Edwin Mtei: Mwasisi wa BoT, Chadema anayekumbukwa kwa mengi

January 23, 2026 3:53 pm · Fatuma Hussein
Share
Tweet
Copy Link
  • Ni Gavana wa kwanza wa BoT na mwanzilishi kuandaa sheria ya benki hiyo.
  • Kigogo mwanzilishi wa Chadema iliyochochea vuguvugu la mabadiliko ya kidemokrasia Tanzania. 

Dar es Salaam. Huwezi kuisimulia historia ya Tanzania kikamilifu bila kulitaja jina la Edwin Mtei, mmoja ya watu mashuhuri nchini waliofanya mageuzi makubwa katika sekta ya fedha na uchumi.

Historia ya kiongozi huyo mashuhuri nchini Tanzania inaacha alama isiyofutika katika harakati za demokrasia ya vyama vingi kutokana na msimamo na kujitoa kwake.

Licha ya historia yake pana iliyodumu kwa zaidi ya miongo tisa, January 20, 2026 nyota ya kiongozi huyo ilizima na kuhitimisha safari ya maisha yake duniani iliyodumu kwa miaka 94. 

Hata hivyo, huenda wengi husasan Gen-Z wakawa wanajiuliza Mtei ni nani?

Kama wewe ni miongoni mwa watu waliomsikia Mtei hivi karibuni basi ondoa shaka, Nukta Habari tumekuandalia historia ya maisha ya kiongozi huyu ambayo yataendelea kuwa somo kwa vizazi vya sasa na vijavyo.

Picha ya awali ya Edwin Mtei aliyoipata kutoka katika nyaraka zake iliyopigwa mwaka 1946. Picha/From Goat Herd to Governor.

Kuzaliwa na maisha ya awali

Mtei, aliyezaliwa Julai 12, 1932 anasimulia katika kitabu chake kiitwacho ‘From Goat Herd to Governor’ (Kutoka uchungaji wa mbuzi hadi ugavana) kuwa kabla ya kuzaliwa kwake, mama yake mzazi Ngianaeli Ngekalio Mtei alikuwa shambani Rawuya, takribani kilomita nane kutoka Marangu ya kati, akivuna maharagwe na mahindi licha ya kuwa na ujauzito mkubwa.

Akiwa shambani, Mtei anasimulia kuwa mama huyo alishikwa na uchungu wa kujifungua na hapo ndipo Mtei alipozaliwa shambani.

Kitu ambacho mama huyo hakufahamu ni kwamba mtoto aliyejifungua angekuja kuchangia maendeleo makubwa kiuchumi na kisiasa nchini. 

Katika kitabu hicho, Mtei alikiri kuwa mazingira ya utoto wake katika Tanganyika ya kikoloni ya miaka ya 1930 na 1940 yalimjenga kuwa mvumilivu, mnyenyekevu na mwenye nidhamu kali.

Wakati anaishi na mama yake katika nyumba ya nyasi, Mtei alijishughulisha na kuchunga mbuzi pamoja na rafiki yake wa utotoni Elimo Njau.

Mwaka 1941, anasema alijiandikisha katika shule ya awali ya Kanisa la Kilutheri Ngaruma akiwa na umri wa miaka minane na miezi sita na kufikia mwisho wa mwaka huo alikuwa tayari anajua kusoma Kiswahili.

Alipenda sana somo la hesabu, na mara kwa mara alikuwa akihesabu migomba na miti ya kahawa shambani, jambo lililowafanya baadhi ya majirani kudhani alikuwa na matatizo ya akili. 

Enzi za uhai wa Hayati Edwin Mtei akiwa shambani kwake Tengeru Arusha.Picha/The Tanzania times.

Bingwa wa mijadala, Kiingereza

Kipaji chake kilianza kuonekana wazi alipokuwa Shule ya Msingi Marangu, na mwaka 1945 alifanya vizuri zaidi katika Mkoa wa Kaskazini na kuchaguliwa kujiunga na Shule ya Sekondari Old Moshi.

Baadaye, Januari 1951, alijiunga na Shule ya Sekondari ‘Tabora Boys’, ambako kwa miaka miwili mfululizo alishika nafasi ya kwanza darasani. 

Katika safari hiyo ya masomo, alitambulika kama bingwa wa mijadala na mtumiaji mahiri wa lugha ya Kiingereza.

