Mwigulu azindua kituo cha uokoaji Mwanza, asisitiza uwajibikaji

January 23, 2026 6:17 pm · Kelvin Makwinya
Share
Tweet
Copy Link
  • Kituo hicho kitaendeshwa kwa saa 24 ili kuhakikisha usalama wa wananchi na wasafiri wanaotumia Ziwa Victoria unalindwa wakati wote.

Dar es Salaam. Waziri Mkuu wa Tanzania Dk Mwigulu Nchemba amewaagiza watendaji wa kituo cha kisasa cha utafutaji na uokoaji majini kilichopo Jijini Mwanza kutumia vizuri kituo hicho kuokoa maisha ya Watanzania wanaotumia Ziwa Victoria.

Dk Nchemba ametoa maagizo hayo leo Januari 23, 2026 baada ya kutembelea kituo hicho jijini Mwanza akisisitiza kuwa uzembe wowote utakaotokea wakati wa uokoaji inapotokea ajali ziwani wahusika watachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria.

“Huduma za uokozi ni kazi ya kuokoa maisha, hivyo hakuna uvumilivu kwa uzembe, kuchelewesha utoaji wa huduma za msaada pindi inapohitajika,” amesisitiza Dk Mwigulu.

Kituo hicho ambacho ni cha kwanza nchini kimejengwa kutokana na changamoto za ajali majini zilizokuwa zikijitokeza katika Ziwa Victoria, ambapo takriban watu 20 wamepoteza maisha katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita.

Miongoni mwa ajali hizo zilizosababisha upotevu wa maisha ya Watanzania ni ajali ya ndege kampuni ya Precision Air iliyotokea Novemba 6, 2022 na kusababisha vifo vya watu 19 na majeruhi 26.

Dk Mwigulu amefafanua kuwa licha umuhimu wa kituo hicho kilichotumia Sh19.8 bilioni kukamilika, ujenzi wake ulisimama kwa miaka miwili kati ya mwaka 2018 hadi 2020 baada ya wahisani kujiondoa.

Aidha, Dk Mwigulu ameagiza kituo hicho kuendeshwa kwa saa 24 ili kuhakikisha usalama wa wananchi na wasafiri wanaotumia Ziwa Victoria unalindwa wakati wote.

“Ikitokea mtu akapigiwa simu ya dharura, ikatokea amesinzia, mtu wa aina hiyo mheshimiwa Waziri wala usimuamishe kituo fukuza kabisa…kwa sababu hii ni kazi inayotaka mtu azingatie na atoe msaada kwa wakati ule msaada unaotakiwa,” amesisitiza Dk Mwiguru.

Kwa upande wake Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa amesema mbali na makao makuu ya kituo hicho kuwa jijini Mwanza, Serikali imejenga vituo vingine vitatu Musoma, Ukerewe na eneo lingine la Ziwa Victoria ili kuhakikisha usalama wa watumiaji majini.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Follow Us on TikTok

Subscribe to Our YouTube Channel

Subscribe

Loading videos...

Loading videos...

Loading videos...

Enable Notifications OK No thanks