Hatua za kumuanzishia mtoto wa miezi sita chakula cha ziada
- Hatua hizo zimegawanyika katika wiki tatu.
- Mtoto huanza kupewa vijiko viwili hadi kufikia robo kikombe akifikisha mwaka mmoja.
Arusha. Lishe ni miongoni mwa mahitaji muhimu katika ukuaji wa mtoto ikimuwezesha kukua vyema na kumuepusha na magonjwa.
Katika miezi sita ya mwanzo wataalamu wa lishe hushauri mtoto apewe maziwa ya mama pekee bila kuchanganya na chochote ili kumpatia virutubisho vinavyohitajika katika hatua hiyo ya ukuaji.
Mwongozo wa lishe kwa watoto wadogo uliotolewa na Taasisi ya Chakula na Lishe (TFNC) unabainisha kuwa baada ya miezi sita ya mwanzo mtoto mchanga anahitaji chakula cha ziada ili kumpatia virutubisho ambavyo hupungua katika maziwa ya mama kadri mtoto anayokuwa.
“Vyakula vya nyongeza vinahitajika ili kumpatia mtoto nishati, vitamini na madini ambayo maziwa ya mama hayatoshelezi kadri mtoto anavyoendelea kukua,” umesema muongozo wa TFNC.
Mwongozo huo umebainisha kuwa mtoto anatakiwa kupata angalau makundi matatu ya chakula kwa kila mlo kati ya kundi la wanga, vyakula vya jamii ya kunde, mafuta na sukari, matunda na vile vyenye asili ya wanyama.
Hata hivyo, vyakula hivyo vya ziada hupaswa kuongezwa kwa hatua kadhaa ili mtoto aweze kuzoea na kurahisisha umengenywaji wake katika mfumo wa chakula wa mtoto.
Daktari Reinfrida Ngairo kutoka Taasisi ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR) ambaye pia ni mkufunzi wa lishe ya mama na mtoto ameimbia Nukta Habari kuwa hatua hizo zimegawanyika katika wiki tatu.

Ni muhimu kuzingatia uzito sahihi wa chakula cha mtoto ili aweze kuoata nishati na virutubisho vingine vya muhimu.Picha/Haakaa.
Wiki ya kwanza
Daktari Ngairo anasema mtoto anayeanzishiwa vyakula vya ziada huanza kupewa vyakula vyepesi (vya maji maji) kwa kiwango kidogo kisichozidi vijiko vitatu kwa siku mbili hadi tatu za mwanzoni.
“Lengo katika wiki ya kwanza ya kuanzisha chakula ni ku ‘introduce’ (kuitambulisha) tu ladha… kwa hiyo akila hata vijiko vitatu tu vinatosha akitaka zaidi ni sawa mpe zaidi na mlo mmoja unatosha kwa wiki ya kwanza.” ameongeza Dk Ngairo.
Vyakula hivyo ni pamoja na matunda yaliyopondwa na kuchanganywa na maziwa ya mama, maziwa ya kopo, au supu kama ndizi, parachichi, papai, embe na tikiti huku siku ya tatu na kuendelea mzazi akiruhusiwa kumpa mtoto uji mwepesi wa nafaka moja ikiwemo mahindi, mtama, ulezi au uwele
“Kuchanganya nafaka zote kwa pamoja, unauchosha mfumo wa tumbo na mtoto anaweza hata asiweze pata virutubisho vyote vnavyohitajika…
kuanzia siku ya tatu ile anapoanza uji unaweza anza pia vyakula vingine mfano bogalishe, mtori, rojo la karoti, viazi, mboga majani na viazi lishe,” amesema Dk Ngairo.
Wiki ya pili
Katika wiki ya pili baada ya mtoto kuzoea chakula Dk Ngairo anashauri kumuanzishia vyakula vinavyoweza kuleta mzio mara moja kwa siku ikiwemo karanga, samaki, kiini cha yai, ufuta na aina nyingine.
“Kwa hiyo hapa unaweza mpa mtoto asubuhi mtori wa supu ya samaki umeweka mnofu kdogo wa samaki ukasaga…unafaya hivi siku mbili au tatu mfululizo ili ujue kama kitampa shida au la,” ameongeza Dk Ngairo.

Wataalamu wa afya wanashauri mtoto apate angalau aina tatu za makundi ya chakula.Picha/Felix Hospital.
Wiki ya tatu
Kuanzia wiki ya tatu hadi mtoto atakapofikisha mwaka mmoja unaruhusiwa kuchanganya vyakula mfano ndizi, kiazi, supu na mboga za majani pia kumpa uji wa nafaka mbili, mbegu na karanga..
Mtoto anakiwa kupewa vyakula hivyo mara tatu au nne kwa siku pamoja na asusa kama sharubati nzito na matunda kati ya mlo na mlo bila kusahau kunyoshwa kila anapohitaji.
Mwongozo wa TFNC unabainisha kuwa kadri mtoto anavyoendelea kukua anatakiwa kumaliza kikombe au kibakuli cha ujazo wa mililita 250 kwa mlo mmoja huku akiendelea kuacha vyakula laini sana kwenda vyakula vilivyopondwa hadi kufikia vyakula vyenye vipande vya kutafuna
Dk Ngairo amewataka wazazi kuzingatia kutoweka chumvi wala sukari katika chakula cha mtoto hadi anapofikisha umri wa mwaka mmoja ili kulinda figo ya mtoto na kusaidia mtoto asipoteze hamu ya kula.
Hakikisha vyombo vya mtoto vinaoshwa ipasavyo huku chakula kikipikwa katika hali ya usafi ili kumuepusha na magonjwa pamoja na kuzingatia mbinu bora za ulishaji.
Latest



