzo muhimu ikichangia zaidi ya asilimia 22 ya mauzo ya nje ya nchi. 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Follow Us on TikTok

Subscribe to Our YouTube Channel

Subscribe

Loading videos...

Loading videos...

Loading videos...

Enable Notifications OK No thanks