Nukta Africa yang’ara tuzo za hakimiliki Afrika
- Ni baada ya mwandishi wake wa habari Daniel Samson, kushinda nafasi ya pili katika tuzo za hakimiliki zinazotolewa na Shirika la Hakimiliki Kanda ya Afrika (ARIPO).
Accra, Ghana. Kampuni ya habari na teknolojia ya Nukta Africa imetambuliwa kimataifa baada ya mwandishi wake wa habari Daniel Samson, kushinda nafasi ya pili katika tuzo za hakimiliki zinazotolewa na Shirika la Hakimiliki Kanda ya Afrika (ARIPO).
Tuzo za ARIPO za Hakimiliki kwa Waandishi wa Habari (ARIPO IP Journalist Awards) zimetolewa wakati wa Mkutano wa 49 wa Baraza la Utawala la ARIPO jijini Accra, Ghana Novemba 19, 2025.
Ushindi wa Samson umeiweka Tanzania miongoni mwa nchi zilizofanya vizuri zaidi mwaka huu katika kutoa elimu ya hakimiliki na ubunifu Afrika.
Mshindi wa kwanza ni Lloyd Makonya kutoka Zimbabwe huku Dorcas Letuka kutoka Lesotho akishika nafasi ya tatu na kukamilisha orodha ya waandishi waliotambuliwa kwa mchango wao katika kuripoti habari za hakimiliki barani Afrika.
Samson amesema tuzo hiyo inaimarisha nafasi ya uandishi wa habari katika kuhamasisha ubunifu na kulinda kazi za wabunifu Tanzania.
“Nimepata heshima ya kipekee kupokea tuzo hii. Inaonyesha kwamba uandishi wa habari unaweza kuwasaidia Watanzania wengi zaidi kuelewa na kulinda ubunifu na biashara zao,” amesema Samson.
Samson ambaye pia ni Mkuu wa Mafunzo na Utafiti wa Nukta Africa amesema ushindi huo unaakisi namna taasisi za hakimiliki Tanzania zilivyojiimarisha katika kuweka mazingira wezeshi kwa wabunifu kulinda kazi na biashara zao.
“BRELA na COSOTA wanafanya kazi nzuri kuwaelimisha wabunifu na wajasiriamali kupitia elimu na huduma za kidijitali. Ni matumaini yangu kuwa mageuzi yataendelea ili kufanya usajili kuwa rahisi na kupatikana zaidi katika wakati huu wa ukuaji wa teknolojia ya akili unde,” amesema.

Mkuu wa Mafunzo wa Nukta Africa, Daniel Samson (Wa tatu kulia) akiwa na wajumbe wa Baraza la Utawala la ARIPO na washindi wengine wawili wa Tuzo za ARIPO za Hakimiliki kwa Waandishi wa Habari muda mfupi baada ya hafla ya kutoa tuzo hizo jijini Accra, Ghana, Novemba 19, 2025. Picha | ARIPO.
Makala zilizompa ushindi Samson ni ile inayoelezea umuhimu wa kampuni changa Tanzania kusajili chapa za bidhaa na huduma zao na mabadiliko ya sera na sheria za hakimiliki kujumuisha ubunifu unaotokana na akili unde.
Mkurugenzi Mkuu wa ARIPO, Bemanya Twebaze akizungumza katika utoaji wa tuzo hizo amewapongeza washindi wote na kusisitiza dhamira ya shirika hilo katika kuongeza uelewa wa hakimiliki barani Afrika.
Amesema waandishi wa habari wana nafasi muhimu katika kuwasaidia wananchi kuelewa thamani ya kulinda mawazo yao, jambo linalochochea ubunifu na ukuaji wa uchumi.
“Tunapowaadhimisha washindi wetu, tunatambua kwamba ninyi si wanahabari tu; ninyi ni waelimishaji, watetezi, na waboreshaji masuala ya jamii,” amesema Mkurugenzi Mkuu. “Kazi yenu ina mchango muhimu katika kusaidia umma kuelewa jinsi ulinzi wa hakimiliki unavyohusiana na ubunifu, ukuaji wa biashara, na sekta za ubunifu,” amesema Twebaze.

Tuzo za Waandishi wa Habari za ARIPO IP zilizinduliwa mwaka 2024, zikilenga kukuza uelewa wa hakimiliki kwa kutambua waandishi wanaohamasisha umma kuhusu umuhimu wa ulinzi wa kazi zao.
Pia zinahamasisha ubora wa uandishi unaobadilisha mitazamo, kueleza masuala mapya ya hakimiliki, na kuipa hakimiliki nafasi muhimu katika maendeleo ya Afrika.
Tuzo hizi ziko wazi kwa waandishi kutoka nchi 22 wanachama wa ARIPO, ambao hutuma kazi zao za kidijitali, magazetini, redioni au televisheni kupitia mfumo maalumu mtandaoni.
Jopo la majaji huchambua kazi zote na kuchagua washindi watatu bora kwa kuzingatia ubora, uelewa na mchango katika kuelimisha jamii kuhusu hakimiliki.
Ushindi huu wa Nukta Africa ambayo inaboresha maisha kwa kutumia takwimu, mafunzo na maudhui ya kidijitali unaonyesha umahiri wake wa uandishi wa habari zenye maslahi mapana kwa umma.
Latest