Bei ya dizeli yapanda, petroli yashuka kidogo mwezi Disemba
- Petroli imeshuka kwa Sh3 kutoka Sh2,752 iliyokua ikitumika mwezi Novemba na dizeli imepanda kwa Sh75 kutoka Sh2,704 iliyotumika mwezi uliopita.
Dar es Salaam. Mwezi Desemba umeanza kwa kilio kwa watumiaji wa dizeli kutokana na kupanda kwa bidhaa hiyo huku kukiwa na afueni kiduchu kwa watumiaji wa petroli ambayo bei yake imepungua kidogo.
Taarifa iliyotolewa na Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji Tanzania (Ewura) Desemba 2, 2025 inabainisha kuwa bei ya rejareja ya petroli ni Sh2,749 kwa lita huku dizeli ikiuzwa kwa Sh2,779 kwa lita.
Kutokana na bei hizo, petroli imeshuka kwa Sh3 kutoka Sh2,752 iliyokuwa ikitumika mwezi Novemba na dizeli imepanda kwa Sh75 kutoka Sh2,704 iliyotumika mwezi uliopita.
Katika kipindi hiki cha msimu wa sikukuu ambacho watu wengi husafiri kwenda sehemu mbalimbali kwa ajili ya mapumziko au kufurahia pamoja na ndugu jamaa na marafiki, huenda kupungua kwa bei ya petroli kutaleta ahueni kiduchu kwa watumiaji wa nishati huku watumiaji wa dizeli wakilazimika kutoboa mifuko yao zaidi kutokana na kuongezeka la bei kwa nishati hiyo.
Licha ya kushuka kwa bei ya mafuta nchini Tanzania, Ewura inasema bei ya nishati hizo katika soko la dunia na gharama za uagizaji kupitia bandari za Dar es Salaam, Mtwara na Tanga zimeongezeka.
“Bei za bidhaa za mafuta ya petroli hapa nchini zinazingatia gharama za mafuta yaliyosafishwa (FOB) katika soko la nchi za Kiarabu. Katika bei kikomo kwa Desemba 2025, bei za mafuta katika soko la dunia zimeongezeka kwa asilimia 1.7 kwa petroli, asilimia 4.8 kwa dizeli na asilimia 6.4 kwa mafuta ya taa,” imesema taarifa ya EWURA.
Hata hivyo, gharama za kuagiza mafuta (premiums) katika Bandari ya Dar es Salaam zimepungua kwa wastani wa asilimia 2.4 kwa mafuta ya petroli na asilimia 3.6 kwa mafuta ya taa, na zimeongezeka kwa asilimia 3.5 kwa mafuta ya dizeli.
Kwa mujibu wa Ewura hakuna mabadiliko ya gharama hizo kwa Bandari ya Tanga na Mtwara.
Aidha, Ewura imeeleza kuwa wastani wa gharama za kubadilisha fedha za kigeni (Applicable Exchange Rate) kulipia Gharama za mafuta (FOB) na gharama za uagizaji (Premiums) ambazo hulipwa kwa kutumia fedha za kigeni ikiwemo Dola ya Marekani umeongezeka kwa asilimia 4.48.
Wakazi wa Kyerwa mkoani Kagera ndio wananunua mafuta kwa bei ya juu zaidi kuliko wote nchini, huko lita moja ya petroli ni Sh3,022 na dizeli Sh3,052.
Latest