Mwigulu alaani vitendo vvya uvunjifu wa amani

December 5, 2025 6:35 pm · Fatuma Hussein
Share
Tweet
Copy Link
  • Aonya wananchi dhidi ya wachochezi awataka kulinda amani ya Tanzania.

Dar es Salaam. Waziri Mkuu wa Tanzania, Dk Mwigulu Nchemba, amesema Serikali haitavumilia tena matukio ya uvunjifu wa amani kama yaliyojitokeza Oktoba 29, 2025, akisisitiza kuwa Tanzania itaendelea kuwa nchi ya utulivu na mshikamano.

Dk Mwigulu aliyekuwa akizungumza leo Disemba 5, 2025, mara baada ya kukagua ofisi ya Mtendaji wa Kata ya Kisesa jijini Mwanza  iliyochomwa moto Oktoba 29, 2025 amesema Serikali imejipanga kuchukua hatua kali dhidi ya wanaochochea vitendo vya uvunjifu wa amani.

“Tuna nchi nzuri inaitwa Tanzania, tuilinde. Tusimpe adui mwanya kupitia mavuguvugu haya….; sisi hatutaruhusu vuguvugu wala vurugu. Anayetaka fujo asimtangulize mtoto wa mtu, aende yeye mwenyewe,” alisema Mwigulu.

Aidha, Mwigulu ameonya vijana kufuata mkumbo akiwataka kutokubali kutumiwa kuchoma mali za wananchi au kusababisha uharibifu huku wahusika wakuu wakibaki mafichoni.

Kwa upande wake, Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro, amewataka Watanzania kutoshabikia vurugu kwa kuwa zina gharama kubwa kiusalama na kiuchumi.

Muliro amesema Jeshi la Polisi linafahamu kuwa linawatumikia wananchi na jukumu lake ni kulinda amani hivyo amewataka wananchi kuzingatia sheria.

Ikumbukwe kuwa katika uchaguzi uliofanyika oktoba 29, 2025, nchini Tanzania kulitokea maandamano yaliopelekea uvunjifu wa amani na kusababisha maafa kwa watu ikiwemo kupoteza mali na maisha.

Hata hivyo, Novemba 18, 2025, Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan aliunda tume ya watu saba kuchunguza matukio ya uvunjifu wa amani yaliyotokea nchini wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu.

Pia, katika mkutano wake na wazee wa Dar es Salaam Desemba 2, 2025, alieleza kuwa matukio ya Oktoba 29 yalikuwa mradi mkubwa wenye nia ovu uliokuwa na wafadhili, washirika na watekelezaji waliodhamiria kuhujumu Serikali huku wengine wakifuata mkumbo.

Rais Samia alisisitiza kuwa kilichotokea si maandamano bali ni vurugu, kwa sababu maandamano ya kisheria ni lazima yawe na kibali, kueleza njia yatakayopita, na kulindwa na Polisi.

Naye, mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, amewataka wananchi kuiamini tume hiyo na kuipa muda kufanya kazi yake.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Follow Us on TikTok

Subscribe to Our YouTube Channel

Subscribe

Loading videos...

Loading videos...

Loading videos...

Enable Notifications OK No thanks