Mwaka 1955, Mtei alijiunga na Chuo Kikuu cha Makerere nchini Uganda kusomea Shahada ya Sanaa, akichukua masomo ya Sayansi ya Siasa, Historia na Jiografia.

Baada ya kuhitimu masomo mwaka 1957, Mtei aliwasili kwa mara ya kwanza jijini Dar es Salaam, tayari kushiriki katika ujenzi wa Taifa lililokuwa likielekea kupata uhuru.

Katika kazi zake za awali Mtei alifanya kazi katika Kampuni ya Tumbaku ya Afrika Mashariki (EATC) kabla ya kujiunga na utumishi wa umma. 

Safari ya kuanzisha BoT

Februari 9, 1959, alipata nafasi ya kuwa mtumishi kamili katika Ofisi ya Katibu Mkuu wa Serikali. 

Akiwa ndani ya utumishi, Mtei, alipanda vyeo kwa haraka na kujikuta akitoka taasisi moja kwenda nyingine.  

Mwaka 1964 aliteuliwa kuwa Katibu Hazina kabla ya miezi michache kuteuliwa tena 𝗄𝗎𝗐𝖺 𝗄𝖺𝗍𝗂𝖻𝗎 𝗐𝖺 𝖶𝗂𝗓𝖺𝗋𝖺 𝗒𝖺 𝖿𝖾𝖽𝗁𝖺 akisimamia kikamilifu ujenzi wa 𝖡𝖾𝗇𝗄𝗂 K𝗎𝗎 𝗒𝖺 𝖳𝖺𝗇𝗓𝖺𝗇𝗂𝖺 (BoT).

Kana kwamba alikuwa anajijengea ofisi yake, mwaka 1966, aliandika historia kwa kuteuliwa kuwa Gavana wa kwanza wa BoT, nafasi aliyohudumu hadi mwaka 1974.

Hayati Edwin Mtei akiwa ofisni kwake kwenye jengo la BoT Julai 1969. Picha/From Goat Herd to Governor.

 Akiwa Gavana, alisimamia kuandaliwa kwa sheria ya Benki Kuu, kuajiri na kutoa mafunzo kwa watumishi, pamoja na kuanzishwa kwa sarafu ya kwanza ya Tanzania (Shilingi), baada ya kuvunjika kwa mfumo wa sarafu ya Afrika Mashariki. 

“Mimi ndiye niliyetayarisha ‘memorandum’ (waraka) ya kuanzisha, hotuba, na muswada wa sheria ya benki kuu,” alisema Mtei kwenye moja ya makala za BoT.

Alitambulika kama mbunifu mkuu wa mfumo wa BoT na mlinzi wa uthabiti wa Shilingi ya Tanzania iliyoingia Tanganyika Machi, 1966 na kutambulishwa rasmi Juni 14 mwaka huo huo.

Migongano ya kisiasa na kujiuzulu

Licha ya mchango wake mkubwa, Mtei aliingia katika mvutano wa kisera na aliyekuwa Rais wa Kwanza wa Tanzania, Mwalimu Julius Nyerere, hususan kuhusu sera za Mfuko wa Kimataifa wa Fedha (IMF). 

Akiwa Waziri wa Fedha na Mipango kuanzia mwaka 1977, Mtei katika kitabu chake anaeleza kuwa alipendekeza Serikali ikubali masharti ya IMF, ikiwemo kushusha thamani ya Shilingi ya Tanzania, ili kuimarisha uchumi, pendekezo ambalo halikukubaliwa na Nyerere.

Chanzo kingine cha mvutano huo kilitokana na hali ya kutorejeshwa kwa mikopo ya benki, jambo lililofikia kiwango cha kutia wasiwasi na kuhatarisha uhai wa taasisi za kifedha. 

Katika kitabu chake, Mtei anaeleza kuwa alimteua mtaalamu kutoka Denmark kufanya utafiti uliofichua matumizi mabaya ya rasilimali, yaliyohusisha maofisa na madereva wasio waaminifu, hali iliyovumiliwa na baadhi ya mameneja wenye maslahi binafsi.

Mapendekezo ya kuchukua hatua yalionekana kuwa mwiko kutokana na umiliki wa serikali wa taasisi husika. 

