Wafahamu wanawake 10 vinara wa mapinduzi ya kilimo Afrika
- Wanawake hao ni wale walioshinda tuzo za YAWA 2025.
Arusha. Shirika la Mapinduzi ya Kijani Afrika (AGRA) kupitia mpango wa VALUE4HER imetoa tuzo kwa wanawake 10 wabunifu wa sekta ya kilimo ili kutambua mchango wao katika sekta hiyo muhimu barani Afrika.
Hafla ya utoaji wa tuzo hizo zilizopewa jina la Women Agripreneurs of the Year Awards (WAYA) imefanyika Dakar, Senegal Septemba 12, 2025 ikiwatambua wanawake hao kutoka maeneo mbalimbali barani Afrika.
Alice Ruhweza, Rais wa AGRA, aliyekuwa akizungumza katika hafla ya ugawaji wa tuzo hizo amesema wanawake hao wamestahili kupata tuzo hizo kutokana na mchango wao katika kukuza kipato na kupunguza uharibifu wa mazao hususani ya chakula.
“Kwa pamoja, wameongeza kipato cha kila mwaka kwa wastani wa asilimia 35, wameokoa mamilioni ya tani za mazao dhidi ya kuharibika na kufikisha chakula kwa zaidi ya kaya 500,000.
Jukumu letu ni kuwaunga mkono kwa sera madhubuti, fedha na upatikanaji wa masoko makubwa zaidi ili kuleta mabadiliko ya kimfumo.” amesema Ruhweza.
Washindi wa WAYA 2025 walitambuliwa kutoka vipengele mbalimbali katika mnyororo wa thamani wa kilimo akiwemo Mathildah Amollo kutoka nchini Kenya ambaye ni mmiliki kampuni ya Greatlakes Feeds inayozalisha vifaranga vya samaki na chakula cha samaki rafiki kwa mazingira.
Kampuni ya Matilda inatoa asilimia 70 ya malighafi kwa wakulima ikiwemo vifaranga vya samaki pamoja na mkopo wa pembejeo jambo linalowawezesha kufuga kibiashara.
Misaada hiyo imeweza kupunguza vitendo vya unyasaji wa kingono kwa wanawake katika mwambao wa Ziwa Victoria pamoja na na utapiamlo.

Mathildah Amollo kutoka nchini Kenya ndiye mshindi wa jumla wa tuzo za YAWA kwa mwaka 2025.Picha/ AGRA.
Juliet Kakwerre Tumusiime
Tuzo ya YAWA katika kipengele cha mwanamke bingwa wa uwezeshaji imeenda kwa Juliet kutoka Uganda ambaye ni mwanzilishi na Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya Cheveux Organique.
Kampuni hiyo ni miongoni mwa kampuni za mwanzo Afrika kutengeneza nywele za bandia kutoka kwenye nyuzi za migomba na kutoa ajira kwa wanawake zaidi ya 2,000 wa vijijini nchini Uganda.
Julienne Olawolé Agossadou
Tuzo ya kipengele cha kiongozi jasiri mwenye msukumo imeenda kwa Julienne kutoka Benin ambaye ni mwanzilishi wa kampuni ya ‘SEDAMI La Reine des Champignons ambayo hubadilisha pumba za mpunga kuwa shamba la uyoga, hatua inayooneza kipato na lishe bora kwa wanawake wa vijijini.
Roberta Edu-Oyedokun
Roberta ni mshindi wa kipengele cha biashara bora ya uongezaji thamani kutokea nchini Nigeria ambaye pia ni mwanzilishi wa kampuni ya Moppet Foods inayoongozwa na wanawake
Kampuni hii huzalisha nafaka na siagi zenye virutubishi ili kukabiliana na utapiamlo, ikiwemo Moppet Nutriblend ambayo ni siagi ya kwanza duniani ya karanga yenye ladha ya matunda.
Joyce Waithira Rugano
Joyce ambaye ni mwanzilishi wa kampuni ya Ecorich Solutions kutoka nchini Kenya ametunukiwa tuzo ya mbunifu bora wa teknolojia ya kilimo kutokana na kugeuza taka za kikaboni kuwa mbolea.
Ecorich inafanya kazi na zaidi ya wanawake 400 wa ukusanyaji taka jijini Nairobi zinazochakatwa kupitia kifaa cha ‘WasteBot decomposer’ kinachoendeshwa kwa nishati ya jua na kusambaza mbolea kwa wakulima.

Roberta Edu (Pichani) ndiye mshinsi wa kipengele cha uongezaji thamani kutokea nchini Nigeria kupitia kampuni yake ya Moppet Food.Picha/AGRA.
Onicca Sibanyona
Onicca kutoka Afrika Kusini amechukua tuzo ya YAWA katika kipengele cha mwanamke mchanga anayechipukia katika kilimo kupitia kampuni yake ya Jwale Farms akiunga mkono uchumi vijijini kwa maji safi, chakula bora na mafunzo ya kilimo kinachozingatia mabadiliko ya tabianchi kwa vijana na wamama.
Pamoja na tuzo hizo, AGRA imewaja washindi wa kikanda wa tuzo hizo ikiwemo kanda ya Afrika Mashariki ambapo mshindi ni Arlène kutoka nchini Burundi ambaye ni mwanzilishi wa kampuni ya SEFACO inayoongeza ushiriki wa wanawake katika ufugaji wa samaki kupitia modeli ya Village-École des Femmes’.
Kwa upande wa Afrika Magharibi tuzo hiyo imechukuliwa na Baliqees Salaudeen-Ibrahim (Nigeria), Afrika ya Kati ni Elie Mbeki Busha Pongo (DRC), na Afrika ya Kusini ni Lusungu kutokea nchini Malawi.
Latest



