Bei ya petroli Dizeli yashuka kwa mara ya pili mfululizo Tanzania
- Petroli yauzwa Sh2,752 na dizeli Sh2,704.
- Bei ya nishati hizo katika soko la dunia na gharama za uagizaji zapaa.
Arusha. Mwezi Oktoba umeanza kwa kicheko kwa watumiaji wa mafuta ya petroli na dizeli baada ya bei ya nishati hiyo kushuka kwa mara ya pili mfululizo.
Taarifa iliyotolewa na Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji Tanzania (Ewura) leo Oktoba1 , 2025 inabainisha kuwa bei ya rejareja ya petroli ni Sh 2,752 huku dizeli ikiuzwa kwa Sh2,704.
Kutokana na bei hizo, petroli imeshuka kwa Sh55 kutoka Sh2,807 iliyokua ikitumika mwezi Septemba na dizeli imeshuka kwa Sh50 kutoka Sh2,754 iliyotumika mwezi uliopita.
Ahueni hii inakuja ikiwa ni miezi miwili baada ya dizeli kupaa kiduchu kwa kwa Sh 10 hali iliyofanya watumiaji kutoboa mifuko yao kujipatia bidhaa hiyo.
Licha ya kushuka kwa bei ya mafuta nchini Tanzania, EWURA inasema bei ya nishati hizo katika soko la dunia na gharama za uagizaji kupitia bandari za Dar es Salaam, Mtwara na Tanga zimeongezeka.
“Bei za bidhaa za mafuta ya petroli hapa nchini zinazingatia gharama za mafuta yaliyosafishwa (FOB) katika soko la nchi za Kiarabu. Katika bei kikomo kwa Oktoba 2025, bei za mafuta katika soko la dunia zimeongezeka kwa asilimia 2.80 kwa mafuta ya petroli, asilimia 3.65 kwa mafuta ya dizeli na asilimia 3.57 kwa mafuta ya taa.” imesema taarifa ya EWURA.
Kwa upande wa gharama za uagizaji mafuta (premiums) katika Bandari ya Dar es Salaam zimepungua kwa wastani wa asilimia 1.95 kwa mafuta ya petroli, zimeongezeka kwa asilimia 2.39 kwa mafuta ya dizeli na hakuna mabadiliko kwa mafuta ya taa.
Katika Bandari ya Tanga zimeongezeka kwa asilimia 6.38 kwa mafuta ya petroli na dizeli na katika Bandari ya Mtwara zimeongezeka kwa asilimia 0.49 kwa mafuta ya petroli na hakuna mabadiliko kwa mafuta ya dizeli.
Latest



