Fursa, EU ikiiondoa Tanzania katika orodha ya nchi hatarishi kifedha
- Uamuzi huo unatarajia kufungua fursa za uwekezaji na kukuza uchumi.
Dar es Salaam. Umoja wa Ulaya (EU) umeiondoa rasmi Tanzania kwenye orodha ya nchi hatarishi kifedha jambo litakalorahisisha biashara na kufungua fursa za uwekezaji baina ya Tanzania na nchi zinazounda umoja huo.
Naibu Waziri wa Fedha, Laurent Luswetula, aliyekuwa akizungumza leo Januari 21, 2025 jijini Tanga, amesema mafanikio haya yanatokana na juhudi kubwa za Tanzania kuimarisha na kudhibiti mifumo yake ya kifedha.
“Mafanikio haya yanatokana na jitihada kubwa za Tanzania kuimarisha utakatishaji fedha na ufadhili wa ujangili, amesema Luswetula katika uzinduzi wa maadhimisho ya tano ya wiki ya huduma za fedha kitaifa mwaka 2026.
EU na taasisi nyingine za kifedha hutoa orodha ya nchi zenye hatari ya kifedha (high risk countries) ili kulinda mfumo wa kifedha wa kimataifa.
Nchi huwekwa kwenye orodha hii ikiwa zina udhibiti dhaifu wa kifedha, uwazi mdogo wa taarifa za kifedha, kiwango kikubwa cha ufisadi au utapeli, utoaji wa mikopo isiyo endelevu, au kushindwa kufuata viwango vya kimataifa kama AML/CFT.
Desemba 5, 2025 EU ilitangaza rasmi kuiondoa Tanzania na nchi nyingine za Afrika ikiwemo Mali, Nigeria, Msumbiji, Afrika Kusini na Burkina Faso baada ya utekelezaji wa marekebisho makubwa ya mifumo yao ya kifedha.
Ni fursa kwa Tanzania
Naibu Waziri Luswetula aliyekuwa akimuwakilisha Waziri wa Fedha, amesema kuwa uamuzi huo wa EU ni fursa kwa Tanzania kuimarisha uchumi wake na biashara katika nchi zinazounda umoja huo.
“Kutokana na hatua hiyo biashara na miamala ya kifedha kati ya Tanzania na nchi za ulaya itakuwa rahisi, haraka na yenye gharama nafuu ifikapo Januari 29, 2026,” amesema Luswetula.
Aidha, Luswetula amebainisha kuwa hatua hiyo itafungua hatua mpya za uwekezaji na kufungua milango ya uwekezaji ikitazamia kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha biashara Afrika.
Huenda umuamuzi huo wa EU ukaongeza mapato yatokanayo na uuzwaji wa bidhaa katika nchi za umoja huo kutoka Sh3.5 bilioni ( Euro 1,195) zilizorekodiwa kwa mwaka 2024 kwa mujibu wa tovuti rasmi ya EU.
Latest