Jiji la Arusha laadhimisha siku ya usafi wa mazingira duniani kwa kufanya usafi

September 20, 2025 2:01 pm · Lucy Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Yawataka wananchi kutunza mazingira na kuzipa taka thamani.

Arusha. Wananchi pamoja na viongozi wa Halmashauri ya Jiji la Arusha wameshiriki zoezi la usafi katika maeneo mbalimbali ya jiji hilo ikiwa ni sehemu ya kuadhimisha siku ya usafi wa mazingira duniani.

Siku ya usafi wa mazingira duniani inayoadhimishwa Septemba 20 kila mwaka ni sehemu ya jitihada za dunia kupunguza uchafu na kutoa elimu ya utunzaji wa mazingira.

Mkurugenzi wa jiji la Arusha John Kayombo aliyekuwa akihitimisha zoezi hilo leo Septemba 20, 2025 amesema kuwa maadhimisho ya mwaka huu yamelenga kuzipa taka thamani.

“Tunataka twende kwenye lengo la kuhakikisha kwamba sio kila kitu kinatupwa, vitu vingine vinachukuliwa na kwenda kwenye matumizi mbadala wa taka.

Tunatambua karatasi, maboksi, plasitiki, chupa zote zinaweza zikarejerezwa na kutumika tena zikawa na thamani badala ya kuwa taka tunataka twende huko na ndiyo lengo la maadhimisho ya siku hii,” amesema Kayombo.

Zoezi hilo la kusafisha jiji la Arusha lilianzia Mianzini mpaka soko la stendi kuu ya mabasi ya jiji hilo, huku likitekelezwa pia katika halmashauri nyingine ikiwemo Halmashauri ya Wilaya ya Arusha waliosafisha soko la Ngaramtoni.

Viongozi pamoja na wananchi wakiendelea na usafi jijini Arusha.Picha/ Halmashauri Jiji la Arusha.

Licha ya kuadhimisha siku hiyo ya usafi wa mazingira jiji hilo limejiwekea utaratibu wa kufanya usafi kila Jumamosi ya mwisho wa mwezi hatua inayotajwa kupendezesha mandari ya jiji hilo linalosifika kwa utalii.

Nukta Habari imepita baadhi ya maeneo ya pembezoni ma jiji hilo ikiwemo  soko la Kilombero, Mbauda na Morombo na kujionea hali ya usafi iliyopo katika maeneo huku baadhi ya watu wakiendelea kufanya usafi.

Aidha, Wananchi walioshiriki katika zoezi hilo wamesema utaratibu huo unapaswa kuendelezwa ili kuhakikisha jiji hilo linakuwa safi wakati wote.

“Nashukuru zoezi limeenda vizuri hakuna changamoto yoyote, mimi naona zoezi hili liendelee kwa sababu linaacha mazingira yetu safi,” amesema Zaina Bakari.

Kwa upande wake Mkuu wa Idara ya Utawala na Usimamizi wa Rasilimaliwatu Halmashauri ya Jiji la Arusha Debora Manase amewashukuru wananchi kwa kujitoa kusafisha viunga vya jiji hilo akiwasihi kuendelea kutunza mazingira na kuzipa taka thamani.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Follow Us on TikTok

Subscribe to Our YouTube Channel

Subscribe

Loading videos...

Loading videos...

Loading videos...

Enable Notifications OK No thanks