WHO: Watu zaidi ya milioni 300 duniani wanahitaji msaada wa afya ya akili
- Waathirika wakubwa ni makundi yenye mahitaji maalum ikiwemo wakimbizi.
- Mtalaamu wa saikolojia asisitiza kutumia busara na lugha ya upendo kuwasaidia.
Dar es Salaam. Wakati dunia inaadhimisha siku ya Afya ya Akili Shirika la Afya Duniani (WHO) limesema zaidi ya watu milioni 300 wanahitaji huduma za afya ya akili na msaada wa kisaikolojia kutokana na athari za migogoro, mabadiliko ya tabianchi na majanga ya asili.
Idadi hiyo ni ya wale waliopata matatizo hayo katika mwaka 2025 pekee ikiwaathiri zaidi makundi yenye mahitaji maalum ikiwemo wakimbizi.
Nchini Tanzania matatizo hayo ya afya akili yamechangiwa na majanga ya asili yaliyotokea hivi karibuni ikiwemo mafuriko na maporomoko ya ardhi yalitokea Hanang mkoani Manyara mwaka 2023.
Maporomoko hayo yaliathiri watu watu zaidi ya 5,600 na kuwasababishia baadhi kukosa chakula,makazi na hata kupoteza maisha suala lilipolekea matatizo ya afya ya akili.
Taarifa ya Mganga Mkuu wa Serikali Grace Magembe iliyotolewa leo Oktoba 10, 2025 inabainisha kuwa ilitoa msaada kwa waathirika mkoani humo pamoja na majanga mengine ikiwemo Covid 19.
“Serikali kwa kushirikiana na wadau iliwafikia watu 3,380 kwa msaada wa kisaikolojia na kijamiini jambo ambalo lilifanyika katika majanga mengine kama mlipuko wa COVID-19, Mpox, Marburg, na maporomoko ya majengo,”
Vilevile, Dk Magembe amesisitiza kuwa ,Serikali imeendelea kuimarisha utoaji wa huduma za afya ya akili nchini ikiwemo kuanzisha madawati ya msaada wa kisaikolojia pamoja na kuwajengea uwezo wahudumu wa afya ngazi ya msingi.
“Kushirikiana na viongozi wa dini, vyombo vya habari, na mashirika ya kijamii katika kutoa elimu kwa umma na kupambana na unyanyapaa dhidi ya watu wenye changamoto za afya ya akili,’’ imeeleza taarifa ya Dk Magembe.
Jinsi ya kumsaidia mtu anayepitia changamoto ya afya ya akili
Mtaalam wa Saikolojia na Mahusiano kutoka mkoani Tanga Leyla Abubakari anaeleza kuwa kumsaidia mtu mwenye changamoto ya afya ya akili kunahitaji huruma, subira na uelewa.
“Mara nyingi, huogopa kuonyesha udhaifu kwa sababu ya matarajio ya kijamii, hivyo ni muhimu kumsaidia kwa njia nyeti na yenye staha. Msikilize bila hukumu, hii ni pamoja na kumpa nafasi ya kuongea bila kumkatiza.Hivyo, mweleze kwamba ni sawa kutokuwa sawa.,” amesema Abubakari
Kwa mujibu wa Abubakari, ni muhimu pia kumuonyesha msaada wa kihisia, kumzalia mazingira salama pamoja na kumsidia kutafuta msaada wa kitaalamu.
“Ili mtu aliye na changamoto ya afya ya akili ajisikie salama na huru kueleza hisia zake, ni muhimu kutomlazimisha kuzungumza bali kumshawishi kwa upole na subira. Unapaswa kuepuka kumkosoa au kumcheka anapojaribu kujieleza, hata kama maelezo yake hayaeleweki kikamilifu,” anafafanua Abubakari
Njia nyingine ni kubadilisha mtazamo kuhusu afya ya akili, hapa ni muhimu kueleza kwa kwa njia rahisi kwamba afya ya akili ni kama afya ya mwili mtu yeyote anaweza kuathirika bila kujali hali yake ya kijamii au kiumri.
Vile vile, kumuhamasisha kwa shughuli zenye afya na kumuepusha na mazingira hatarishi ikiwa ni pamoja na kuepuka matumizi ya pombe kupita kiasi, dawa za kulevya, au watu wanaomkatisha tamaa kwani vitu hivi vinaweza kuzidisha hali yake ya kihisia.
“Badala yake, msaidie kuanzisha ratiba bora ya maisha inayojumuisha usingizi wa kutosha, lishe bora na muda wa kupumzika ili kusaidia afya yake kwa ujumla,” ameeleza Abubakari.
Latest