Makatibu wakuu wa Kiafrika wa Rais Nyerere, Desemba 1964. Kuanzia kushoto kwenda kulia mstari wa nyuma: P. A. Sozigwa, E. I. M. Mtei, D. Nkembo, C. D. Msuya, G. Rugarabamu, G. Nhigula, B. Mulokozi, L. Mwajasho, B. Maggidi.
Mstari wa mbele: Bhoke Munanka, C. Mtawali, C. Kallaghe, J. Namata, Rais, F. Burengelo, O. Mwambungu, M. C. Othman. Picha/From Goat Herd to Governor.

Msimamo huo mgumu ulisababisha tofauti kubwa za kimtazamo kuhusu mwelekeo wa sera za uchumi.

Mtei anaeleza kuwa baada ya tofauti hizo alivyomaliza kutoa maoni yake kwenye kikao alichoitwa na Raisi arirudi ofisini kwake akaandika barua ya kuacha kazi kwa mkono na kwenda kumkabidhi mwenyewe Rais.

Hata hivyo, akiwa anatoka katika jengo la ofisi yake alikutana na Batoa Katibu wa Rais aliyemkabidhi barua aliyotakiwa kukabidhiwa mwenyewe. 

Alipokea barua kutoka kwa Rais kisha akaiweka kwenye kiti cha pembeni ya gari alokuwa akiendesha na baada ya hapo akawasha gari na kuelekea moja kwa moja kwa Rais ambaye hakutarajia kumuona kwa muda ule maana walikuwa wamemaliza kikao.

Baada ya hapo alimkabidhi barua ambayo Mtei akusubiri iandikwe na katibu wake na baada ya Rais kuisoma barua ile alimuagiza Katibu wake wa Habari, Paul Sozigwa, aitwe ofisini. 

Baada ya Sozigwa kufika Nyerere alimweleza kuwa Mtei amewasilisha barua ya kujiuzulu wadhifa wa Waziri wa Fedha na Mipango, na kwamba ameikubali mara moja.

Baada ya kujiuzulu mwaka 1979 anasema walipeana mkono na Nyerere na kisha kurejea nyumbani kwake Tengeru, Arusha.

Mchango katika siasa za vyama Vingi

Baada ya kurejea kwa mfumo wa vyama vingi mwaka 1992,  Mtei alikuwa miongoni mwa waaanzilishi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na kuwa Mwenyekiti wake wa kwanza.

Aliwasilisha Katiba ya chama hicho kwa Mwalimu Nyerere, ambaye aliisifu kama katiba bora ya chama cha siasa nchini.

Akiwa mmoja wa waasisi 12 wa chama hicho, alibaki kuwa muongoza njia na alama ya misingi ya demokrasia, uwajibikaji na siasa za hoja. 

Ingawa hakufanikiwa katika uchaguzi wa ubunge wa Arusha Mjini mwaka 1995, mchango wake katika kujenga misingi ya upinzani wa kisiasa nchini unabaki kuwa wa kihistoria.

Mwisho wa Safari

Mbali na siasa na utumishi wa umma, Mtei alikuwa mkulima, mfugaji na mfanyabiashara, akiendesha shamba la kahawa la Ogaden Estate, Tengeru. 

Mwaka 2009, alichapisha kitabu alichokiita ‘From Goat Herd to Governor’ (Kutoka uchungaji wa mbuzi hadi ugavana), ukielezea kwa kina safari ya maisha yake.

Mtei alifariki dunia Januari 19, 2026, akiwa na umri wa miaka 94, akiwa njiani kuelekea Hospitali ya Seliani mkoani Arusha. 

Kifo chake kimeacha simanzi kubwa kitaifa, huku Rais Samia Suluhu Hassan akimtaja kama kiongozi aliyeacha alama isiyofutika katika maandiko na ujenzi wa taifa. Ili kumuenzi kiongozi huyo, Chadema walitangaza maombolezo na siku 7 na kutangaza kujenga chuo kitakachoezi mchango wake katika ukuaji wa demokrasia nchini.

Safari ya Mtei inatarajiwa kuhitimishwa Januari 24, 2026, atakapozikwa nyumbani kwake Tengeru jijini Arusha.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Follow Us on TikTok

Subscribe to Our YouTube Channel

Subscribe

Loading videos...

Loading videos...

Loading videos...

Enable Notifications OK No thanks