Saba wateuliwa kuchunguza vurugu zilizotokea baada ya uchaguzi
- Wanaounda wa Tume hiyo ni viongozi na wataalamu waliowahi kushika nyadhifa za juu serikalini, kwenye vyombo vya ulinzi na usalama pamoja na diplomasia.
Dar es Salaam. Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, ameunda tume ya watu saba kuchunguza matukio ya uvunjifu wa amani yaliyotokea nchini wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu uliofanyika Oktoba 29, 2025.
Tume hiyo inaundwa ikiwa ni siku tatu tangu Rais Samia atoe ahadi hiyo alipokuwa akihutubia Bunge kwa mara kwa kwanza katika awamu ya pili ya uongozi wake Novemba 14 mwaka huu.
Taarifa ya Katibu Mkuu Kiongozi Dk Moses Kusiluka, iliyotolewa leo Novemba 18, 2025 inabainisha kuwa tume hiyo imeundwa kwa mujibu wa mamlaka ya Rais chini ya kifungu cha 3 cha Sheria ya Tume za Uchunguzi, Sura ya 32.
“Mheshimiwa Mohamed Chande Othman, Jaji Mkuu Mstaafu wa Mahakama ya Tanzania ameteuliwa kuwa Mwenyekiti wa tume hiyo,” imesema taarifa ya Dk Kusiluka.
Wajumbe wengine wanaounda tume hiyo ni pamoja na Jaji Mkuu Mstaafu wa Mahakama ya Tanzania, Profesa Ibrahim Hamis Juma, pamoja na Dk Stergomena Lawrence Tax, aliyewahi kuwa Katibu Mtendaji wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).
Aidha, Rais Samia amewateua wanadiplomasia wengine akiwemo Balozi Ombeni Yohana Sefue, Balozi Mstaafu, Balozi Radhia Msuya, Balozi Mstaafu, Lt. Gen. Paul Meela, Balozi Mstaafu, David Kapya pamoja na aliyekuwa Mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania, IGP mstaafu, Said Ally Mwema kuunda tume hiyo.
Pamoja na jitihada hizo tayari mashirika mbalimbali ya kimataifa yalitoa wito huku mengine yakiahidi kuanza kufanya uchunguzi wa kilichotokea wakati na baada ya uchaguzi nchini Tanzania ikiwemo Umoja wa Mataifa (UN).
Hata hivyo, taarifa hiyo haijaweka wazi ni lini tume hiyo itaanza rasmi kazi hiyo pamoja na muda utakaotumika kuikamilisha na kuwasilisha ripoti ya uchunguzi kwa Rais Samia.
Itakumbukwa kuwa kuanzia Oktoba 29, mwaka huu maeneo mbalimbali ya Tanzania yaliripoti vurugu na ghasia zilizosababisha vifo vya watu, majeruhi na uharibifu wa miundombinu, mali za umma na binafsi zilizopelekea kusimama kwa shughuli mbalimbali nchini.
Siku chache baadae Rais Samia alitoa salamu za rambirambi kwa waliopoteza maisha katika vurugu hizo huku akiagiza baadhi ya vijana walioshikiliwa na Jeshi la Polisi wakihusishwa na vurugu hizo kuachiliwa.
Latest