Balozi 16 za EU zalaani yaliyotokea Oktoba 29
- Zatoa wito kwa Serikali ya Tanzania kufanya uchunguzi huru, wa wazi na shirikishi.
Dar es Salaam. Balozi 16 kutoka Umoja wa Ulaya (EU) zimesikitishwa na ukiukwaji wa haki za binadamu uliotokea wakati na baada ya Uchaguzi mkuu wa Tanzania, Oktoba 29, 2025, na kutaka uchunguzi huru, wazi na shirikishi kufanyika.
Balozi hizo zinazojumuisha mataifa ya Uingereza, Canada, Norway, Uswisi, Ubelgiji, Denmark, Ufini, Ufaransa, Ujerumani, Ireland, Italia, Uholanzi, Poland, Slovakia, Hispania na Uswidi ambazo zimetoa tamko hilo leo Disemba 2, 2025 zikishinikiza haki na uwajibikaji.
Tamko kutoka balozi hizo linakuja ikiwa ni sikumoja tu tangu Serikali ya Marekani kutangaza kutathimini upya uhusiano baina yake na Tanzania, kutokana na ukandamizaji mkubwa wa haki za binadamu na ukatili dhidi ya raia unaofanywa kabla na baada ya uchaguzi wa Oktoba 29.
Hata hivyo, Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan Disemba 2, mwaka huu wakati alipokuwa akizungumza na wazee wa Jiji la Dar es Salaam alisema kuwa Tanzania ni nchi huru na haiwezi kupangiwa cha kufanya na mataifa mengine.
“Nje huko wanakaa Tanzania ifanye moja, ifanye mbili, ifanye tatu halafu ndio itakuwa hivi, ‘Who are you?” alihoji Rais Samia.
Licha ya ukosoaji huo kwa mataifa ya nje kuingilia masuala ya Tanzania, tayari Rais Samia alishaunda tume ya kuchunguza matukio hayo ya uvunjifu wa amani na vifo yaliyotokea kipindi hicho Novemba 20 mwaka huu
Tume hiyo inayoongozwa na Jaji Othman Chande itafanya kazi kwa miezi mitatu ikishirikisha Wananchi na wadau wengine kisha kuwasilisha ripoti kwa Rais Samia.
Katika tamko hilo la pamoja balozi hizo zimetoa wito kwa Tanzania kutimiza ahadi zake za kimataifa za kulinda haki za msingi, ikiwa ni pamoja na haki za kikatiba za kupata taarifa na uhuru wa kujieleza kwa Watanzania wote.
Aidha, mataifa hayo yamesema wamesikitishwa na vifo na majeruhi waliotokana na matukio ya wakati wa uchaguzi wakisistiza umuhimu wa vyombo vya ulinzi vya Tanzania kutekeleza majukumu yao kwa uangalifu mkubwa.
“Taarifa za kuaminika kutoka mashirika ya kitaifa na kimataifa zinaonesha ushahidi wa mauaji nje ya utaratibu wa kisheria, kupotea kwa watu, ukamataji kiholela na ufichaji wa miili ya waliopoteza maisha,” limesema tamko hilo.
Mbali na hayo, wametoa wito kwa Serikali ya Tanzania kukabidhi miili ya marehemu kwa familia zao, kuwaachia huru wafungwa wote wa kisiasa, na kuhakikisha waliokamatwa wanapata msaada wa kisheria na matibabu.
“Zaidi, tunatoa wito kwa serikali kushughulikia mapendekezo yaliyotolewa katika ripoti za awali za waangalizi wa uchaguzi wa AU na SADC ambazo ziliweka bayana mapungufu yaliyojiri wakati wa mchakato wa uchaguzi,” limesema tamko hilo.
Mabalozi hao pia wamesisitiza kwamba uchunguzi wowote utakaofanywa lazima uwe huru, wazi na shirikishi, ukijumuisha asasi za kiraia, taasisi za kidini, na wadau wote wa kisiasa.
Latest