Bima ya Afya kwa Wote kuanza rasmi Januari 26
- Awamu ya kwanza kuanza na makundi maalum ikiwemo wajawazito, wazee na watoto.
- Bei mpya ya kitita yatangazwa.
Dar es Salaam. Serikali imetangaza kuanza rasmi kwa utekelezaji wa awamu ya kwanza ya Bima ya Afya kwa Wote (BAW) kuanzia Jumatatu, Januari 26, 2026 hatua inayolenga kupunguza mzigo wa gharama za matibabu kwa wananchi, hususan makundi yasiyo na uwezo.
Akizungumza leo Januari 24, 2026, Waziri wa Afya Mohamed Mchengerwa katika kikao kazi cha kitaifa cha kujadili utekelezaji wa mpango huo, amesema bima hiyo itaanza kutumika kwa kitita cha huduma muhimu, kitakacholenga makundi yaliyo hatarini.
Makundi hayo yanajumuisha wazee, watoto, wajawazito na watu wenye ulemavu, ambao gharama zao zitagharamiwa na Serikali huku Wananchi wa kawaida wakitangaziwa bei mpya ya kitita cha huduma muhimu.
“Bei ya kitita hicho ni Sh150,000 kwa kaya isiyozidi watu sita, kikiwa kinazingatia utaratibu wa rufaa katika vituo vya afya vilivyoingia mkataba na Skimu za Bima ya Afya,” ameongeza Mchengerwa.
Bima ya afya kwa wote ni miongoni mwa mipango iliyokosolewa vikali wadau wa sekta ya afya na baadhi ya wananchi katika mitandao ya kijamii tangu kuwasilishwa kwa mswada wa kwanza wa sheria hiyo bungeni Dodoma Septemba 23,2022.
Tangu mwaka huo mswada huo umekuwa ukikumbana na viunzi vilivyosababisha kushindwa kutekelezeka hata baada ya Bunge kupitisha rasmi Novemba 1, 2023 na kufanyiwa maboresho Februari 12, 2025.
Hata hivyo, Novemba 14, 2025 Rais Samia Suluhu Hassan aliyekuwa akihutubia Bunge kwa mara ya kwanza aliahidi kutekelezwa kwa hatua za awali za mpango huo katika siku 100 za uongozi wake wa awamu ya pili.
Hata kabla ya siku hizo kuisha tayari Watanzania wameanza kuona mwelekeo chanya unaoashiria mwanzo mpya wa huduma bora za afya nchini.
Mifumo ya Tehama kusomana
Mchengerwa Ameongeza kuwa Serikali inaendelea kuimarisha mifumo ya Tehama ili kuweka kumbukumbu za wagonjwa katika vituo vyote vya afya nchini, hatua itakayosaidia kuondoa urudiaji wa vipimo na kupunguza usumbufu kwa wagonjwa pamoja na mzigo kwa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF).
“Mwananchi hapaswi kubaki nje ya mfumo kwa sababu ya urasimu au uzembe wa mifumo. Pale mifumo ilipo na mtu hajasajiliwa, hilo ni tatizo la uongozi,” amesisitiza Waziri.
Naye Mganga Mkuu wa Serikali Dk Grace Magembe, amesema utekelezaji wa Bima ya Afya kwa Wote utahakikisha upatikanaji wa huduma za afya, kurahisisha uwezo wa kugharamia huduma hizo na kuboresha ubora wa huduma nchini.
Latest