Rais Samia aitwika zigo zito tume ya kuchunguza yaliyotokea Oktoba 29

November 20, 2025 2:02 pm · Fatuma Hussein
Share
Tweet
Copy Link
  • Aipa tume jukumu la kuchunguza chanzo cha vurugu na madai ya haki za vijana.
  • Aitaka tume ichunguze malalamiko ya uchaguzi, matamshi ya upinzani na ufadhili wa maandamano.

Dar es Salaam. Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, ameizindua rasmi tume ya uchunguzi ya matukio ya uvunjifu wa amani yaliyojitokeza wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025, na kuikabidhi jukumu zito la kubaini sababu za matukio hayo.

Majukumu hayo yanayotarajiwa kutekelezwa na tume hiyo yanaanza ikiwa ni siku tano tangu Rais Samia atoe ahadi hiyo alipokuwa akihutubia Bunge kwa mara kwa kwanza katika awamu ya pili ya uongozi wake Novemba 14 mwaka huu.

Rais Samia aliyekuwa akizungumza katika hafla ya uzinduzi iliyofanyika leo Novemba 20, 2025 jijini Dodoma, amesema anatambua ukubwa wa kazi hiyo, lakini ana imani kuwa wajumbe walioteuliwa wana weledi na uzoefu wa kuibeba.

“Mpaka mmefika hapa kuja kusikiliza majukumu na kuzinduliwa ina maana mmekubali kubeba mzigo huu… tunajua ni mzigo mzito tumekupeni lakini kwa sifa zilizotajwa hapa tunajua mtaweza kwenda kuutekeleza,” amesema Rais Samia.

Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan akiwa na Katibu Mkuu Kiongozi Balozi DkMoses Kusiluka, Mwenyekiti wa Tume Huru ya Uchunguzi wa Matukio ya Uvunjifu wa Amani, Jaji Mkuu Mstaafu wa Mahakama ya Tanzania Mohamed Chande Othman katika picha ya pamoja na Wajumbe wa Tume hiyo, Ikulu Chamwino. Picha/ CCM Tanzania.

Kwa mujibu wa kiongozi huyo wa nchi, tume hiyo inapaswa kuchunguza kiini cha vurugu na malalamiko yaliyowasukuma vijana kuingia mitaani, ikiwemo kubaini ni haki gani waliyoamini wameikosa. 

“Tunatarajia ikatuangalizie sababu hasa iliyoleta kadhia ile ni nini? Kiini cha tatizo ni nini? Na wakati inatokea kadhia ile vijana waliingizwa barabarani kudai Haki? Tunataka kujua haki gani? Ambayo vijana hawa wamekosa…ili tuweze kuifanyia kazi na wapate haki yao,’’ amesema Rais Samia akiilekeza tume hiyo.

Aidha, ameitaka tume kuchambua matamshi ya baadhi ya vyama vya upinzani na kuchunguza uhusiano wao na Tume Huru ya Uchaguzi katika kipindi hicho pamoja na madai ya vijana walioandamana kulipwa.

“Lakini niseme hata kama kulikuwa na changamoto baina ya tume na vyama vya siasa, Msajili na vyama vya siasa, Serikali na vyama vya siasa, je hakukuwa na njia nyingine? Na njia ilikuwa ile moja peke yake ya kuingia kuchafua nchi, kuchoma nchi kusababisha vifo kwa wananchi…,” ameongeza Rais Samia.

Kwa mujibu wa Rais Samia, tume hiyo itachunguza pia namna vyombo vya dola vilivyokabiliana na vurugu hizo, ikiwemo kuchambua hatua zilizochukuliwa na athari zake.

Itakumbukwa kuwa kuanzia Oktoba 29, mwaka huu maeneo mbalimbali ya Tanzania yaliripoti vurugu na ghasia zilizosababisha vifo vya watu, majeruhi na uharibifu wa miundombinu, mali za umma na binafsi  zilizopelekea kusimama kwa shughuli mbalimbali nchini.

Baada ya kutokea kwa matukio hayo vyombo mbali vya utetezi wahaki za binadamu kutoka ndani na nje ya nchi vimekuwa vikishinikiza kufanyika kwa uchunguzi huo kuhusu uvunjifu wa haki za binadamu uliojitekeza.

Rais wa Tanzanai Samia Suluhu Hassan akizungumza na viongozi mbalimbali Ikulu Chamwino mkoani Dodoma. Picha/CCM Tanzania.

Hata hivyo, Rais Samia amesema kuwa ni muhimu kufanya uchunguzi wa ndani kabla ya kuomba msaada kutoka kwa jumuiya ya kimataifa kama UN au Umoja wa Ulaya (EU).

Matokeo ya tume hiyo yanatarajiwa kuwa msingi wa majadiliano ndani ya Tume ya Maridhiano aliyoiahidi kuanzishwa ndani ya siku 100 tangu aingie madarakani. 

Licha ya uzinduzi huo kufanyika leo, Serikali pia imeahidi kuiwezesha tume hiyo kwa vifaa, sekretarieti na muda wa kutosha kwa kuanzia miezi mitatu ili kuhakikisha uchunguzi unafanyika kwa uadilifu na ushahidi wa kutosha.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Follow Us on TikTok

Subscribe to Our YouTube Channel

Subscribe

Loading videos...

Loading videos...

Loading videos...

Enable Notifications OK No thanks