Mpango aitaka Afrika kuimarisha ufadhili endelevu wa sekta ya afya

September 23, 2025 6:20 pm · Kelvin Makwinya
Share
Tweet
Copy Link

Dar es Salaam. Makamu wa Rais wa Tanzania, Dk Philip Mpango, amelitaka bara la Afrika kuimarisha ufadhili endelevu wa sekta ya afya ili kukabiliana na dharura za kiafya zinazoweza kujitokeza.

Dk Mpango ameyasema hayo wakati akizungumza katika Mkutano wa Kamati ya Wakuu wa Nchi na Serikali wa Kituo cha Kuzuia na Kudhibiti Magonjwa Afrika (CDC) uliofanyika jijini New York Marekani.

Akizungumza katika mkutano huo Dk Mpango amebainisha kuwa Serikali ya Tanzania inaunga mkono mipango ya kikanda inayopunguza utegemezi wa misaada kutoka nje ili kuhakikisha vipaumbele vya afya barani Afrika vinashughulikiwa na Waafrika wenyewe.

Dk. Mpango amesema milipuko ya magonjwa ya kuambukiza, ikiwemo homa ya Marburg, imeonesha umuhimu wa maandalizi ya haraka na mifumo imara ya afya. Picha | Ofisi ya Makamu wa Rais.

Dk. Mpango amesisitiza pia umuhimu wa kuwekeza katika uzalishaji wa ndani wa vifaa vya uchunguzi, matibabu na bidhaa muhimu za kiafya mkakati ambao utalisaidia bara la Afrika kujitegemea huku akihimiza kuanzishwa kwa viwanda vya ndani, mamlaka za udhibiti za pamoja na ubia wa uhawilishaji teknolojia ili kuongeza uwezo wa nchi za Afrika katika kukabiliana na changamoto za kiafya za sasa na zijazo.

Akirejea tukio la hivi karibuni, Dk. Mpango amesema milipuko ya magonjwa ya kuambukiza, ikiwemo homa ya Marburg, imeonesha umuhimu wa maandalizi ya haraka na mifumo imara ya afya. 

Aidha, amesema kuwa Tanzania imeendelea kuimarisha vitengo vya matibabu ya magonjwa ya mlipuko, kupeleka timu za dharura kwa haraka pamoja na kuwekeza katika miundombinu ya afya na wataalamu wake.

“Ni muhimu kuimarisha nguzo zote za dharura za afya ya umma, kuanzia ufuatiliaji wa magonjwa, maabara, udhibiti wa maambukizi, vifaa hadi uratibu wa haraka…hatua hizi ndizo zitakazowezesha kukabiliana na milipuko kwa wakati na ufanisi,” amesema Dk Mpango.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Follow Us on TikTok

Subscribe to Our YouTube Channel

Subscribe

Loading videos...

Loading videos...

Loading videos...

Enable Notifications OK No thanks