Polisi Tanzania wachunguza madai ya kutekwa Polepole
- Lasema bado linamsubiri aripoti katika ofisi ya DCI.
Arusha. Jeshi la Polisi Tanzania limesema linachunguza madai ya kutekwa kwa aliyekuwa Balozi wa Tanzania nchini Cuba, Humphrey Polepole, siku moja baada ya ndugu zake kueleza kuwa ametekwa na watu wasiojulikana.
Habari za kutekwa kwa Polepole, ambaye amekuwa akitumia mitandao ya kijamii kukosoa mwenendo wa Chama cha Mapinduzi (CCM) na Serikali, zilianza kusambaa Oktoba 6 asubuhi baada ya moja ya ndugu zake kueleza taarifa hizo mtandaoni.
Katika taarifa yake kwa umma, Msemaji wa Jeshi la Polisi, David Misime amesema bado wanaendelea kumsubiri aripoti katika Ofisi ya Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI).
Ndani ya miezi mitatu ya hivi karibuni, Polepole amekuwa akiikosoa vikali Serikali kwa nyakati tofauti hatua iliyowafanya polisi kumtaka kufika ofisini kwa DCI ili kutoa maelezo kuhusiana na tuhuma hizo.
Mmoja wa ndugu zake Godfrey Polepole ameliambia Shirika la Habari la Uingereza (BBC Swahili) kuwa walijulishwa na mwenye nyumba kuhusu iwapo wanajua tukio lilotokea nyumbani kwa Polepole.
Godfrey amesema wamekuta damu nyingi nyumbani kwa Polepole na tayari wamesharipoti tukio hilo katika kituo cha polisi Mbweni.
“Jeshi la Polisi limeona taarifa zinazosambazwa kwenye mitandao ya kijamii na ndugu zake kuwa ametekwa, tayari tumeanza kufanyia kazi taarifa husika ili kupata ukweli wake,” amesema Misime, leo Oktoba 6, 2025.
Polepole alitangaza kujiuzuru katika nafasi yake ya ubalozi Julai 13 mwaka huu kwa madai ya kukiukwa kwa misingi ya haki.
Wiki chache baadae Rais Samia alitengua rasmi uteuzi wa balozi huyo kupitia barua rasmi ya Balozi Dk Moses Kusiluka, Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.
Habari hii imeboreshwa na kuongezwa muktadha zaidi
Latest



