Serikali: Mauzo ya bidhaa za nje kufikia asilimia 26.1 mwaka 2030
- Ni kwa lengo la kuimarisha uchumi wa Taifa, kuongeza mapato ya fedha za kigeni na kupanua fursa za biashara.
Dar es Salaam. Serikali imeweka mkakati wa kukuza mauzo ya nje ya bidhaa na huduma kutoka kiwango cha sasa cha asilimia 17.8 hadi kufikia asilimia 26.1 ifikapo mwaka 2030, hatua inayolenga kuimarisha uchumi wa Taifa, kuongeza mapato ya fedha za kigeni na kupanua fursa za biashara.
Waziri wa Viwanda na Biashara, Judith Kapinga, aliyekuwa akizungumza na wanahabari leo Januari 24, 2026 amesema mpango huo utafikiwa kwa kuuza bidhaa nyingi zilizoongezewa thamani kuliko malighafi.
“Ili tuweze kuuza zaidi kuna haja ya kuongeza thamani, ili tunapouza tusiuze malighafi tuuze bidhaa zilizoongezwa thamani, ndio maana Rais Samia Suluhu Hassan alianzisha kongani za viwanda kila wilaya….
….Lengo letu mazao yakitoka huko yatoke kama bidhaa iliyoongeza thamani,” amesema Kapinga wakati akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa ahadi za Rais Samia ndani ya siku 100 za uongozi wake kwa awamu ya pili.
Kapinga amesema ili kufikia lengo hilo, Serikali imejipanga kukuza mauzo ya nje kwa wastani wa asilimia 8.5 kila mwaka, ikilenga kuzalisha zaidi kwa ajili ya soko la nje kuliko mahitaji ya ndani ya nchi.

Tanzania imekuwa ikisafirisha bidhaa mbalimbali kwenda masoko ya nje, zikiwemo dhahabu na madini mengine, bidhaa za kilimo, pamoja na bidhaa za viwandani kama saruji, bidhaa za chuma na vyakula vilivyosindikwa huku masoko makuu yakiwa ni nchi za Asia, Ulaya, Mashariki ya Kati na Afrika. Picha | Mwananchi
Kwa muda mrefu, Tanzania imekuwa ikisafirisha bidhaa mbalimbali kwenda masoko ya nje, zikiwemo mazao ya kilimo, mazao ya baharini na vito vya thamani hatua iliyopaisha mchango wa sekta ya viwanda na biashara hadi asilimia 7.3 mwaka 2024.
Wawekezaji wa ndani kulindwa
Ili kulinda na kuhamasisha wafanyabiashara na wawekezaji wa ndani, Kapinga amesema Serikali itaendelea kuwalinda kwa kuondoa kodi ya ongezeko la thamani (VAT) kwa kampuni za wazawa zilizosajiliwa nchini.
Watakaopewa kipaumbele zaidi ni wazawa waliosajiliwa na Mamlaka ya Uwekezaji na Maeneo Maalumu ya Kiuchumi Tanzania (Tiseza) wanaouza bidhaa nje ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).
“Hakika ni faida kubwa kwa wafanyabiashara wetu, kwa uchumi wa Taifa letu na wananchi wote kwa ujumla,” amebainisha Kapinga.
Huenda mpango wa Serikali kuondoa VAT kwa wazawa ukafungua fursa zaidi kwa wazalishaji wa ndani hatua itakayopanua masoko na upatikanaji wa ajira.
Latest