TCU yakamilisha awamu ya tatu ya udahili wa shahada ya kwanza 2025/2026

October 20, 2025 3:13 pm · Fatuma Hussein
Share
Tweet
Copy Link
  • Waombaji waliopata nafasi katika zaidi ya chuo kimoja wanatakiwa kuthibitisha chuo watakachosoma kati ya Oktoba 20, hadi  Novemba 3, 2025.

Dar es Salaam. Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) imetangaza kukamilika kwa awamu ya tatu na ya mwisho ya udahili wa wanafunzi wa shahada ya kwanza kwa mwaka wa masomo 2025/2026 katika vyuo vya elimu ya juu nchini.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Oktoba 20,2025 na Katibu Mtendaji wa TCU, Prof Charles Kihampa imeeleza kuwa majina ya waombaji waliodahiliwa katika awamu ya tatu yametangazwa na vyuo husika kupitia tovuti zao na njia nyingine rasmi za mawasiliano.

“Udahili katika awamu ya tatu na ya mwisho kwa ngazi ya shahada ya kwanza katika Taasisi za Elimu ya Juu nchini kwa mwaka wa masomo 2025/2026 umekamilika,” amesema Prof Kihampa.

Taarifa hii ya TCU inakuja wiki mbili baada ya kupokea maombi ya kuongezwa kwa muda wa kutuma maombi ya udahili kutoka kwa Jumuiya ya Wanafunzi wa Taasisi za Elimu ya Juu Tanzania (TAHLISO) na Vyuo vya Elimu ya Juu kwa ajili ya waombaji ambao hawakufanikiwa kupata udahili katika awamu zilizopita na kwa programu ambazo bado zina nafasi.

Kulingana na TCU, waombaji waliopata nafasi katika zaidi ya chuo kimoja wanatakiwa kuthibitisha chuo watakachosoma kati ya Oktoba 20, hadi  Novemba 3, 2025.

Aidha, taarifa hiyo imefafanua kuwa uthibitisho huo utafanyika kwa kutumia namba maalum ya siri (confirmation code) iliyotumwa kupitia ujumbe mfupi au barua pepe iliyotumika wakati wa kuomba udahili.

“Wale ambao hawatapata kwa wakati ujumbe huo, wanashauriwa kuingia kwenye mifumo ya udahili ya vyuo walivyodahiliwa na kuomba namba hiyo ili kuweza kujithibitisha katika chuo husika,’’ ameongeza Prof Kihampa.

Hata hivyo, waombaji wanatakiwa kufanya uthibitisho kupitia akaunti zao binafsi walizotumia wakati wa kuomba nafasi za masomo huku orodha ya majina ya waliodahiliwa katika zaidi ya chuo kimoja inapatikana kupitia tovuti ya TCU: www.tcu.go.tz.

Vile vile, TCU imewakumbusha waombaji wote wa shahada ya kwanza kuwa masuala yote yanayohusu udahili au uthibitisho wa chuo yawasilishwe moja kwa moja katika vyuo husika.

Tume imetoa rai kwa waombaji wote kuhakikisha wanakamilisha uthibitisho wao ndani ya muda uliopangwa ili kuepuka kupoteza nafasi zao za masomo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Follow Us on TikTok

Subscribe to Our YouTube Channel

Subscribe

Loading videos...

Loading videos...

Loading videos...

Enable Notifications OK No thanks