INEC yatangaza ratiba mpya uchaguzi udiwani Kata za Mindu, Mzinga, Kirua

October 24, 2025 3:05 pm · Fatuma Hussein
Share
Tweet
Copy Link
  • Uchaguzi katika kata hizo kufanyika Jumatano Januari 5, 2026.
  •  Uteuzi mpya hautahusisha mgombea mwingine yeyote aliyeteuliwa kihalali katika uteuzi uliofanyika awali.

Dodoma.Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) imetangaza mabadiliko ya ratiba ya uchaguzi wa madiwani katika Kata ya Mindu (Jimbo la Morogoro Mjini), Kata ya Mzinga (Jimbo la Kivule) na Kata ya Kirua Vunjo Magharibi (Jimbo la Vunjo).

Uamuzi huo umetokana na vifo vya wagombea watatu waliokuwa wakiwania nafasi za udiwani katika kata hizo.

Taarifa iliyotolewa leo Oktoba 24, 2025 na Mkurugenzi wa Uchaguzi wa INEC, Ramadhani Kailima, imeeleza kuwa kwa mujibu vifungu vya sheria ya uchaguzi wa Rais, wabunge na madiwani ya mwaka 2024, uchaguzi katika jimbo hilo ulisitishwa rasmi Oktoba 21, 2025.

Taarifa hiyo, imebainisha kuwa fomu za uteuzi katika kata hizo zitatolewa Oktoba 28, 2025 hadi Novemba 3,2025 kwa wagombea udiwani wa Chama cha mapinduzi (CCM), Chama cha The Civic United Front (CUF), na Chama cha ACT Wazalendo.

Baada ya uchukuaji wa fomu hizo, siku hiyo hiyo ya Novemba 3 kutafanyika uteuzi wa mgombea kupitia vyama hivyo.

Kulingana na taarifa hiyo, kampeni za uchaguzi wa madiwani katika kata hizo zitafanyika kuanzia Novemba 4, 2025 hadi Januari 4, 2026 na uchaguzi kufanyika siku ya Jumatano Januari 5, 2026.

Aidha, tume imefafanua kuwa uteuzi mpya hautahusisha mgombea mwingine yeyote aliyeteuliwa kihalali katika uteuzi uliofanyika awali isipokuwa kama atatoa taarifa ya kujitoa.

Wagombea hao waliofariki ni pamoja na Hamisi Mohamedi Msasa (ACT-Wazalendo) aliyefariki Oktoba 17,2025, Rashid Abdallah Nandonde (CUF) Oktoba 19, 2025 na John Boniface Kessy (CCM) aliyefariki Oktoba 21, 2025.

Aidha, tume imevikumbusha vyama vya siasa, wagombea na wadau wa uchaguzi kuendelea kuzingatia katiba ya Tanzania, sheria za uchaguzi, kanuni, maadili, taratibu, miongozo na maelekezo yatakayotolewa na tume katika kufanikisha ratiba ya uchaguzi husika.

Taarifa hii ya INEC inakuja ikiwa zimebaki siku tano pekee zoezi la upigaji kura kuchukua nafasi yake ifikapo Oktoba 29, 2025.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Follow Us on TikTok

Subscribe to Our YouTube Channel

Subscribe

Loading videos...

Loading videos...

Loading videos...

Enable Notifications OK No thanks