Matokeo ya uchaguzi wa Rais Uganda kujulikana Januari 17
- Jumla ya wapiga kura milioni 21.6 walisajiliwa kupiga kura kuchagua viongozi watakao waongoza akiwemo Rais wa nchi hiyo.
Dar es Salaam. Matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa Uganda yanatarajiwa kutangazwa rasmi Jumamosi, Januari 17, 2026, baada ya ukamilika kwa zoezi la upigaji kura jana Januari 15,2026.
Kwa mujibu wa Tume ya Uchaguzi Uganda, jumla ya wapiga kura milioni 21.6 walisajiliwa kupiga kura kuchagua viongozi watakao waongoza kwa kipindi cha miaka mitano ikiwemo Rais wa Taifa hilo.
Kampeni za uchaguzi nchini Uganda zilianza rasmi Septemba 29,2025 kabla ya kutamatika Januari 13, 2026 siku mbili kabla ya tarehe rasmi ya kupiga kura ambapo jumla ya vyama 13 vya siasa vimeshiri katika kampeni hizo vikinadi sera zao.
Katika uchaguzi huo vyama 12 vya upinzani vinachuana vikali na chama tawala cha National Resistance Movement (NRM), ambacho kimemsimamisha Rais Yoweri Museveni (81) kuendelea kutetea kiti cha urais kwa miongo minne mfululizo tangu mwaka 1986.
Museveni anawania muhula wa saba wa uongozi wa nchi hiyo, kufuatia marekebisho ya kikatiba yaliyoondoa vizingiti vya umri na muda wa uongozi.
Mpinzani mkuu wa Museven katika uchaguzi huu ni Robert Kyagulanyi Ssentamu, maarufu kama Bobi Wine kutoka Chama cha National Unity Platform (NUP), chama ambacho kimepata umaarufu mkubwa hasa kwa vijana na wakazi wa mijini kutokana na sera zake zinazolenga kupambana na ufisadi na kuboresha ajira kwa vijana.
Bobi Wine anashiriki uchaguzi huo kwa mara ya pili akichuana Museveni tangu walipokutana kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka 2021 wa nchi hiyo ambapo alizidiwa kete na Museveni.
Hata hivyo, licha ya kijana huyo mwenye umri wa miaka 43 kuonyesha upinzani mkubwa kwa Museveni na kukubalika kwa watu, vyombo mbalimbali vya habari nchini humo pamoja na vile vya kimataifa vimeripoti kuwepo kwa vikwazo vikali vya kiusalama, ukamatwaji wa wafuasi wake, na mashambulio ya nguvu za usalama kwenye baadhi ya mikutano ya kampeni zake katika uchaguzi huu, jambo ambalo limeongeza wasiwasi juu ya uhuru na demokrasia kwa wapinzani nchini humo.
Uchaguzi gizani
Licha ya vyombo vya habari nchini Uganda kuripoti kutamatika kwa zoezi la upigaji kura kwa amani jana Januari 15, 2026, baadhi ya vyombo vya habari vya kimataifa viliripoti uchaguzi huo kufanyika gizani.
Serikali ya nchi hiyo ilizima huduma ya interneti na kufunga mawasiliano ya simu za kimataifa mapema Januari 13, 2026 siku mbili kabla ya zoezi la kupiga kura kufanyika.
Hata hivyo, Mamlaka ya Mawasiliano nchini humo (UCC) ilieleza hatua hiyo ililenga kupunguza uenezi wa habari za uongo na kuwazuia wahamasishaji wa vurugu kutumia mtandao kusababisha ghasia.
Kwa sasa wananchi wa Uganda wanasubiri kutangazwa kwa mshindi ambaye ataongoza jahazi la Serikali ya nchi hiyo mpaka mwaka 2031.
Iwapo Museveni atashinda, atendelea kuliongoza taifa hilo kwa miaka mitano zaidi, akiingia katika muhula wake wa saba, na kufanya kuwa na jumla ya takriban miaka 45 madarakani tangu alipoingia ofisini mwaka 1986.
Na iwapo Bobi Wine atashinda, itakuwa ni mara ya kwanza upinzani kushinda nafasi ya urais wa Uganda tangu kupatikana kwa uhuru wa nchi hiyo mwaka 1962.
Latest