Mwigulu: Kutangaza idadi ya vifo ni kutonesha vidonda vya Watanzania
- Asema kuwa ni sawa na kuimba wimbo wa waliokuwa na nia ya kutaka yaliyotokea yatokee.
Dar es Salaam. Waziri Mkuu wa Tanzania Dk Mwigulu Nchemba amesema Serikali haijaweka wazi idadi ya waliofariki kutokana na vurugu zilizotokea baada ya maandamano ya Oktoba 29 na siku zilizofuata kwa sababu kwa sasa Serikali bado inaendelea kurejesha hali ya umoja, ushirikiano na utengamano nchini.
Kwa mujibu wa Dk Mwigulu aliyekuwa akizungumza na wahariri pamoja na wanahabari leo Novemba 25, jijini Dar es Salaam, kutangaza idadi ya waliofariki kutatonesha vidonda kwa waathirika wa madhila yaliyojitokeza wakati na baada ya maandamano.
Akijibu swali lililoulizwa na Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Deogratius Balile lililohoji “ni watu wangapi walio uwawa au kufa?” kwenye tukio lililotokea, Dk Mwigulu amesema kutaja idadi ya watu waliofariki ni sawa na kusheherekea vifo hivyo, jambo ambalo linatweza utu na halijazoeleka katika miiko na tamaduni za Mtanzania.
Aidha, ameongeza kuwa, kwa kufanya hivyo ni sawa na kuimba wimbo wa waliokuwa na nia ya kuona vurugu zinatokea katika nchi ya Tanzania jambo aliloliambatanisha na kuhoji uhalali wa idadi ya vifo vinavyoripotiwa kwenye vyombo vya habari na mashirika ya kimataifa.
“Tunaongelea watu wamepoteza wapendwa wao, haya si majengo, ni nchi ya aina gani hiyo ya ku ‘celebrate’ maisha ya mtu… kwanini tusheherekee watu kupoteza maisha ?,” amehoji Dk Nchemba.
Hata hivyo, kauli ya Dk Nchemba inakuja siku moja tu tangu Msemaji Mkuu wa Serikali Gerson Msigwa kubainisha kuwa idadi ya watu waliopoteza maisha itafahamika baada ya Tume ya Kuchunguza Matukio yaliyotokea kukamilisha uchunguzi wake.
Aidha, hii si mara ya kwanza kwa Serikali ya Tanzania kuficha idadi ya vifo vilivyotokea kutokana na janga au changamoto fulani kama ilivyo sasa.
Mbali na hayo, Dk Nchemba amewasisitizia wanahabari na Watanzania kuendelea kuhubiri amani akitaadhalisha kuwa maendeleo na mabadiliko hayawezi kupatikana kwenye vurugu na kutoelewana.
“Tunakiri kwamba jambo limetokea ambalo limepoteza maisha ya watu… vurugu yeyote ikitokea lazima watu watapoteza maisha” ameongeza Dk Nchemba.
Latest