Dk Mpango ataja mambo manne Watanzania kumuenzi Mwalimu Nyerere

October 14, 2025 3:22 pm · Kelvin Makwinya
Share
Tweet
Copy Link
  • Asema misingi iliyowekwa na Mwalimu Nyerere isipozingatiwa itahatarisha umoja wa Taifa.

Dar es Salaam. Makamu wa Rais wa Tanzania, Dk Mpango amewataka Watanzania kumuenzi Mwalimu Nyerere kwa mambo manne ikiwemo kulinda uhuru wa Taifa letu pamoja na kudumisha umoja na amani.

Dk Mpango aliyekuwa akizungumza leo Oktoba 14, 2025 jijini Mbeya wakati wa maadhimisho ya kumbukizi ya Mwalimu Nyerere, amesema siku ya leo ni muhimu kwa Watanzania wote kwa kuwa ni wakati wa kutafakari mchango mkubwa alioutoa katika ujenzi wa Taifa kisiasa, kijamii na kiuchumi.

Pamoja na mambo mengine katika kumuenzi Hayati Nyerere, Dk Mpango amewataka Watanzania kusimamia haki miongoni mwa jamii akisisitiza kuwa kutofanya hivyo kwa dhati kunaweza kuleta hatari ya Taifa kusambaratika.

“Tunapofanya kumbukizi ya Mwalimu Nyerere, tunasheherekea maisha yake ambayo aliyatoa katika kulitumikia Taifa letu alilolipenda sana,” amesema Dk. Mpango ambaye alimuwakilisha Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan.

Aidha, Dk Mpango amewataka Watanzania kumuenzi Mwalimu Nyerere kwa kujenga na kuimarisha maadili mema katika jamii hasa miongoni mwa vijana ambao ni Taifa la sasa na kesho.

“Ni lazima kukemea mmomonyoko wa maadili ikiwemo rushwa na ufisadi ambavyo baba wa Taifa alivichukia sana na kuvipiga vita kwa vitendo” amesisitiza Dk Mpango.

Mambo mengine aliyosisitiza Dk Mpango ni kufanya kazi kwa bidii ili kuboresha maisha na kuinua vipato pamoja na uhifadhi wa mazingira hasa kulinda vyanzo vya maji, upandaji wa miti na kufanya usafi wa mazingira.

Kila mwaka Tanzania huadhimisha siku ya kumbukizi ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, tarehe 14 Oktoba, ikiwa ni siku maalumu ya kumkumbuka kiongozi huyo kwa mchango wake mkubwa katika ujenzi wa Taifa na harakati za ukombozi wa Afrika. 

Maadhimisho hayo hufanyika kwa lengo la kutafakari maisha, fikra na misingi aliyoiweka katika uongozi, ikiwemo umoja, utu, usawa na uzalendo. 

Mwaka huu, 2025, Taifa linaadhimisha miaka 26 tangu kifo cha Mwalimu Nyerere, kilichotokea tarehe 14 Oktoba 1999 katika Hospitali ya Mtakatifu Thomas, London, nchini Uingereza ambazo zimefanyika sambamba na kilele cha kuzimwa kwa mbio za Mwenge wa Uhuru.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Follow Us on TikTok

Subscribe to Our YouTube Channel

Subscribe

Loading videos...

Loading videos...

Loading videos...

Enable Notifications OK No thanks