Idadi ya watu Zanzibar kuongezeka hadi milioni 2.16 mwaka 2026
- Inaratajia kuongezeka kwa 14.3% kutoka milioni 1.88 iliyorekodiwa katika Sensa ya Watu na Makazi ya 2022.
- Wastani wa umri wa kuishi Wazanzibar utakua miaka miaka 69.
- Vijana kutawala nguvu kazi visiwani humo.
Dar es Salaam. Idadi ya watu Zanzibar inatarajia kuongezeka kwa asilimia 14.3 hadi kufikia milioni 2.16 ifikapo mwaka 2026 huku wastani wa umri wa kuishi ukiongezeka kidogo hadi miaka 69.
Makadirio ya idadi ya watu wa Zanzibar kwa mwaka 2026 yaliyotolewa na Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali Zanzibar (OCGS) leo Disemba 30, 2025 visiwani humo wastani wa ongezeko la idadi ya watu kwa mwaka ni asilimia 3.7.
Kwa mujibu wa makadirio hayo, kwa mwaka 2026, idadi ya watu wa Zanzibar itafikia milioni 2.16 ikiongezeka kwa asilimia 14.3 kutoka milioni 1.88 iliyorekodiwa katika Sensa ya Watu na Makazi ya 2022.
Kati ya idadi hiyo, wanaume watakuwa milioni 1.05 (48.6%) na milioni 1.10 ni wanawake/
Idadi ya wanawake wenye umri wa kuzaa (miaka 15 hadi 49) inakadiriwa kuwa 547,224 ambapo wastani wa umri wa kujifungua utakua miaka 29. Kwa makadirio hayo, kwa wastani, mwanamke mmoja visiwani humo anatarajia kupata watoto wanne.
“ Katika kupanga maendeleo ya Serikali, taasisi na wizara ni muhimu kutumia takwimu za idadi ya watu, tunafurahi zaidi pale makadirio ya watu ambayo yanatolewa ndiyo takwimu hizo zitumike kwa mwaka husika,” amesema Mtakwimu Mkuu wa Serikali Zanzibar (OCGS) Salum Kassim Ali.
Umri wa kuishi waongezeka kiduchu
OCGS katika takwimu zake ilizowasilisha leo, imeeleza kuwa wastani wa umri wa kuishi kwa watu wa Zanzibar utaongezeka hadi miaka 69 mwaka ujao kutoka miaka 68.9 ya sasa.
Wazee waliofikia umri wa miaka 70 na zaidi wanataraji kuwa 37,726 sawa na asilimia 1.74 ya watu wote milioni 2.16 watakaokuwepo mwakani. Hiyo ni sawa kusema takriban watu wawili kati ya 100 ndio watafikisha umri wa miaka 70 na zaidi.
Vijana kutawala nguvu kazi Taifa
Uchambuzi wa makadirio hayo uliofanywa na Nukta Habari (nukta.co.tz) yanaonyesha Zanzibar itakuwa na nguvu kazi ya watu milioni 1.20 wenye umri wa miaka 15 hadi 64, jambo linaloashiria rasilimali kubwa ya watu wenye uwezo wa kufanya kazi.
Kati yao, vijana wa miaka 15 hadi 24 ni 414,922, sawa na takribani asilimia 35 ya nguvu kazi yote, hali inayoonyesha kundi kubwa la wanaoingia au wanaotarajiwa kuingia katika soko la ajira kwa mara ya kwanza.
Zaidi ya hapo, vijana wenye umri wa miaka 15 hadi 35 wanakadiriwa kuwa 771,404. Hii inaonyesha Zanzibar ina idadi kubwa ya vijana, hivyo uwekezaji katika elimu, ujuzi, ajira na ujasiriamali ni muhimu ili kunufaika na rasilimali hii ya kidemografia.
Watu 102,065 wanatarajiwa kufikia umri wa kustaafu (miaka 60), sawa na takribani asilimia 8.5 ya nguvu kazi. Hii inaashiria nafasi za ajira zitakazofunguka, lakini pia inaweka shinikizo la maandalizi ya kizazi kipya kuchukua nafasi hizo kupitia mafunzo na uendelezaji wa ujuzi.
Makadirio haya yanatoa msingi muhimu kwa Serikali na wadau wa maendeleo katika kupanga sera na mipango ya huduma za jamii, afya, elimu, ajira na mipango ya maendeleo endelevu, huku wakizingatia ongezeko la idadi ya watu na mabadiliko ya idadi ya watu visiwani humo.
Latest