Panda shuka za Paul Makonda katika siasa

January 9, 2026 4:55 pm · Kelvin Makwinya
Share
Tweet
Copy Link
  • Safari yake ya kisiasa ilianzia kupitia UVCCM ambapo alijifunza misingi ya siasa za chama, mbinu za uhamasishaji na uongozi wa vijana. 

Dar es Salaam. Uongozi ni safari ndefu yenye milima na mabonde inayoweza kumpandisha au kumshusha yoyote katika nyadhifa fulani kutokana na mabadiliko ya kisiasa au maamuzi ya wenye mamlaka katika nchi.

Muktadha huo umejidhihirisha katika safari ya mwanasiasa machachari Paul Makonda, ambaye jina lake limewahi kutokea katika nyadhifa za juu Serikalini na katika Chama cha Mapinduzi (CCM).

Januari 8 mwaka huu jina na Paul Makonda limetokea katika uteuzi aliofanya Rais Samia Suluhu Hassan na kumpandisha hadhi kuwa  Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kutoka kuwa naibu waziri wa wizara hiyo kwa takribani siku 53 pekee.

Safari ya Makonda kisiasa

Makonda alianza safari yake ya kisiasa kupitia Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM). Hapa ndipo alipojifunza misingi ya siasa za chama, mbinu za uhamasishaji na uongozi wa vijana. 

Kiongozi huyo alijijengea umaarufu kama kijana mwenye uwezo wa kuzungumza, kupanga hoja na kushawishi wenzake, jambo lililomfanya atambulike mapema ndani ya CCM.

Hatua kubwa zaidi katika safari yake ya kisiasa ilikuja mwaka 2016, alipoteuliwa na Rais wa awamu ya tano wa Tanzania, Hayati John Pombe Magufuli, kuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam. 

Makonda alipata umaarufu mkubwa alipoteuliwa na Rais wa awamu ya tano wa Tanzania, Hayati John Pombe Magufuli, kuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam. Picha | Bongo5

Akiwa RC wa jiji hilo lenye heka heka na mishe za kila namna Makonda alijijengea sifa ya uwajibikaji, na utatuzi wa kero na changamoto za wananchi licha ya kubezwa na kukosolewa vikali na baadhi ya wadau. 

Makonda alihudumu katika nafasi hiyo kwa mwaka na miezi mitatu hadi Julai 15, 2020 baada ya kutangaza nia ya kuwania ubunge wa jimbo la Kigamboni kwa tiketi ya CCM. 

Kukaimu nafasi hiyo, Hayati Rais Magufuli alimteua Abubakar Kunenge kuchukua nafasi yake ili kumruhusu Makonda kujiingiza katika kinyanganyiro hicho cha ubunge.

Hata hivyo, Bahati haikuwa upande wake, Makonda aliangukia pua katika kura za ndani za maoni za chama (primaries) na kushindwa kuendelea na hatua nyingine za uchaguzi.

Kushindwa uchaguzi huo kulimuweka nje ya ulingo wa siasa kwa miaka mitatu, hatua ambayo baadhi ya wadau waliitafsiri kama kushindwa au kupotea kabisa katika ulimwengu wa siasa.

Jina la Makonda liliibuka tena katika vyombo habari na ulimwengu wa siasa Oktoba 22, 2023 alipoteulia kuwa Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM.

Rais Samia Suluhu Hassan amempandisha hadhi Makonda kuwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kutoka kuwa naibu waziri wa wizara hiyo kwa takribani siku 53 pekee. Picha | Mwananchi.

Katika nafasi hii, Makonda alifanya ziara za kikazi mikoa mbalimbali nchini, akikemea na kuwawajibisha viongozi wazembe pamoja na kutatua  kero za wananchi papo hapo hatua iliyomfanya kujizolea umaarufu kisiasa.

Hata hivyo, Makonda alihudumu nafasi hiyo kwa miezi mitano pekee kabla ya Rais Samia kumteuwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha Machi 31, 2024. 

Kama Mkuu wa Mkoa, Rais Samia alimuagiza kuimarisha maendeleo ya mkoa wa Arusha, kuboresha huduma za utalii, na kusimamia miradi ya miundombinu.

Juni 24, 2025, Rais Samia alimuondoa Makonda katika nafasi ya ukuu wa mkoa Arusha, ili kumpa nafasi ya kutia nia katika kinyanganyiro cha kuliwakilisha jimbo la Arusha Mjini bungeni.

Tofauti na mwaka 2020 safari hii Makonda alishinda kwa kishindo katika kura za ndani za maoni za chama hicho kwa kura za maoni 9,056 sawa na asilimia 97.6 ya kura zote zilizopigwa akiwatupa mbali wapinzani wake. 

Hata baada ya kumalizika  kwa kampeni na kuingia katika uchaguzi mkuu Oktoba 29, 2025, Makonda alishinda kwa kishindo ubunge wa jimbo hilo hatua iliyomrudisha bungeni kwa mara nyingine tena.

Alipofika bungeni nyota yake iling’aa tena na kuteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Novemba 17 mwaka jana.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Follow Us on TikTok

Subscribe to Our YouTube Channel

Subscribe

Loading videos...

Loading videos...

Loading videos...

Enable Notifications OK No thanks