Mpina akwama mahakamani, ndoto za Urais 2025 zayeyuka

October 15, 2025 3:47 pm · Kelvin Makwinya
Share
Tweet
Copy Link
  • Ni baada ya Mahakama Kuu Masjala Kuu Dodoma kusema Inec haipaswi kuingiliwa na chombo chochote.
  • ACT Wazalendo yasema inakusudia kukata rufaa ikishirikisha wadau wa kimataifa na kitaifa.

Dar es Salaam. Mahakama Kuu Masjala Kuu Dodoma imeitupa kesi ya Luhaga Mpina na ACT-Wazalendo, ikieleza kwa mujibu wa Sheria na Katiba ya nchi, Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) haipaswi kuingiliwa na chombo chochote kwa jambo ambalo ilifanya kwa nia njema.

Mpina alikuwa akipinga kuenguliwa katika nafasi ya kugombea urais katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025.

Uamuzi huo umetolewa leo Jumatano Oktoba 15, 2025 mbele ya mahakama hiyo na kiongozi wa jopo la majaji wanaosikiliza kesi hiyo Jaji Fredrick Manyanda. Majaji wengine waliosikiliza kesi hiyo ni Sylvester Kainda na Abdallah Gonzi.

Kwa uamuzi huo, Mpina hataweza kushiriki kinyang’anyiro cha uchaguzi mkuu, ambao kwa sasa vyama vya siasa vinavyoshiriki vinaendelea na kampeni.

Hata hivyo, Chama cha ACT Wazalendo kimetangaza kuchukua hatua za kisheria ikiwemo kukata rufaa ya uamuzi huo.

Taarifa ya Mwanasheria Mkuu wa ACT iliyotolewa muda mchache baada ya hukumu hiyo imebainisha kuwa  sambaba na kukata rufaa ya uamuzi huo  ACT itawashirikisha wadau wa ndani na nje ya nchi ili kuendelea kupigania mabadiliko ya kisheria na kikatiba katika mchakato wa uchaguzi.

Aidha, ACT Wazalendo imewashukuru wanachama na wafuasi wake kwa mshikamano na kujitoa wakati wote wa mashauri hayo na kuwataka kuwa watulivu, wamoja, na kuendelea kujielekeza kwenye mapambano ya demokrasia na haki. 

“Tubaki wamoja na safari inaendelea” imeeleza taarifa hiyo.

Hii ni kesi ya pili kwa Mpina ndani ya mwezi mmoja akipigania haki yake ya kugombea Urais katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29. 

Awali Mpina alienda mahakamani kupinga uamuzi wa INEC kumzuia kurejesha fomu za kuwania kiti hicho na Mahakama Kuu ilimpa ushindi. 

Hata hivyo, siku moja baada ya kurejesha fomu na kuteuliwa kuwania Urais, INEC ilimuondoa tena kwenye orodha ya wagombea baada ya kupokea pingamizi kutoka kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Hamza Johari.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Follow Us on TikTok

Subscribe to Our YouTube Channel

Subscribe

Loading videos...

Loading videos...

Loading videos...

Enable Notifications OK No thanks